Friday, 24 October 2014

Chadema; Hakuna kiongozi aliye msafi hata mmoja CCM


Mwenyekiti wa Taifa Mstaafu wa Baraza la Vijana CHADEMA, (BAVICHA), John HecheCHAMA cha Demorasia na Maendeleo, (CHADEMA), kimesema wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliondoa kipengele cha uadilifu kwenye tunu za taifa kwa sababu walijua watakosa viongozi kwani hakuna aliye msafi.
Aidha, wamedai vipengele vyote vilivyoondolewa kwenye rasimu ya pili ya Katiba ni vile vilivyokuwa vikisimamia maslahi ya taifa na kuwabana mafisadi.

Pia, chama hicho kikuu cha upinzani, kimemshangaa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, kutaka kugombea urais wakati anajua hana sifa wala uwezo, kwani ameshindwa hata kufufua kampuni ya simu nchini, (TTCL), ambayo imetoa nafasi kwa kampuni binafsi kutoa huduma ya mawasiliano.
Hayo yalisemwa juzi na Mwenyekiti wa Taifa Mstaafu wa Baraza la Vijana CHADEMA, (BAVICHA), John Heche, wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Sengerema, mkoani Mwanza.
Alisema kuwa kwenye rasimu ya pili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, suala la uadilifu liliwekwa baada ya wananchi kulalamika kwamba viongozi wanaiba rasilimali za umma lakini wanaendelea kuwa kwenye nafasi zao au kupewa nyingine, hivyo kuendelea kuliibia taifa.
“Waziri mmoja maarufu alimuuzia hawara yake nyumba ya Serikali eneo la Mikocheni kwa sh. milioni mbili wakati bei ya kiwanja tu katika eneo hilo ni sh  bilioni moja.
“Wakati haya yakitendeka Chenge (Andrew), alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, si mlisikia naye alificha mabilioni ya fedha kwenye kisiwa cha New Jersey nchini Uingereza, alipoulizwa akasema ni vijisenti, leo tunaambiwa ndiyo kaongoza Kamati ya kutuandikia Katiba, halafu mtegemee vipengele vya kudhibiti wezi viwekwe!,” alihoji Heche.
Alisema kuwa Ibara ya 22 ya rasimu iliyowasilishwa na Tume, ilikataza mtumishi wa umma aliye kwenye ajira ya kudumu serikalini kutopewa ajira nyingine, lakini wabunge wa CCM wameiondoa kwa kuwa wanajua hata sasa kuna wabunge wengi wa chama hicho tawala ambao pia ni wakuu wa wilaya na mikoa.
TENDEGA AWASHUKIA MABALOZI
Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Wanawake CHADEMA Taifa, (BAWACHA), Grace Tendega, aliwaonya mabalozi wa nyumba 10 wa CCM kuacha kupita kwenye nyumba za watu kujifanya wanaandikisha wananchi kwa ajili ya uchaguzi za Serikali za Mitaa.
Alisema kazi hiyo ni ya watendaji wa Serikali kwenye maeneo yote na inapaswa kufanyika siku 21 kabla ya uchaguzi ambayo ni Novemba 23 mpaka 29 mwaka huu.
Tendega, alisema kuwa haki haiombwi wala kugawiwa kama pipi bali  lazima itafutwe na ikibidi ipiganiwe, hivyo aliwataka wananchi kuhakikisha wanajiandikisha muda utakapofika.
“Hapa mnalalamika mmechagua viongozi kwa ahadi ya kuwamalizia tatizo la maji lakini hawafanyi hivyo, sasa huu ndiyo wakati wa nyie kuwaonyesha hasira zenu, muwanyime kura wasipate hata kitongoji kimoja,” alisema Tendega.
WANANCHI WANENA
Wakiongea kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima wananchi wa Sengerema walisema kuwa, wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji ambayo huwalazimu kununua madumu matatu kati ya sh 1,200 mpaka 1,500.
Walimlaumu mbunge wao, William Ngeleja, kwa kushindwa kuwatatulia kero hiyo ambayo awali aliwaahidi iko mbioni kuisha, kwani ameshapata wafadhili lakini hivi sasa wakimkumbusha anakuwa mkali.
“Ngeleja akija kuongea hapa, anakuja na askari wengi wa kumlinda, ukimuuliza kuhusu maji anakuwa mkali kama pilipili, kuna siku alituambia hatuna cha kumfanya akaondoka,” alisema Koleta Jolijo mkazi wa Igogo B.

No comments: