Tuesday, 24 February 2015

Ccm yaburuzwa na Chadema


 Wafuasi wa Chadema wakishangilia katika Kata ya Chanji baada ya chama hicho kuibuka na ushindi katika uchaguzi wa marudio wa Serikali za Mitaa uliofanyika juzi mjini Sumbawanga

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeigaragaza vibaya CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika juzi katika kata tatu za Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa ambazo hazikufanya uchaguzi Desemba 14, mwaka jana.
Uchaguzi katika kata hizo uliahirishwa kutokana na kasoro mbalimbali jambo lililosababisha mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, William Shimwela kusimamishwa kazi.
Msimamizi wa uchaguzi huo uliofanyika katika kata za Msua, Chanji na Kizwite na mitaa mingine miwili iliyorudia uchaguzi, Hamid Njovu alisema Chadema ilinyakua jumla ya mitaa 37 kati ya 44 na kuiacha CCM ikiambulia mitaa mitano.
Matokeo hayo mapya yanaibuka sasa wakati Ofisi ya Waziri Mkuu ilishahitimisha kutangaza matokeo ya jumla ya mitaa katika uchaguzi huo ikisema ulikuwa umekamilika kwa asilimia 100.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tamisemi, Kalist Luanda alisema Desemba 24, mwaka jana kuwa mitaa yote 3,875 nchini ilifanya uchaguzi na kukamilika kwa asilimia 100 huku CCM ikipata asilimia 66.66 baada ya kuzoa mitaa 2,583, ikifuatiwa na Chadema iliyopata mitaa 980 (asilimia 25.3), CUF mitaa 266 (asilimia 6.9), NCCR Mageuzi mitaa 28 (asilimia 0.7), TLP mtaa mmoja (asilimia 0.03), ACT mitaa 12 (asilimia 0.31), UDP mitaa mitatu  (asilimia 0.08), NRA mtaa mmoja (asilimia 0.03) na UMD mtaa mmoja (asilimia 0.03).
Matokeo mapya
Akitangaza matokeo hayo jana, Njovu alisema katika Kata ya Kizwite kati ya mitaa 15 iliyofanya uchaguzi Chadema ilishinda mitaa 13 dhidi ya CCM iliyoambulia mitaa miwili, Kata ya Msua mitaa yote 13 iliyofanya uchaguzi ilikwenda kwa Chadema na CCM kuambulia patupu.
Alisema kwa Kata ya Chanji ambayo ilikuwa na mitaa 14 iliyofanya uchaguzi, Chadema ilishinda mitaa 10 na CCM mitatu huku mtaa mmoja wa Nankasi kura ziligongana katika nafasi ya uenyekiti, hivyo kuamuliwa uchaguzi utarudiwa Jumapili.
Njovu alisema katika uchaguzi wa marudio uliofanyika kwenye mitaa miwili kila chama, CCM na Chadema, kiliibuka na ushindi katika mtaa mmoja ambao mtaa wa Bangwe Kata ya Izia ulichukuliwa na CCM na ule wa Tambazi katika Kata ya Sumbawanga ukaenda Chadema.
Uchaguzi huo uliofanyika kwa amani na utulivu tofauti na ilivyokuwa Desemba 14, mwaka jana ambapo ulivurugika katika kata hizo kutokana na kasoro kadhaa zilizojitokeza ikiwa pamoja na vituo kuchelewa kufunguliwa.
Hali hiyo ilisababisha wananchi waliokaa vituo kwa zaidi ya saa nane wakisubiri kupiga kura kuhamaki na kujichukulia sheria mkononi kwa kuchoma moto ofisi ya mtendaji wa kata ya Kizwite na Chanji na kuteketeza nyaraka zote za kupigia kura, hivyo kufanya mchakato mzima wa uchaguzi huo kufanyika upya.
Akizungumza baada ya matokeo hayo, Mwenyekiti wa Chadema mkoani Rukwa, Zeno Nkoswe aliwashukuru wananchi waliojitokeza kwa wingi kupiga kura na kufanya Chadema kuibuka na ushindi wa kimbunga na kuwa huo ni mwanzo wa kuelekea ukombozi wa Taifa kutoka mikononi mwa CCM.

Kwa upande wake, Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Rukwa, Clement Bakuli alisema wameyapokea matokeo hayo kwa masikitiko, lakini katika mpambano wowote lazima mshindi apatikane, hivyo chama kitakaa kufanya tathmini kuona wamekosea eneo gani ili waweze kujirekebisha katika uchaguzi ujao.
Pamoja na matokeo hayo, timu nzima ya CCM ngazi ya wilaya ikiongozwa na mwenyekiti wake wa mkoa, Emmanuel Kilindu na Mbunge wa Sumbawanga Mjini Aeshi Hilaly walipiga kambi na kufanya kampeni za nguvu katika kata hizo lakini haikufua dafu.
Ushindi huo ni mwendelezo wa mafanikio ya Chadema ndani ya Ukawa katika uchaguzi huo Desemba 14 na kurudiwa Desemba 21 katika baadhi ya maeneo, yaliyoonyesha kuwa uungwaji mkono wa CCM katika maeneo ya mijini umeporomoka kwa kasi huku wa upinzani ukiimarika.
Katika uchaguzi huo, chama kipya cha ACT-Tanzania kilichomoza na kuviacha baadhi ya vyama vikongwe ambavyo havikupata hata nafasi ya ujumbe katika uchaguzi ulioelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) kuwa ulikuwa umekamilika kwa asilimia 99.
Katika maeneo ya vijiji na vitongoji, CCM ilipata ushindi wa asilimia 79.81 (vijiji) na 79.83 katika vitongoji, wakati kwenye mitaa ambayo ipo sehemu za mijini kilishuka zaidi na kupata asilimia 66.66, ikilinganishwa na matokeo ya uchaguzi wa mwaka 1999, ambapo chama hicho kilipata asilimia 89.2 katika mitaa, asilimia 91 katika vitongoji na asilimia 91.6 katika vijiji.

No comments: