Monday 20 October 2014

Real Madrid uso kwa uso na Liverpool kesho kutwa

England. Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid wataingia dimbani keshokutwa kumenyana na Liverpool katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya makundi.
Mechi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Anfield mjini Liverpool inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa sababu timu hizo zina majina makubwa Ulaya na zimetwaa mara nyingi ubingwa wa Ulaya, Madrid ikiwa imetwaa mara 10 wakati Liverpool mara tano.
Steven Gerald
Ronaldo
Pia katika mechi nyingi zilizokutanisha timu hizi Liverpool imekuwa ikiibuka na ushindi hivyo Real Madrid inataka kulipiza kisasi.
Katika msimu wa 2008/09, Liverpool iliichapa bao 1-0 Real Madrid katika mechi ya hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyochezwa mjini Madrid na ziliporudiana huko England, Liverpool ilishinda 4-0. Pia Liverpool iliichapa Real Madrid bao 1-0 katika mashindano ya kombe la ubingwa wa Ulaya mwaka 1981.
Hivi sasa katika kundi B, Real Madrid ndiyo inayoongoza kundi ikiwa na pointi sita wakati Liverpool katika kundi hilo inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tatu.
Timu hizi pia zina wachezaji wenye muunganiko kimataifa ambao ni Coutinho, Lucas na Marcelo (Brazil); Dejan Lovren na Modric (Croatia); Mamadou Sakho, Raphael Varane na Karim Benzema (Ufaransa); Joe Allen na Gareth Bale (Wales).
Hata hivyo, katika mechi hii macho ya mashabiki wengi yatakuwa kwa mchezaji bora wa dunia, Cristiano Ronaldo atakayekuwa akiiongoza Real Madrid kusaka ushindi huku Liverpool ikimtegemea Mario Balotelli katika kuzifumania nyavu.

No comments: