Friday, 24 October 2014

FIFA yaridhika na maandalizi ya Kombe la dunia 2018 Urusi


Blatter mit Putin 13.07.2014 in Rio

Shirikisho la Kandanda Ulimwenguni limeridhika na hatua zilizopigwa na wenyeji Urusi kabla ya Kombe la Dunia mwaka wa 2018. Kamati ya ukaguzi ya shirika hilo imekamilisha ziara yake ya kwanza rasmi nchini humo
Ujumbe huo umevitembelea viwanja vya St Petersburg, Kazan, Sochi na viwanja viwili mjinji Moscow. Wakaguzi walisema yapo masuala kadhaa yanayostahili kushughulikiwa lakini wakakubaliana kuwa mwendo wa maandalizi ni wa kasi ya kutosha. Chris Unger ni mkuu wa ujumbe huo "ufikia sasa inaonekana tuko katika mwendo mzuri, tuna baadhi ya viwanja vilivyokamilika. Hiyo inatusaidia sana katika mipango yetu, lakini haimaanishi kuwa kazi yetu imekamilika. Tuna kazi kubwa ya kuvikarabati viwanja hivyo na kuviweka katika kiwango cha Kombe la Dunia. Na hivyo ndivyo tunavyoshughulikia masuala hayo kulingana na namna kila uwanja unatakikana kutimiza muda uliowekwa".
Aliongeza kuwa baada ya Kombe la Dunia nchini Brazil, maandandilizi ya Urusi kwa ajili ya tamasha lijalo ndiyo yanayoangaziwa kwa sasa na FIFA. Maafisa wa Urusi wanaamini kuwa kila kitu kitakamilika kwa wakati unaofaa kama anavyoeleza hapa Waziri wa Michezo Vitaly Mutko. "juu ya yote hayo tunasonga na mwendo mzuri, lakini hilo halimaanishi kuwa hatuna matatizo. Lakini hii pia haimaanishi kuna mattaizo tusiyoweza kutatua. Ukweli ni kuwa bado tunakabiliwa na masuala mengi, na ndio tumeanza tu kuutekeleza mpango huu. Tuna miaka mitatu mbele yetu na tutahitaji kufanya kazi kwa nguvu zaidi.
Kamati ya FIFA itafanya ziara saba nchini Urusi kabla ya Kombe la Dunia 2018. Kinyang'anyiro hicho kitavihusisha viwanja 12 mjini Moscow, St Petersburg, Samara, Saransk, Rostov-on-Don, Sochi, Kazan, Kaliningrad, Volgograd, Nizhny Novgorod na Yekaterinburg. Nembo rasmi ya Kombe la Dunia nchini Urusi itazinduliwa wiki ijayo Oktoba 28.

No comments: