Friday 1 January 2016

Magari ya kibinafsi kuzuiwa kuingia Delhi

DelhiMagari ya kibinafsi yamekuwa yakiongezeka sana Delhi
Wasimamizi wa mji mkuu wa India, Delhi wameanza kuzuia baadhi ya magari ya kibinafsi kuingia mjini ili kupunguza uchafuzi wa hewa.
Magari ya kibinafsi yenye nambari za usajili zinayogawika na mbili bila masalio (namba shufwa) na yale yenye nambari zisizogawika na mbili (namba witiri) zitakuwa zikiruhusiwa mjini siku tofauti.
Mpango huo utafanyiwa majaribio kwa kipindi cha wiki mbili, na unatarajiwa kuzuia magari milioni moja kuingia mjini kila siku.

Magari ya huduma za dharura kama vile ambiulesi, magari ya polisi, magari ya wazima moto na teksi hayataathiriwa na mpango huo.
Mji wa Delhi umeshuhudia uchafuzi wa hewa wa kiwango cha juu majira haya ya baridi.
Serikali ya mji ilitangaza mpango huo baada ya mahakama kuagiza kiwango cha uchafuzi, ambacho ni mara 10 zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa na Shirika la Afya Ulimwenguzi (WHO), kidhibitiwe.
Serikali imeweka mabasi 3,000 ya kusafirisha watu kutoka maeneo ya makazi hadi mjini ili kurahisisha usafiri.
Shule pia zimefungwa hadi mwisho wa kipindi cha majaribio ya mpango huo 15 Januari ili mabasi ya shule yatumiwe kusafirisha watu.
Polisi wa trafiki watasaidiana na maelfu ya watu wa kujitolea kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa kufuatilia magari katika makutano ya barabara. Wanakaokaidi mpango huo watatozwa faini ya rupia 2,000 ($30; £20) na kutakiwa kurejea wanakotoka.
Wanaharakati wa uhifadhi wa mazingira wamesifu mpango huo wakisema hatua kali zinahitaji kudhibiti viwango vya uchafuzi.

No comments: