UBISHI mkubwa uliokuwa umetawala kwenye usajili wa Simba ni
kuhusiana na usajili wa vichwa vitatu, straika Elius Maguli wa Ruvu
Shooting, Mrundi Pierre Kwizera wa Afad ya Ivory Coast na kiungo wa
zamani wa Msimbazi, Shaaban Kisiga. Ubishi huo umekwisha jana Ijumaa
kiulainii na vijana hao tayari wako Msimbazi.
Mrundi Pierre Kwizera wa Afad ya Ivory Coast. |
Kama ubishi huo hautoshi Simba jana ilifunga
hesabu ya wachezaji wa kigeni watakaovaa uzi mwekundu msimu ujao na
kufuta kabisa uwezekano wa Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza kutua Msimbazi
kama mmoja wao akitemwa na Yanga kwani tayari Simba ina vichwa vitano.
Mbali na Kwizera, Simba ina wachezaji wengine wa
kigeni ambao ni Amissi Tambwe (Burundi), Donald Mosoti (Kenya ), Joseph
Owino (Uganda) na Paul Kiongera ambaye amewaahidi viongozi kwamba
atamalizana na KCB ya Nairobi wikiendi hii na Jumatatu atatua Msimbazi
kusaini mkataba ambao tayari wameshapatana bei kwani wiki iliyopita
alikuwa Bongo ambapo alifikia Kijitonyama.
KWIZERA
Kwizera ambaye ni bingwa wa kupiga mipira mirefu
na kufunga magoli kwa faulo baada ya kutua jana aliiambia ukombozi
kuwa: “ Nimekuja kuwapa ubingwa Simba na kazi yangu kubwa ni kuhakikisha
ushindi unapatikana na timu inafunga lakini pia hairuhusu goli kwenye
lango letu.
“Mimi ni kiungo na ninapenda kucheza nafasi ya
kiungo mkabaji zaidi kuliko ile ya kiungo mshambuliaji na zaidi
napendelea kucheza mipira mirefu. Hivyo ninachoomba ni muda kidogo wa
kuzowea mazingira lakini pia nataka kucheza Simba kwa mafanikio, niko
tayari kwani hata nilivyokuja nimetoka kwenye ligi na naamini
sitawaangusha Wanasimba.
“Ninachoomba ni michezo miwili ya kujiweka sawa na
kumuonyesha kocha kile nilichonacho, tena nitaonyesha kile
nilichojifunza nikiwa Ivory Coast na hii itanifanya niwe na nguvu na
kuisaidia Simba. Namjua Tambwe kwani tuliwahi kucheza wote timu ya Taifa
ya Burundi, anajua kufunga lakini pia ninafuraha kuwa tayari ninajua
jinsi anavyocheza na tena nimeifuatilia Simba kwa zaidi ya misimu miwili
na kuiona hivyo sina wasiwasi wa kucheza.
MAGULI NA KISIGA
MAKAMU wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’
aliwatambulisha wachezaji hao jana. Maguli ambaye alishika nafasi ya
pili katika ufungaji bora msimu uliopita akiwa na mabao 14 na Tambwe
alikuwa mfungaji bora kwa mabao 16.
Kaburu alisema Maguli amesaini mkataba wa miaka miwili na Kisiga mwaka mmoja.
“Tumekamilisha usajili wa Maguli ambaye kwa muda
mrefu tulikuwa tunamhitaji, kamati pia imefanikiwa kumalizana na klabu
yake ya Ruvu ambao walikuwa na mkataba naye, watu wanaweza kuona mambo
yanaenda taratibu, hayo yote yanatokana na ukweli kwamba tunataka
kufanya usajili kwa umakini mkubwa,” alisema Kaburu ambaye ni mzoefu wa
mambo ndani ya Simba.
MKUTANO NA SIMBA DAY
Akizungumzia kuhusu Mkutano Mkuu wa Simba, Kaburu
alisema utafanyika kesho Jumapili kama ulivyotangazwa na Rais wake
Evans Aveva ambao utafanyika katika Bwalo la Maofisa wa Polisi lililopo
Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Kaburu alisema Zesco United ya Zambia itacheza nao katika siku ya Simba Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa.
LOGA ANENA
KOCHA wa Simba, Zdravko Logarusic akishakabidhiwa
Paul Kiongera, Saady Kipanga na Elius Maguli atalazimika kubadili mfumo
na kuchezesha washambuaji wengi zaidi. Logarusic alisema Kiongera,
Maguli na Kipanga si washambuliaji kamili hivyo anaweza kuwachezesha
nyuma ya mshambuliaji wake mahiri Mrundi Amissi Tambwe kwa kutumia mfumo
wa 4-2-3-1.
No comments:
Post a Comment