Monday 23 February 2015

Waziri Majaliwa ataka shule kufanya tambiko

Mpwapwa. Ingawa Serikali ya Tanzania haiamini katika ushirikina wala matambiko, kuna watu mbalimbali na jamii tofauti zinaamini katika mambo hayo.
Serikali imekuwa ikipinga na kulaani vitendo vinavyoashiria ushirikina hata kuwashughulikia watu wanaonaswa wakishabikia imani hizo potofu.
Hata hivyo baadhi ya maeneo nchini bado watu wake wanaendeleza imani za kishirikina pamoja na matambiko.
Hata hivyo siyo jambo la kawaida kwa kiongozi hasa wa Serikali kusikika akihimiza kufanyika kwa matambiko ingawa kimsingi tukio hilo linahesabiwa kuwa ni namna ya kutafuta ufumbuzi kwa njia za kiakili na siyo ushirikina.
Ndivyo ilivyotokea hivi karibuni wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.
Ni kama hadithi, lakini katika tukio la Februari 8 asubuhi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa maagizo ya kufanyika kwa tambiko muda mfupi baada ya kuwasili eneo la Sekondari ya Mpwapwa kwa ajili ya kutoa pole na kuwafariji wanafunzi wa kike ambao bweni lao liliteketea kwa moto.
Baada ya maelezo kutoka kwa mkuu wa shule hiyo pamoja na mbunge wa Jimbo la Mpwapwa Gregory Teu, naibu waziri aligeuka na kutoa maagizo ya kufanya matambiko mazito katika eneo hilo.
Ilivyokuwa
Mkuu wa Sekondari ya Mpwapwa, Nelson Milanzi alianza kwa kutoa simulizi ya tukio la moto ulioteketeza mabweni ambalo lilitokea Januari 20 mwaka huu akisema kuwa vituko vilianza siku moja kabla ya tukio.
“Wanafunzi walitoa maelezo kwamba kulikuwa na nyoka mkubwa aliyeonekana akishuka kutoka katika paa la bweni na alipodondoka chini, uliwaka moto mkubwa. Lakini cha ajabu, moto huo uliunguza shuka mbili za bluu mashati mawili na ghafla ulizimika. Majivu niliyakuta,” anasimulia Milanzi.
Mkuu huyo anasema kuwa tukio hilo lilikuwa na ajabu kiasi cha kumfanya akusanye wanafunzi wa kiume na walimu zaidi ya 10 na kuwapandisha katika dari na kuanza kufanya msako mkali, lakini hawakumuona nyoka huyo.
Siku iliyofuata, mambo yaligeuka, nyoka yule yule aliyeungua jana, alitua chini ghafla na safari hii kukiwa na mwanafunzi mmoja wa kike na moto uliwaka na kushika kasi ya ajabu, ambapo kila kilichokuwa ndani kiliteketea.
Kwa mujibu wa maelezo ya kiongozi huyo, aliyemnukuu mwanafunzi aliyekuwa ndani ya bweni, hii ni mara ya pili kukutwa na mambo ya ajabu kama hayo.
Anasema kuwa mwanafunzi huyo alieleza kuwa katika kipindi cha mitihani mwaka jana alitokewa na mambo ya ajabu ambayo yalimfanya kushindwa kuhitimu kidato cha sita, hivyo kulazimika kurudia darasa hilo.
Kwa mujibu wa walimu, mwanafunzi huyo (jina tunalo) ni miongoni mwa wasichana wenye vipaji vya hali ya juu, lakini inasemekana kuwa bibi yake anayetajwa kuwa mganga wa kiasili anataka kumrithisha mikoba, lakini binti huyo alipokataa ndipo mambo hayo yalimkuta.
Mbali na tukio hilo, Milanzi anakiri kuwapo kwa matukio mengine ya ajabu yanawakumba hata wanafunzi wa kiume ambao mara kadhaa hulazimika kuita viongozi wa dini kwa ajili ya kuombewa.
Simulizi ya mbunge
Mbunge wa Mpwapwa Mjini, Gregory Teu ni miongoni mwa watu waliohudhuria ujio wa naibu Waziri Majaliwa, ambaye kwa kinywa chake anaeleza kuwa alikulia eneo hilo wakati huo baba yake (George) akiwa mwalimu shuleni hapo, kilipokuwa chuo cha kilimo kabla ya kuwa shule ya sekondari.
Maelezo ya mbunge huyo yanafanya watu wengi kupatwa na mshangao, hasa pale anaposisitiza kuwa taarifa za ‘redio mbao’ kuhusu ushirikina, zina ukweli ndani yake juu ya kilichojificha nyuma ya moto huo.
Teu anasema kuwa mambo yaliyotokea ingawa wengi hawaamini ni ya kweli na kwamba ni lazima kuwaita viongozi wa dini zote ili kuliombea eneo hilo na kuondoa mikosi na mapepo. “Mimi nimekulia hapa, baba yangu alikuwa mwalimu wa kilimo enzi hizo. Hili bweni lililoungua ndipo ilipokuwa maabara ya kilimo, nasema lazima hapa watu waje kuombea na tutaandaa utaratibu kwa gharama yoyote,” anasema Teu.
Anabainisha kuwa eneo hilo ni miongoni mwa maeneo yaliyokuwa tulivu nyakati zote na halikuwahi kukumbwa na mambo ya ajabu kama yanatokea sasa.
Majaliwa ashituka
“Kabla sijasema mambo mengi, naomba kuagiza na hili liwe ni agizo kwamba, lazima wazee waje hapa ili kufanya mambo yao maana haiwezekani nyoka akageuka kuwa moto. Hii ni ajabu kweli, ndugu zangu, isiwe viongozi wa dini pekee yao tu,” anasema Majaliwa.
Naibu waziri huyo anasema kuwa katika Tanzania mambo kama hayo kwa siku hizi ni ya kawaida na kwamba kuna maeneo mengine mbali na kuwaita viongozi wa dini zote huanza na wataalamu kama wazee wa mila.

Anatoa mfano kuwa katika Shule ya Sekondari ya Mahuta, mkoani Lindi kuliwahi kutokea mambo kama hayo, lakini walipoitwa wazee walipita na kuimba na hali ikatulia.
“Unaweza kukuta wakaja hapa na kuimba tu na wakitoka mambo yote yanakuwa safi, huenda kuna mzee yupo hai au alishatangulia mbele za haki, lakini ana manung’uniko ya miaka mingi kwamba ardhi yake ilitwaliwa bila ya kulipwa fidia”, anasema
Anasisitiza kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya utamaduni ambao jamii haina budi kuukubali na usikwepwe ili kunusuru na kuondokana na athari zinazoigharimu Serikali.
Agizo la waziri linaeleza kuwa lazima mambo hayo yafanyike katika kipindi kifupi kijacho, kabla ya kuanza kwa ujenzi wa jengo jingine kwani bila ya kufanya hivyo inaweza kuwa sawa na kudharau mizimu.
Wazee wakubali
Mzee Mohammed Athuman Mwile (86), mmoja wa wakazi jirani na shule hiyo anakiri kuwa yanapotokea mambo ya ajabu kama hayo ni lazima kuikumbuka mizimu pamoja na watu waliotangulia mbele za haki kwa kutumia utaratibu maalumu.
“Agizo la naibu waziri kwetu ni jambo la kheri, tunachoweza kufanya sasa ni utekelezaji wa haraka, ili tutimize wajibu wetu na kuwaachia mambo yao nao,” anasema Mwile.
Mzee huyo anasema kuwa suala la matambiko katika mambo yanayoleta migogoro ni la kawaida na la muda mrefu linalostahili kuendelezwa katika nyakati hizi.
Anasimulia kuwa zamani eneo la Mpwapwa lilisifika kwa matambiko ikiwamo kuomba mvua kupitia mizimu na kila lilipofanyika hali ilikuwa nzuri na mambo yalirejea bila kuleta madhara.
Hata hivyo, Mwile anaeleza kwamba anaamini kuna dini zinazoweza kuombea mapepo yakatoka, lakini inapobidi kufanya matambiko hakuna shida yoyote.
Kuhusu vifaa, mzee huyo anasema kuwa tambiko huhitaji kondoo pamoja na nguo nyeusi na kwamba kama watajiridhisha kuwa ni tambiko dogo, hakuna haja ya kufanya yote, bali ni wazee kusema maneno yao tu. Mwinjilisti Jackson Emmanuel wa Kanisa la EAGT, anasema yupo tayari kufanya maombi, lakini pia anakubali wazee kufanya matambiko kama imani yao inawatuma hivyo.
“Tunachoamini sisi ni kwamba tutalifunika eneo hilo kwa damu ya Yesu na hakuna kitu kitakachotokea tena. Mambo ya matambiko siamini, lakini kama wako wanaoamini, basi watangulie ili sisi tukasafishe,” anasema Emmanuel.
Wakati maandalizi yakiendelea, hofu inazidi kuenea kwa wanafunzi ambao wanaona kuwa mambo hayo yakianza tena, huenda milango itakuwa ikifunguka kukaribisha mizimu.
Mwanafunzi Rhoda (si jina lake) anamtaka mkuu wa shule kuachana na mambo yote kwa madai kuwa yanaweza kuita mapepo wabaya ambao mwishowe yatawadhuru zaidi.

SOURCE; MWANANCHI

No comments: