Tuesday 12 January 2016

Samatta ataka kusherehekea tuzo yake na majirani zake





Mbwana Samatta 


Mwanasoka Bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka ndani ya Afrika, Mbwana Samatta hapendi makuu kwani familia yake ilipomuuliza achague hoteli watakayomfanyia sherehe ya kumpongeza kwa kutwaa tuzo hiyo ya Afrika alichowajibu kiliwaacha hoi.






Mwanasoka Bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka ndani ya Afrika, Mbwana Samatta hapendi makuu kwani familia yake ilipomuuliza achague hoteli watakayomfanyia sherehe ya kumpongeza kwa kutwaa tuzo hiyo ya Afrika alichowajibu kiliwaacha hoi.
Baba mzazi wa nyota huyo, Pazi Ally Samatta akielezea alichojibiwa na mwanae huyo alisema, “Baada ya kumwambia Samatta kwamba familia imekuambia chagua ni wapi utafurahia tukikufanyia sherehe ya kukupongeza,  yeye alinijibu baba nifanyie sherehe hiyo nyumbani kwa sababu nataka kufurahia pamoja na majirani wote wanaotuzunguka,” alisema.


Mzee huyo alisema kwa kuwa anamjua mwanae siyo mpenda makuu, hivyo alimwambia,”Ni kweli hapa ni nyumbani kwetu ulipokulia, lakini kutokana na eneo kuwa dogo na wewe utakuwa na marafiki zako pamoja na wanahabari haitawezekana, Mbwana aliniambia sawa baba tafuteni popote ila msiumize kichwa juu ya hilo.”
Jana usiku ndiyo familia ya Mzee Samatta imekutana ili kupanga ni wapi wanaweza kumfanyia sherehe Mbwana ambayo itakuwa ni maalumu kwa ajili ya kumpa wosia nyota huyo ya namna ya kulinda nidhamu kabla ya kwenda Ulaya.
“Lengo la familia kumpongeza ni kutaka kumpa baraka na kumshauri kwani pamoja na mafanikio hayo bado ni mtoto wetu, anatakiwa kuongozwa kabla ya kwenda kwenye nchi anazotarajia kwenda, mimi nimekaa huko Ulaya wakati nasomea mambo ya kuchukua picha za video na mitambo ya studio,” alisema Mzee Samatta.
Wiki iliyopita, Mbwana Samatta raia wa Tanzania anayeichezea TP Mazembe ya DR Congo aliandika historia kwa kutwaa tuzo ya mchezaji Bora wa Afrika kwa wanaocheza ligi za ndani ya Afrika.

No comments: