KAMA dili ikifanyika kwa haraka kabla
msimu haujamalizika, Simba inaweza kuandika rekodi nyingine ya kuuza
mchezaji kwenye timu kubwa zenye hadhi Afrika tena kwa fedha nyingi.
Kiungo wa Simba aliyeko kwa mkopo kwenye klabu ya
Stand United ya Shinyanga, Haruna Chanongo ameitwa kwa majaribio kwenye
klabu tajiri ya TP Mazembe na ataondoka nchini wiki ijayo.
Iwapo Chanongo atafuzu na kusaini Mazembe kabla ya
msimu huu kumalizika Simba itaula, lakini kama akisaini baada ya msimu
kumalizika itakuwa imekula kwa Mnyama kwa vile mkataba wake na mchezaji
huyo utakuwa umemalizika na atakuwa huru.
Kuondoka kwa mchezaji huyo huenda kukaipa ahueni
Yanga kwa vile atakosa mechi baina ya timu yake ya sasa ya Stand United
dhidi ya Jangwani kwenye Uwanja wa Taifa wiki ijayo.
Mazembe ndiyo klabu wanayochezea Watanzania; Mbwana Samata (aliyetokea pia Simba) na Thomas Ulimwengu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mkurugenzi wa Ufundi wa
Stand, Muhibu Kanu alisema kuwa wataweza kumkosa Chanongo kwa kuwa
amepata nafasi ya kwenda kufanya majaribio kwenye klabu ya TP Mazembe.
“Kwa sasa kocha wetu anamwandaa kwa ajili ya
kufanya majaribio, hivyo amemwandalia programu ya peke yake nia ni
kutaka kuona kijana anafuzu kwa kuwa hii ni sifa ya Tanzania nzima kama
akiweza kusajiliwa na TP Mazembe,” alisema Kanu.
Alisema pia itakuwa ni pengo kubwa kwao kwani wana
mechi mbili kubwa ya Kagera Sugar na Yanga huku tayari tiketi ya ndege
ikitarajiwa kutumwa kwa ajili ya safari hiyo.
Meneja wa Chanongo ambaye ni Jamal Kisongo amekiri
kuwa mchezaji huyo ataondoka nchini wiki ijayo kuifuata Mazembe huko
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
“Chanongo ataondoka wiki ijayo na hilo viongozi wa
Stand wanalielewa ijapokuwa wamesikitishwa mchezaji huyo kuondoka
wakati anahitajika sana katika timu hiyo, lakini kwa ajili ya maendeleo
yake lazima akajaribu bahati yake,” alisema.
Meneja huyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kituo cha
Kukuza Soka kwa vijana kinachojulikana kwa jina la ‘Jaki’ kilichopo
Mbagala jijini Dar es Salaam, alimtaka Chanongo kutumia vema nafasi hiyo
ingawa ataenda kukutana na changamoto ya viungo waliopo Mazembe.
“TP Mazembe wana viungo vya ushindani wa hali ya juu, lakini Chanongo akifanya vizuri ana nafasi kubwa,” alisema.
No comments:
Post a Comment