Sunday, 22 June 2014

Nigeria waichapa Bosnia-Hercegovina 1 -0

Emenike alichangia pakubwa mechi hii
Nigeria ilisajilia ushindi wake wa kwanza katika kombe la dunia katika kipindi cha miaka 16 ilipoilaza Bosnia-Hercegovina 1-0 katika mechi yao ya pili ya kundi F.
Ushindi wa mwisho wa Super Eagles ilikuwa ni mwaka wa 1998.
Bao hilo la pekee lilifungwa na Peter Odemwinge kunako dakika 29 ya kipindi cha kwanza alipopokea pasi safi kutoka kwa Emenike .
Mfungaji bao hilo Peter Odemwinge naye alifunga bao lake la kwanza la kombe la dunia baada ya miaka minne.
Bao hilo hata hivyo litajadiliwa kwa upana na marefu ikizingatiwa kuwa wachezaji wa Bosnia walimlalamikia vikali refarii wa mech hiyo wakisema kuwa Emenike alikuwa ameponda nahodha wa Bosnia Spahic kabla ya kummegea odemwinge pasi murwa.
Odemwinge akiifungia Nigeria bao dhidi ya Bos- Hez
Aidha msaidizi wa refarii atakumbukwa kwa kumnyima bao safi Edin Dzeko aliyesemekana kaotea lakini picha za runinga zilionesha haikuwa kweli na hivyo Bosnia watelekea nyumbani wakijua vyema kuwa mechi hiyo ingeishia sare ya Moja kwa moja isingalikuwa ni msaidizi wa refarii.
Kipa wa Super Eagles Vincent Enyeama alikuwa na wakati mgumu kumzima Dzeko aliyefanya mashambulizi katika muda wa majeruhi katika mechi hii.
Nigeria sasa itakabiliana na Argentina katika mechi yao ya mwisho ya makundi .
Kufuatia Ushindi huo Super Eagles imejikita katika nafasi ya pili ikiwa na alama 4 mbili nyuma ya vinara Argentina ambao walilazimika kufanya kazi ya ziada kuilaza Iran bao 1-0.
Iran ni ya tatu huku Bosnia ikiyaaga mashindano haya baada ya mechi yao ya mwisho dhidi ya Iran.
Nigeria itafuzu kwa mkondo ujao iwapo itashinda ama kutoka sare na Argentina katika mechi yao ya mwisho.
Vilevile Super Eagles itafuzu iwapo Bosnia itailaza Iran.

Ghana yatoshana nguvu na Ujerumani

Ujerumani 2-2 Ghana
Asamoah Gyan aliifungia Ghana bao la pili na kusadia Black Stars kusajili alama yake ya kwanza katika kombe la dunia baada ya kuambulia kichapo cha 2-1 dhidi ya Marekani katika mechi yao ya kwanza.
Baada ya kipindi cha kwanza kuishia sare tasa, nipe nikupe baina ya timu hizo zilizaa matunda dakika tano baada ya kipindi cha pili kuanza.
Mario Gotze alikuwa ameifungia Ujerumani bao la kwanza kwa kichwa kunako dakika ya 51 lakini furaha yao haikudumu kwani Andre ayew akaisawazishia Black stars dakika tatu tu baadaye.
Matumaini ya timu ya Afrika kufuzu kwa mkondo wa pili yaliimarika Nahodha Asamoah Gyan alipoiweka Ghana mbele kunako dakika ya 63 ya kipindi cha pili.
Bara la Afrika lilihuzunishwa Miroslav Klose alipofuma kona ya Ujerumani kimiani na kuisawazishia ujerumani kunako dakika ya 71 ya mechi hiyo na hivyo timu hizo zikagawanya alama mechi ilipokamila mabao yakiwa ni 2-2 .
Kufuatia bao hilo la Klose mjerumani huyo anayeicheza Lazio ameweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika historia ya kombe la dunia kwa pamoja na Ronaldo.
klose amefunga mjumla ya mabao 15.
Ujerumani 2-2 Ghana
Kwa upande wake Asamoa Gyan naye ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka barani Afrika ambaye amefunga mabao katika michuano tatu ya kombe la dunia.
Vijana wa Joachim Low sasa wamejikita kileleni mwa kundi G wakiwa na alama 4 moja zaidi ya Marekani huku Ghana ikiwa ya tatu na alama moja kutokana na sare hii ya leo.
Ureno licha ya kuwa na wachezaji wenye haiba ya juu kama vile Christiano Ronaldo bado wanaburuta mkia wakiwa bila ya alama yeyote .
Black stars sasa watakuwa wanaomba kuwa Christiano Ronaldo ataisaidia Ureno kuibana Marekani kisha nao wailaze Ureno iliwafuzu kwa mkondo wa pili.

Wapiganaji wa jihad waiteka miji zaid


Wapiganaji wa ISIS
Wapiganaji wa Jihadi wameendelea kuyateka maeneo zaidi nchini Iraq,baada ya kuliteka eneo moja la kivuko karibu na mpaka wa Syria, na sasa wanalekea mjini Baghdad kupitia bonde la Euphrates.
Mwandishi wa BBC nchini Iraq amesema kuwa hatua hiyo inawafungulia njia wapiganaji wengine wa ISIS nchini Syria.
Wapiganaji hao vilevile wameiteka miji zaidi katika mkoa wa Anbar ambapo mwandishi huyo anasema kuwa lengo lao ni kuitumia kuvamia mji mkuu wa Baghdad.
Waasi hao wanasema kuwa waliiteka miji hiyo bila kumwaga damu kupitia majadiliano na makabila ya kisunni.
Wanamgambo wa Kishia hapo jana walifanya gwaride mjini Baghdad, na kuzua wasiwasi kuhusu tofauti inayozidi kuibuka kati ya watu wa dhehebu la kishia na wale wa Kisuni.

Shambulio jingine Nigeria 10 wauwawa

kiongozi wa boko haram Abubakr Shekau
Takriban watu kumi wameuawa katika shambulizi la kijiji kimoja kazkazini mashariki mwa Nigeria,karibu na eneo ambalo zaidi ya vijana 200 walitekwanyara mnamo mwezi Aprili.
Wakaazi wanasema kuwa watu waliojihami walivamia kijiji cha Korongi-nim kilichopo takriban kilomita 14 kutoka Chibok ambapo wasichana hao walitekwa nyara na wapiganaji wa Boko Haram.
Kiongozi moja wa eneo hilo ameiambia BBC kwamba wanamgambo hao walikichoma kijiji chote cha Koronginim.
Ripoti pia zinaarifu kuwa kundi hilo limedaiwa kuwatekanyara wanaume na wasichana kutoka kijiji chengine katika jimbo la Yaza siku ya alhamisi.

Papii Kocha na Babu seya walia na Kikwete

  Wanamuziki wa Bendi ya Wafungwa, Nguza Viking ‘Babu Seya’ (kulia) na mwanaye Johnson Nguza "Papii Kocha’ (wa pili kulia) wanaotumikia kifungo cha maisha gerezani, wakitumbuiza na wenzao katika maadhimisho ya Siku ya Magereza yaliyofanyika katika Chuo cha Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam jana.

Wanamuziki Nguza Viking na Papii Kocha wanaotumikia kifungo cha maisha jela, wamemuomba Rais Jakaya Kikwete awasamehe kwa makosa waliyofanya.
Nguza na mwanaye Papii walitoa ombi hilo kupitia wimbo wakati wakitumbuiza katika maadhimisho ya Siku ya Magereza yaliyofanyika Chuo cha Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam.
Ombi hilo waliliwasilisha kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe aliyekuwa mgeni rasmi kwenye sherehe hizo ambapo Nguza maarufu Babu Seya na mwanawe, Johnson Nguza (Papii Kocha), walitumbuiza wakiwa na Bendi ya Wafungwa. Walimwomba Waziri Chikawe kufikisha ombi lao kwa Rais Kikwete.
Babu Seya na Papii Kocha walitoa burudani hiyo huku wakighani mashairi yenye ujumbe wa kuomba Rais awasamehe, hali iliowafanya mamia ya watu waliofurika kwenye hafla hiyo kutulia kimya, wengine wakilengwa na machozi.
Akiimba huku akitabasamu, Papi Kocha alikuwa akionyesha mikono ya kuomba msamaha na kusema: “Kosa gani sisi tusilosamehewa; vifungo vya maisha, miaka 30 gerezani havifundishi.”
“Waziri Chikawe tunaomba umfikishie Rais Jakaya Kikwete ombi letu, mwambie atusamehe. Hata Petro alimkana Yesu mara tatu, lakini Yesu alimsamehe kwa nini sisi….,” alisikika akiimba Papi Kocha na baadhi ya wananchi waliohudhuria uwanjani hapo wakiinamisha vichwa chini na wengine kutokwa na machozi.
Akijibu ombi hilo wakati akiwahutubia wananchi Waziri Chikawe alisema: “Nimesikia maombi yenu, yamefika na nitajitahidi kuyafikisha kwa Rais Kikwete.”
Chikawe akijibu ombi hilo alisema “Mtu akishatumikia kifungo kwa miaka saba au 10 gerezani nina hakika kama ana moyo na nafasi ya kuacha, atakuwa amebadilika hivyo anaweza kupewa msamaha.”
Baadaye Chikawe alitembelea mabanda ya maonyesho na Bendi ya Wafungwa ikipewa tena nafasi ya kutumbuiza. Babu Seya aliimba wimbo maarufu wa  ‘Seya tucheze wote’ na umati wa watu kutoka kwenye mabanda ya maonyesho na kumiminika jukwaani kucheza wakiwamo askari magereza na wakishangilia jambo lililowafanya askari kuzuia bendi hiyo kuendelea kutumbuiza.
Awali, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Minja  alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na Magereza katika kutekeleza majukumu ya jeshi hilo.

Sita wafariki Dunua 12 wajeruhiwa

Wananchi wakiangalia daladala linalofanya safari kati ya Makumbusho na Kunduchi lililopata ajali eneo la Lugalo jijini Dar es Salaam jana. Watu sita walifariki dunia papohapo na 12 kujeruhiwa.

Watu sita wamefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa baada ya kutokea ajali iliyohusisha magari matatu, eneo la Lugalo, jijini Dar es Salaam jana.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni Camillius Wambura, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa ilitokea baada ya gari la abiria aina ya DCM kupoteza mwelekeo na kuhama njia, kisha kuligonga gari jingine la abiria lililokuwa upande wa pili, ambalo nalo liligonga gari lililokuwa mbele yake.
 “Kati ya waliofariki dunia, watatu ni wanawake na watatu wengine ni wanaume. Majeruhuri wanane kati ya 12 ni wanaume, wanne ni wanawake na wawili kati yao wamepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi,” alisema Kamanda Wambura na kubainisha kuwa baada ya ajali hiyo madereva wa magari yote walikimbilia kusikofahamika.
Mkuu wa Hospitali ya Lugalo, Brigedia Jenerali Dk. Josiah Mekere alisema kuwa amepokea maiti za watu sita na majeruhi 12 na kwamba wawili walihamishiwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi akieleza kuwa wameumia zaidi maeneo ya kichwani.
‘’Wengi wamepata madhara kichwani, waliopelekwa Muhimbili (wawili) ni kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi kwa kuwa wanahitaji kufanyiwa kipimo cha CT scan,’’ alisema Dk. Mekere.
Akisimulia ajali ilivyotokea David Jailos, mkazi wa Tegeta aliyejeruhiwa mdomo na mguu katika ajali hiyo alisema: “Nikiwa katika daladala kutoka Ubungo kwenda Tegeta iliyokuwa katika mwendo kasi, dereva alitaka kulipita gari lililokuwa kulia kwake, lakini alipotokeza ili apite, akakuta kuna gari na kushindwa kurudi eneo lake kutokana na mwendo kasi, hivyo kuligonga kwa nyuma gari la mbele yake.
Alifafanua kuwa baada ya kuligonga, gari hilo nalo likagonga gari la mbele yake, hivyo ajali hiyo kuhusisha magari matatu, mawili ya abiria yaliyokuwa yakienda Kunduchi na jingine Tegeta.
Majeruhi mwingine, Jamila Mohamed mkazi wa Kigamboni aliyeumia mkono na bega alieleza kwa uchungu kuwa mtoto (Nasseri Nassoro) ni miongoni mwa abiria sita waliofariki kwenye ajali hiyo. Alisema kuwa alishtukia kioo kimemwangukia kikiwa kimesambaa na mtoto wake aliyekuwa amekaa naye kiti kimoja akiwa amemwangukia na baada ya kutolewa ndani ya gari, ndipo alipobaini kuwa amefariki dunia.
“Gari yetu ilikuwa imesimama, sikuelewa kilichoendelea zaidi ya kusikia mtikisiko mkubwa na mwanangu akaniangukia, baada ya hapo sikufahamu kilichoendelea hadi nilipofikishwa hapa hospitalini na kuona mwanangu ni miongoni mwa waliofariki katika ajali, ambayo siwezi kuielezea, “alisema Jamila.

Polisi nchini Kenya kuishi kwa pamoja

KITENGO cha utendaji kazi cha askari polisi nchini Kenya kimekumbwa na ukosefu wa makazi.

Hali imekuwa mbaya zaidi katika siku za hivi karibuni kiasi kwamba maafisa wa kike na kiume wanalazimika kutumia kwa pamoja vyumba vyao vichache.

Hali hiyo imetokea baada ya zaidi ya maafisa wapya 7,000, kuingizwa katika kitengo hicho miezi miwili iliyopita na kuongeza idadi ya maafisa wa polisi nchini Kenya kwa asilimia 10.

Kwa mujibu wa BBC, hali inaweza kudorora zaidi mwaka ujao ikiwa vyumba vipya havitapatikana kwa haraka.

Maafisa wengine 10,000 wataapishwa kujiunga na idara ya polisi kuwatumikia wananchi na kulinda usalama.

Mpango huo wa kupanua kitengo hicho, ulizinduliwa Bungeni na katibu wa fedha, Henry Rotich, alipoisoma bajeti ya 2014/2015, juma lililopita.

Katika taarifa ya makamanda wa majimbo iliyooneshwa kwa waandishi wa habari, maafisa waliamrishwa kuwakaribisha wenzao wapya katika vyumba vyao wanamoishi pamoja na familia zao.