Friday, 27 February 2015

Tibaijuka abishana dakika 415, Chenge aenda Mahakama Kuu

Wakati Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka jana alitumia dakika 415 (takribani saa 7) akibishana katika mpambano mkali wa kisheria kuhusika kwake katika sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, mwenzake wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge aliamua kutimkia Mahakama Kuu kukwepa kuhojiwa na Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Jana, mwenyekiti wa baraza hilo, Jaji Hamisi Msumi alitoa uamuzi kuhusu pingamizi la Chenge aliyetaka baraza hilo lisisikilize shtaka lake la kukiuka maadili ya uongozi wa umma.
Hata hivyo, Chenge alikwamisha kwa mara ya pili baada ya kuomba kwenda Mahakama Kuu kutafuta tafsiri iwapo baraza hilo linaweza kusikiliza shauri lake kinyume na amri ya mahakama iliyoagiza lisijadilie na taasisi kwa kuwa kuna kesi kadhaa mahakamani zinazohusiana nalo.
Profesa Tibaijuka na Chenge kila mmoja aliingiziwa Sh1.6 bilioni kwenye akaunti zao binafsi kutoka kwa mkurugenzi wa VIP Engineering iliyokuwa ikimiliki asilimia 30 ya hisa za kampuni ya Independent Power Solution Limited (IPTL).
Baraza hilo, linasikiliza mashauri hayo kuhusu ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 katika vipengele vya matumizi mabaya ya madaraka na sakata la escrow.
Chenge, juzi katika baraza hilo alipoitwa kuhojiwa aliibua hoja ya zuio la Mahakama Kuu na baada ya mabishano ya kisheria, Jaji Msumi alisema angekwenda kuisoma amri huyo kisha kutoa uamuzi wake jana.
Akisoma uamuzi huo, Jaji Msumi alisema: “Mlalamikiwa ametoa hoja ya amri ya Mahakama Kuu kuwa ndiyo hiki kinachojadiliwa, chimbuko lake ni miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow ambalo chimbuko lake ni bungeni na mahakama ilizuia lakini amri hiyo haizuii mamlaka hii.”
“Orodha ya taasisi zilizotajwa hailihusu baraza hili, wadaiwa wote pamoja na mawakala, watumishi, wasaidizi wao au watu wengine wanaofanya hili. Amri iliyoandikwa, Baraza si mlengwa wa hili. Kinachozuiwa kufanywa ni kupelekwa bungeni au kujadiliwa taarifa ya (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali pamoja na umiliki wa IPTL,” alisema.
Akihitimisha kusoma uamuzi wa baraza hilo, Jaji Msumi alisema: “Hoja iliyotolewa na mlalamikiwa haina msingi na tunaomba kuendelea kulisikiliza.”
Mara baada ya kumaliza, Chenge aliyekuwa amevalia shati la kitenge na suruali nyeusi akiwa haonyeshi kuwa na wasiwasi alisema: “Nashukuru kwa uamuzi huo lakini sina nia ya kubishana, natoa hoja ya kukata rufaa ya kwenda Mahakama Kuu ili mahakama itafasiri kama Baraza lina mamlaka ya kujadili suala hili.”
Chenge ambaye pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema: “Kama wanasheria wa sekretarieti wangejituma kidogo kwenda masijala ya Mahakama Kuu kupitia wangeliona hili. Amri hii ya zuio ni pana kuliko uamuzi wa Baraza lako uliofikia, naomba nitumie nafasi hii kwenda Mahakama Kuu.”
Akihitimisha hoja hiyo, Jaji Msumi alisema: “Nakuruhusu, niongeze tu sina hakika kama kanuni zimetengenezwa kuruhusu rufaa na kama hazipo kutakuwa na utaratibu. Ukipeleka itasaidia kujenga Baraza lakini Mahakama Kuu ina haki, kila mtu ana haki kwa suala lolote, mimi siwezi kukuzuia.”
Mara baada ya uamuzi huo, Chenge akiwa anatoka ukumbini waandishi wa habari walianza kumpiga picha huku wengine wakimtaka kuzungumzia uamuzi wake wa kupeleka suala hilo Mahakama Kuu, lakini yeye alisema: “Nani anataka nimpeleke tuisheni,” kauli iliyowafanya waandishi hao kucheka.
Profesa Tibaijuka
Shauri la Profesa Tibaijuka lililoanza kusikilizwa saa 3:16 asubuhi hadi saa 5:18 asubuhi kabla ya kuahirishwa na kurejea tena saa 6.30 mchana hadi lilipohitimishwa saa 11.23 jioni, lilivuta hisia za wananchi na watumishi mbalimbali wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Barbro Johansso wakiongozwa na Mkuu wa Shule hiyo, Halima Kamote.
Mashtaka
Akisoma hati ya malalamiko dhidi ya mbunge huyo wa Muleba Kusini, mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili, Wemaeli Wilfred alisema: “Mheshimiwa Profesa Anna Tibaijuka kwa kutumia wadhifa wake (waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi) alishawishi na kuomba na kupokea fedha Sh1.617 bilioni kutoka kwa James Rugemalira.
Mara baada ya kumaliza kusoma hati hiyo, Wakili wa Profesa Tibaijuka, Rugemeleza Nshala alisimama na kusema: “Tunayakataa yote.”
Kutokana na kauli hiyo, Jaji Msumi aliingilia kati na kusema: “Hii siyo mahakama ya kisheria, taratibu zetu siyo za kimahakama, hivyo ni vizuri kuyafikiria hayo.”
Ushahidi
Baada ya kauli hiyo shahidi wa Sekretarieti, Waziri Kipacha ambaye pia ni Katibu Msaidizi, Idara ya Siasa ya Sekretarieti alisimama na kuanza kutoa ushahidi wake akiongozwa na Wilfred.
Shahidi huyo alisema alichokifanya Profesa Tibaijuka (kuomba na kupokea fedha hizo) wakati huo akiwa waziri, ni kinyume na sheria za maadili ya vingozi wa umma.
“Kuna tatizo, kwa mujibu wa masharti ya maadili ya viongozi wa umma hawaruhusiwi kuomba maslahi ya kiuchumi kutoka kwa mtu yeyote, mheshimiwa Tibaijuka Februari 12 mwaka 2014 alipokea fedha kutoka VIP Sh1.617 bilioni...hapa kuna tatizo la kimaadili.”
Kipacha aliendelea kulieleza baraza hilo kuwa: “Kiongozi wa umma haruhusiwi kupokea maslahi ya kiuchumi lakini mheshimiwa Tibaijuka alifanya hivyo akijua kuwa ni makosa kutokana na sheria ya maadili ya viongozi wa umma.

“Profesa Tibaijuka kupokea kiasi kikubwa cha fedha kama hicho na wadhifa aliokuwa nao wa uwaziri ni ukiukwaji wa sheria za viongozi wa umma mheshimiwa mwenyekiti. Viongozi wa umma wanapaswa kuzingatia maadili wanapokuwa na uhusiano na kampuni au taasisi binafsi.”
Baada ya maelezo hayo, Wakili Nshala alimuuliza Kipacha kuwa ni kosa gani alilolifanya kupokea mchango wa shule kama alivyokwishaeleza?
Kipacha alijibu: “Hapa ni ukiukwaji wa sheria ya maadili, Profesa Tibaijuka alipokea mchango ambao ni kiasi kikubwa cha fedha tena kwa kupitia akaunti yake binafsi, jambo ambalo ni kinyume kabisa cha sheria hii.”
Nshala aliuliza tena: “Je, kama kiongozi wa nchi yetu ana jukumu la kuhamasisha na kusaidia watoto wetu kupata elimu, sasa hapa Profesa Tibaijuka kosa lake ni lipi?
Kipacha alijibu: “Kama kusaidia kwa kutoa fedha zake mfukoni siyo kosa na kama unachangisha au kuhamasisha watu kuchangia elimu na fedha hizo zinakwenda moja kwa moja kwa walengwa siyo kosa, lakini fedha hizo zikiingia moja kwa moja kwako hapo ni makosa kwa mujibu wa sheria hii ya maadili ya viongozi wa umma.”
Nshala aliendelea kumuuliza, “Baada ya kufuatilia ninyi kwa uchunguzi wenu baada ya yeye (Profesa Tibaijuka) kuingiziwa fedha mlibaini nini?”
Kipacha kwa upole na kujiamini wakati wote alijibu: “Tulibaini fedha hizo zilianza kutoka kwa mafungu. Februari 18, 2014 zilitoka Sh1 bilioni kwenda Bank M na Machi 12, 2014 zilitoka Sh500 milioni kwenda Bank M na kubakiwa na Sh117 milioni katika akaunti yake ambayo hatujui alizifanyia nini. Lakini mwenyekiti hapa lalamiko ni ukiukwaji wa maadili tu.”
Nshala aliuliza tena: “Kwa nini katika uchunguzi wenu hamkwenda kuwahoji Bank M au bodi ya wadhamini wa shule kwa kuwa ndiko fedha zilikwenda na iwapo wao walitoa uamuzi huo?
Kipacha alisema: “Kwa mujibu wa sheria hii sisi hatukuona sababu ya kwenda kuwahoji wao.”
Baada ya kauli hiyo, Jaji Msumi aliingilia kati na kusema: “Katika uchunguzi wenu kwa nini hamkwenda kuhoji zaidi wakati mnasema kuna taasisi imenufaika kwa nini hamkwenda huko?
Akijibu hoja hiyo, Kipacha alisisitiza kuwa hawakuona sababu ya kufanya hivyo.
Sh10 milioni za mboga 

Hoja iliyoibua vicheko barazani ni kauli ya Profesa Tibaijuka kuwa kati ya fedha hizo alichota kwanza Sh10 milioni za kununua mboga.
Akitoa utetezi wake ambao mara zote ulikuwa ukiwafanya watu waliojaa ukumbini humo kuangua vicheko, Profesa Tibaijuka akihojiwa na mwanasheria wa sekretarieti hiyo, Getiruda Cyriacus aliyetaka kujua kama fedha hizo ziliingia Februari 12, 2014 kwa nini zilitoka Februari 18, mwaka huo na wakati huo huo kuna kiasi cha Sh10 milioni kilitoka mapema?
Profesa Tibaijuka alisema: “Nilitoa kiasi hicho kwenda kununua mboga, kwani kuna kosa gani.”
Akiendelea, Profesa Tibaijuka alisema: “Uongozi mzima wa shule ya Babro wanafanya kazi kwa uadilifu, uwazi na ukweli wa hali ya juu na mimi kuomba mchango wa kuwasaidia watoto wa kike waliokuwa hawana fursa ya kupata elimu bora sioni kosa lake.
“Harakati hizi zitaendelea kwani nimekuwa nikizifanya nje na ndani ya nchi na ndiyo maana Rais mstaafu, Benjamini Mkapa alitupa kiwanja cha shule hiyo inayopigiwa kelele na yeye alishachangia fedha na watu wengine wakiwamo wafadhili wakubwa, mfano Serikali ya Sweden iliyochangia zaidi ya Sh8 bilioni lakini leo hii Sh1.6 inanidhalilisha hapa.”
Aliongeza: “Mimi ni mstaafu wa Umoja wa Mataifa nina mafao yangu napata na nina akaunti za benki kama 10 ndani na nje ya nchi, sasa hii ya Rugemalira kama ningetaka angeiingizia katika akaunti nyingine, lakini yeye alisema ili asaidie shule nifungue akaunti Benki ya Mkombozi, sasa ningefanyaje?
Profesa Tibaijuka aliongeza, “Leo hii nadhalilishwa na kusimamishwa hapa kwa harakati zangu za kumkomboa mtoto wa kike, niwahakikishie kuwa nitaendeleza harakati hizi na malengo yangu ni kuhakikisha kila kanda kunakuwa na shule hizi za mfano, tulianza na Dar es Salaam, Bukoba sasa tunatafuta kiwanja Mwanza na Mbeya.”
Mbunge huyo aliambatana na mashahidi wake wawili, Balozi Paul Rupia ambaye ni mlezi wa Bodi ya Wadhamini wa shule hiyo na mwenyekiti wa bodi hiyo, Simon Odunga ambao wote kwa pamoja walisema fedha walizopokea kutoka kwa Rugemalira kupitia akaunti ya Profesa Tibaijuka zilitumika kulipa deni la Sh2 bilioni walilokuwa wakidaiwa na Bank M, ambalo hata hivyo halikumalizika.
Baada ya utetezi huo, Jaji Msumi alizitaka pande zote ziandae majumuisho ambayo yatawasilishwa kabla ya Machi 13 mwaka huu, ili Baraza liandae mapendekezo ya siri yatakayopelekwa kwenye mamlaka za juu.

No comments: