Pamoja na mpango wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
kuliaga Bunge kukwama jana, Chama cha ACT- Tanzania kimetangaza
kukamilisha maandalizi ya kumpokea mwanasiasa huyo kuanzia leo.
Mbunge huyo alipanga kuliaga bunge na alisema
amekwishapata ruksa ya Spika kuwa angesimama bungeni kuwaaga wabunge na
wanachama wa Chadema baada ya chama hicho kumtimua uanachama wake hivi
karibuni, lakini ghafla mpango huo uliyeyuka kwa kile kilichoelezwa kuwa
Spika amemkatalia.
Tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka mmoja
uliopita, Zitto amekuwa akihusishwa kukianzisha, hivyo kitendo chake cha
kujiunga nacho kitahitimisha mjadala wa muda mrefu wa mashabiki wake
waliokuwa wakihoji wapi ataelekea baada ya kung’olewa Chadema.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa
ACT, Samsom Mgamba aliangua kicheko na bila kuuma maneno alisema:
“Hahahaa... tutampokea kuanzia kesho (leo) na maandalizi yamekamilika.”
Alipotakiwa kueleza wapi mapokezi hayo yatafanyika
alisema: “Hilo mbona liko wazi, yatafanyikia makoa makuu yetu (yapo
Makumbusho, Dar es Salaam) lakini kwa taarifa zaidi tutawajuza.”
Zitto anaingia ACT ikiwa ni siku tisa kabla ya
chama hicho kufanya uchaguzi wake mkuu, huku akitajwa kuwa ameandaliwa
kushika wadhifa wa mwenyekiti kuendeleza harakati zake za siasa.
Hivi karibuni, chama hicho kilimvua uongozi
aliyekuwa mwenyekiti mwanzilishi, Lucas Limbu kutokana na mgogoro
uliokuwapo baina ya viongozi na kufanya nafasi hiyo kubaki wazi.
Tayari washirika wa Zitto waliohusishwa naye
kuandika waraka wa mapinduzi ndani ya Chadema na baadaye kufukuzwa
uanachama, Mwigamba na Profesa Kitila Mkumbo wametua ndani ya chama
hicho kipya.
Chama hicho ambacho kinaendelea na uchaguzi katika
ngazi ya mikoa kikibakiza Mkoa wa Geita unaofanya uchaguzi wake kesho.
Kitaanza vikao vyake vya kitaifa Machi 27 na kuhitimisha kwa mkutano
mkuu Machi 29.
Akizungumzia uchaguzi huo, Mwigamba alisema:
“Maandalizi yanakwenda vizuri na hakuna shaka utafanikiwa kwa kiasi
kikubwa na tunawaomba Watanzania watuunge mkono.”
Tangu juzi, Zitto alitarajiwa kuliaga Bunge lakini
hakufanya hivyo kwa kilichoelezwa kuwa aliitwa na Spika wa Bunge, Anne
Makinda na kupewa ushauri kuwa afanye hivyo jana jioni.
Jana asubuhi mbunge huyo hakuingika katika kikao
cha Bunge lakini alionekana katika viwanja vya Bunge akiwa amevaa shati
la drafti na suruali ya kaki akizungumza na rafiki yake wa karibu, Deo
Filikunjombe ambaye ni mbunge wa Ludewa kupitia CCM.
Katika kipindi cha jioni, mbunge huyo aliingia katika viwanja
vya Bunge saa 11:10 jioni akiwa amebeba mafaili huku akizungumza na simu
na baadaye kutaniana na waandishi wa habari waliokuwa nje ya ukumbi wa
Bunge.
Mbunge huyo aliyekuwa amevalia shati nyeupe na
suruali nyeupe kabla ya kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge alizungumza na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya.
Akwama kuliaga Bunge
Habari zilizopatikana bungeni jana jioni zilieleza
kuwa Spika Bunge, Makinda alimpiga ‘stop’ mbunge huyo kuaga bungeni
bila kuweka wazi sababu za kufanya hivyo.
Mbunge huyo juzi alitinga bungeni kwa mara ya
kwanza tangu Chadema kitangaze kumvua uanachama na kufanya kikao cha
siri na Makinda kwa zaidi ya saa moja na baadaye kulieleza gazeti hili
kuwa angezungumzia hatima ya ubunge wake jana.
Habari zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa
na watu wake wa karibu naye zilieleza kuwa licha ya Makinda kumshauri
mbunge huyo kuaga bungeni, jana aligoma kumpa ruhusa hiyo.
“Kazuiwa kuaga sijui kwa nini, ila kwa jinsi
tunavyoona Makinda ni kama anahitaji Zitto aendelee kubaki bungeni.
Ngoja tusubiri kwanza tuone nini kitatokea,” zilieleza habari hizo.
Alipoulizwa juu ya taarifa hizo Zitto, alisema:
“Hata mimi nasikia hivyo ila sina hakika sana. Ngoja niende ndani
nitajua zaidi, mimi nataka kuaga, can’t stay any more (siwezi kuendelea
kubaki).
Alipoingia katika ukumbi wa Bunge, Zitto
alionekana akizungumza na baadhi ya wabunge wa upinzani na baadaye
wakati mjadala wa muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Uhamiaji
ukiendelea, alitoka nje na watu wa karibu wa mbunge huyo walisema
alikuwa akishinikiza kuaga kama alivyopanga.
Spika Makinda hakupatikana kuzungumzia sababu za
kukataa kumruhusu mbunge huyo na Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John
Joel alipoulizwa juu ya suala hilo alisema hajui chochote.
Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage
alisema mbunge huyo kisheria hana mamlaka ya kushinikiza kuaga bungeni
na kumtaka asubiri mamlaka husika zifanye kazi hiyo, akimaanisha Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) kulijulisha Bunge kuwa Zitto si mbunge tena
baada ya kupata barua ya Chadema.
Chadema ilitangaza kumvua Zitto uanachama siku 10
zilizopita, saa chache baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam
kutupa shauri lake alilofungua akitaka chombo hicho cha sheria
kimlazimishe katibu mkuu wa chama hicho kumpa nyaraka za vikao vya
Kamati Kuu vilivyomvua nyadhifa zote.Awali, Mahakama hiyo ilitoa amri ya muda ya kuzuia Chadema kumjadili na
amedumu kwenye nafasi ya ubunge chini ya zuio hilo kwa takribani mwaka
mmoja.
No comments:
Post a Comment