Monday 9 February 2015

Matokeo ya kidato cha Nne yakaribia kutoka

Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limesema usahihishaji wa mitihani ya kidato cha nne uliofanyika Novemba mwaka jana, umekamilika.
Katibu mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde aliliambia gazeti hili wiki hii kuwa “usahihishaji umekamilika na baraza lipo katika uchambuzi wa kuyapanga na tutakapokamilisha tutayatangaza”.
Alipoulizwa ni lini hasa matokeo hayo yatatangazwa, Dk Msonde alisema: “Tumemaliza kusahihisha na mchakato wa kuyapanga ukikamilika tutawaeleza hivyo msiwe na shaka.”
Katika kipindi cha miaka miwili mfululizo, mwaka 2012 na 2013, Necta ilitangaza matokeo ya kidato cha nne mwishoni mwa Februari na mwanzoni mwa Machi.
Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne uliofanyika mwaka 2013 yalitangazwa Februari 22, mwaka jana na 2012 yalizua gumzo kutokana na asilimia 60 ya watahiniwa kufeli.
Kwa kawaida, muhula wa masomo kwa kidato cha tano huanza Julai, huku Machi na Aprili mchakato wa kuwapangia shule hufanyika wakati Mei na Juni hutumiwa kwa maandalizi kwa wanafunzi hao.
Katika matokeo ya 2013 kama ilivyokuwa katika matokeo ya mwaka 2012, shule binafsi zilikuwa na matokeo mazuri kulinganisha na za Serikali zilizokuwa zikitamba miaka ya nyuma.
Kwa mujibu wa Necta, matokeo ya mwaka 2013, shule kongwe za Serikali na zile za vipaji maalumu, zilishindwa kuingia kwenye orodha ya shule 30 bora.
Shule kongwe kihistoria zimekuwa zikitoka kapa katika matokeo ya Mtihani wa Taifa. Tofauti na matarajio ya wengi, shule hizo nyingi hazikuwamo hata katika orodha ya shule 100 bora.
Baadhi ya shule hizo ni Fidel Castro ambayo ilishika nafasi ya 83, Malangali (172), Ifunda Ufundi (205), Jangwani (226), Bwiru (242), Songea Wavulana (257), Pugu (325) na Azania (333).
Ikiwa ni mwaka mmoja umekamilika tangu Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ulipoanzishwa, taasisi ya Hakielimu ilitoa matokeo ya utafiti wake yanayoonyesha hakuna kilichofanyika.
Kaimu Mkurugenzi wa HakiElimu, Godfrey Boniventura alisema Serikali isitumie kigezo cha kuongezeka ufaulu kama ishara tosha ya kuimarika kwa elimu, kwani licha ya ufaulu huu kuonyesha kupanda ghafla, kuna changamoto nyingi katika sekta hiyo ambazo bado hazijatatuliwa na juhudi kubwa zinahitajika.“Mfano migogoro ya mara kwa mara kati ya walimu na mwajiri, utoro wa walimu, ukosefu wa maabara, vifaa vya kufundishia na tofauti kubwa iliyopo katika gharama za utoaji elimu nchini kati ya shule za serikali na shule za binafsi,” alisema Boniventura.

No comments: