Tuesday 21 October 2014

Mrema kawa mkali kama simba awavua uanachama wa TLP baadhi ya wanachama mamluki

MWENYEKITI wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, amekunjua upya makucha yake yaliyowahi kurarua viongozi wenzake akiwa katika NCCR-Mageuzi na TLP, na sasa amefukuza hadharani madiwani wawili wa chama chake waliounga mkono nia ya Mbunge wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ambaye ametangaza kugombea ubunge wa Vunjo.
Mrema amewavua uanachama wa TLP, Meja Mstaafu Jesse Makundi, aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo kabla ya Mrema; na Yorolanda Lyimo, Diwani wa Kilema Kaskazini.
Jimbo hilo linawakilishwa na Mrema tangu 2010, na amesema mara kadhaa kwamba hataki kusikia mtu akitaka ubunge katika jimbo lake. Tayari amemlalamikia Mbatia kwa rais na katika Bunge Maalumu la Katiba.
Kilichowaponza Makundi na Lyimo ni kushiriki harambee iliyoongozwa na Mbatia ya ujenzi wa maabara na mabweni katika shule za Sekondari za Pakula, Kiluani na Mwika, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika harambee hiyo, Makundi alisema anatambua uwezo wa Mbatia na kwamba, kwa sababu hiyo, anamuunga mkono katika azima yake ya kuwa mbunge mwakani.
Alisema kwa kuwa alipokea tochi ya kumulikia wana Vunjo kutoka kwa Mbatia, ameona ni busara kuirudisha kwa yule aliyemkabidhi tochi hiyo.
“Leo nimefikia uamuzi ambao naamini ndio hitaji la wana Vunjo, kwa kuwa Jimbo hili nililipokea kutoka kwa Mbatia na kwa kuwa yeye ndiye aliyenikabidhi hii Tochi, natamka hadharani kuwa Mbatia ndiye chaguo langu, yeye ndiye atakayemulika wana Vunjo,” alisema Makundi.
Yorolanda naye alidai kuwa uamuzi wa kumuunga mkono Mbatia ni wa Mungu.
“Tunamuomba Mungu amuinue aweze kuwa Mbunge wetu. Mimi ni Diwani wa TLP, nina Mbunge wangu, namuheshimu sana (Mrema), lakini namuomba Mungu amteue Mbatia chaguo letu Wana Vunjo. Nafahamu wapo watakaonukuu maneno yangu lakini kama mbaya acha iwe mbaya,” alisema.
Mrema amekerwa na kauli hizo, akawavua uanachama akidai wameonyesha utovu wa nidhamu na wamekiuka katiba ya chama chao kuunga mkono mtia nia wa ubunge wa chama kingine, katika jimbo lake ambalo naye ameshatangaza kuwania nafasi hiyo tena mwakani.
Alikuwa akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye Kijiji cha Mwanjeni, Kata ya Mwika Kusini.
Hata hivyo, Makundi amesema uamuzi wa Mrema ni batili, kwani mwenyekiti wake huyo hana mamlaka hayo.
Mrema amekuwa analalamikia hatua ya Mbatia kutaka ubunge wa Vunjo, akisema kinachomtia kiburi ni ubunge wa kuteuliwa aliopewa na Rais Jakaya Kikwete.
Analaumu pia vyama vya NCCR-Mageuzi, CHADEMA na CUF vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ambavyo vimetangaza kuweka mgombea mmoja mmoja kila jimbo kwa ushirikiano.
Hata hivyo, UKAWA haijatangaza mgombea wa Vunjo. Licha ya Mbatia, yupo mtia nia mwingine kutoka CHADEMA, John Mrema, ambaye naye ameshatangaza kugombea ubunge huo, akisubiri uamuzi wa mwisho wa UKAWA.
Lakini Mrema amekuwa anamshambulia Mbatia kwa kuwa ndiye amekuwa anafanya mikutano ya mara kwa mara.
Akizungumza katika mahojiano maalum na na waandishi wa habari hivi karibuni, Mbatia, malalamiko ya Mrema hayana msingi wowote, na kwamba hatajibizana naye.
“Siko tayari kujibizana na mtu. Kuna kazi kubwa mbele yetu. Tuelekeze nguvu zetu kuwatumikia Wana Vunjo. Mkutano wa Septemba ndio unaomtesa. Nyinyi ni mashahidi. Tangu Septemba 6, sijafanya mkutano wowote. Kulalamika kwake ni sawa na kulalamikia kivuli. Kivuli chake kinamuhukumu. Mimi siko tayari kumjibu,” alisema Mbatia.
Kati ya 1995 na 2005, Mrema akiwa mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na baadaye TLP, aliwahi kuthubutu kutimua viongozi wenzake kwa mtindo huo.
Miongoni mwao ni aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wake, Harold Jaffu na Thomas Ngawaiya, ambao aliwaitia Kamati ya Utendaji na kuwashitaki kwa kuwashitukiza, baada ya kugundua wamepunguza utii wao kwake.
Kabla ya hapo, alijaribu kufukuza Kamati Kuu ya NCCR-Mageuzi, akiishitaki kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu kwamba kamati hiyo ilikuwa haimsaidii kufanya kazi. Kati ya wajumbe 22 wa kamati hiyo, aliungwa mkono na wajumbe saba tu.
Kamati Kuu, ikiongozwa na Mabere Marando, ilikataa kufukuzwa na Mrema, na baadhi yao (Ndimara Tegambwage na Profesa Mwesiga Baregu) wakamshauri ajiuluzu akagoma; kukazuka mtafaruku mkubwa ulioenea kwa njia na sura mbalimbali, na hatimaye ukasambaratisha chama hicho.
Aliwahi pia kuthubutu kuwafukuza Balozi Paul Ndobho na Steven Wassira aliokuwa nao NCCR-Mageuzi, akiwatuhumu kwamba walikuwa wanafanya njama za kumwengua asigombee urais, walipokuwa wanamshawishi aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba (sasa hayati) ajiunge na NCCR-Mageuzi.
Baadaye Mrema alikimbilia TLP mwaka 1999, na kwa staili hii, alifukuza viongozi wote wa Mkoa wa Kagera wa chama chake, siku alipokwenda kumzika aliyekuwa mbunge pekee wa chama hicho wakati huo, Phares Kabuye, wa Biharamulo Magharibi.
Sababu ya kuwafukuza ni kwamba waliunga mkono hoja ya upinzani kuweka mgombea mmoja wa CHADEMA dhidi ya CCM katika uchaguzi mdogo.
Wajuzi wa siasa za Vunjo ndani ya TLP wanasema Makundi ndiye alikuwa kisiki muhimu katika ngome ya kisiasa ya Mrema jimboni; na kwamba kwa kuthubutu kumvua uanachama ni sawa na Mrema kuhatarisha ubunge wake, mithili ya mtu anayekata tawi alilokalia.

No comments: