HATIMAYE Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), jana kimetangaza rasmi kumvua uanachama Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe kwa tiketi ya chama hicho.
Chama hicho kimechukua uamuzi huo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kutupilia mbali pingamizi la Mbunge huyo dhidi ya Kamati Kuu ya CHADEMA, kutojadili uanachama wake.
Bw. Kabwe alikuwa akikabiliwa na mashtaka ya ukiukwaji wa Katiba ya chama chake, kanuni na mwongozo wa chama ambapo kikao cha Kamati Kuu, kilichokaa Novemba 20-22, mwaka 2013, kiliazimia aachishwe nafasi zote za uongozi alizokuwa akishikilia.
Kamati hiyo pia iliazimia Bw, Kabwe achukuliwe hatua zaidi za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kuachishwa, kufukuzwa uanachama kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji za 6.5.2(d).
Lissu atoa tamko
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Bw. Tundu Lissu, alisema kutokana na uamuzi huo wa mahakama, CHADEMA kinakusudia kuiandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Lengo la barua hiyo ni kuitaarifu NEC kuwa Bw. Kabwe si mwanachama tena wa chama hicho, hivyo amepoteza sifa ya kuwa mbunge kwa tiketi ya CHADEMA ili aweze
kumjulisha Spika wa Bunge.
Bw. Lissu alisema licha ya mahakama hiyo kutupilia mbali kesi ya Mbunge huyo, imemtaka alipe gharama zote za kesi tangu ilipofunguliwa hadi uamuzi ulipotolewa.
\"Mahakama imeamua kulifuta pingamizi lililowekwa na Bw. Kabwe mwaka 2014 akizuia kikao cha Kamati Kuu kisimjadili kabla ya shauri lake halijasikilizwa na Baraza Kuu.
\"Pingamizi hilo limetupiliwa mbali baada ya Mahakama kupitia hoja zake na kubaini kuwa, hakufuata taratibu za kisheria, hivyo
kutokana na uamuzi huo, chama kinatamka rasmi kumvua uanachama Bw. Kabwe ambaye pia alikuwa Naibu Katibu Mkuu,\" alisema Bw. Lissu.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, mwanachama yeyote anapofungua kesi mahakamani dhidi ya chama chake, kama atashindwa katika kesi hiyo atakuwa amejiondoa uanachama wake.
Maelezo ya Kabwe
Kwa upande wake, Bw. Kabwe alisema hakuwa na wito wa kwenda mahakamani jana na Jaji wa kesi hiyo amehamishiwa Tabora, hivyo yeye na Mawakili wake hawana taarifa ya Jaji Mpya; lakini Mwanasheria wake atafuatilia hukumu hiyo.
\"Mimi nilikuwa kwenye kikao cha Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA), nikaona katika mitandao ya kijamii kuwa kesi yetu imetupwa lakini katika kumbukumbu zetu, ilikuwa twende mahakamani Machi 12 mwaka huu si kwa ajili ya maamuzi bali kwa ajili ya kesi kutajwa.
\"Taarifa hizi zimetushangaza baada ya kusikia uamuzi umetolewa leo na CHADEMA kutangaza kunivua uanachama, hadi sasa sina taarifa rasmi, naendelea na kazi zangu kama kawaida na ratiba yangu inaonesha kesho (leo), nitakuwa TANESCO,\" alisema.
Aliongeza kuwa, kesho atakuwa anashughulikia mabilioni ya Uswisi ambapo kwa upande wake, hana taarifa rasmi na ataweza kusema chochote baada ya kupata taarifa rasmi na Wanasheria wake wameenda mahakamani kupata hati ya maamuzi ili waone hatua za kuchukua.
Kesi ya msingi
Januari 2, 2014, Mahakama hiyo ilitoa zuio la muda kwa Kamati Kuu ya CHADEMA kutojadili uanachama wa Bw. Kabwe katika kikao cha chake cha Januari 3, 2014.
Siku hiyo ya Januari 3, 2014, Mahakama hiyo ilisikiliza hoja za mawakili wa pande zote kuhusu maombi hayo mbele ya Jaji John Utamwa ambapo Januari 7, 2014, Mahakama hiyo ilitoa amri kwamba Bw. Kabwe asijadiliwe uanachama wake hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa maamuzi.
Bw. Kabwe alikuwa anatetewa na wakili, Albert Msando ambapo CHADEMA iliwakilishwa na Bw. Lissu pamoja na Peter Kibatala.
Katika kesi ya msingi, Bw. Kabwe alifungua kesi dhidi ya Baraza la Wadhamini la chama hicho na Katibu Mkuu, Dkt.Willbrod Slaa, akiiomba Mahakama itoe zuio la muda kwa
Kamati Kuu kutojadili suala la uanachama wake hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa maamuzi.
Katika maombi yake, Bw. Kabwe aliiomba mahakama hiyo kuiamuru Kamati kuu na chombo chochote kisijadili uanachama wake hadi rufaa yake itakaposikilizwa na Baraza Kuu la chama.
Pia aliiomba Mahakama imwamuru, Dkt. Slaa kumkabidhi nakala za taarifa na mwenendo mzima wa vikao vilivyomvua uongozi ili akate rufaa katika ngazi ya juu ya chama hicho.
No comments:
Post a Comment