Thursday 30 October 2014

Ufaransa yatoa somo uwekezaji gesi

ufaransaBALOZI wa Ufaransa nchini, Malika Berek, amesema watanzania wana fursa kubwa kuwekeza katika sekta ya mafuta na gesi kwa kushirikiana na wawekezaji wa nje  kwani mtaji wao ni rasilimali zao.
Alisema mtaji pekee wa watanzania katika uwekezaji huo ni rasilimali yao na wawekezaji wa nje watakuja na mitaji na teknolojia yao.
Balozi huyo, alitoa kauli hiyo jana wakati alipomtembelea Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi katika Ofisi ya Makao Makuu ya IPP jijini Dar es Salaam.
Balozi huyo mpya nchini, alipingana na dhana kwamba watanzania hawawezi kuwekeza kwenye sekta hiyo kwani hawana mitaji na badala yake alisisitiza mtaji wa rasilimali iliyopo nchini, inatosha kuwa mtaji wao kuwekeza kwa ubia na wawekezaji wa nje.
“Sikubaliani na dhana kwamba watanzania hawana mitaji ya kuwekeza kwenye gesi, hapana. Nakubaliana nawe kwamba rasilimali iliyopo inatosha kuwa mtaji wa kuwekeza kwa ubia na wawekezaji wa nje,” alisema Balozi Berek.
Alisema lengo la Serikali yake ni kuimarisha zaidi mahusiano yake na Tanzania na iko tayari kutoa mafunzo kwa vijana wa kitanzania na kutolea mfano wa baadhi ya waandishi wa habari nchini waliokwenda nchini Ufaransa kwenye ziara ya mafunzo kwa vitendo na kubadilishana mawazo na wenzao wa Ufaransa.
Pia alisema Serikali yake imeandaa mkutano maalum wa Biashara kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na Ufaransa, utakofanyika Paris Desemba 15 na kwamba mkutano huo utafungua milango ya uwekezaji nchini.
Balozi huyo alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Dk. Mengi aliyetaka kujua maoni yake kuhusu dhana kwamba watanzania ni masikini na hawawezi kuwekeza kwenye sekta ya gesi na mafuta.
Dk. Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), alisema kumekuwa na maoni na dhana potofu kwamba watanzania ni masikini sana, hivyo hawana uwezo wa kuwekeza kwenye sekta hiyo wakati wanamiliki rasilimali kubwa ya ardhi, mafuta, madini na nyinginezo.

No comments: