Wednesday 20 January 2016

Serikali Yatoa Tamko Kuhusu Dawa Mpya ya Ukimwi Iliyogundulika Hivi Karibuni

SERIKALI imesema kama Shirika la Afya Duniani (WHO), litapitisha matumizi ya dawa mpya ya ugonjwa Ukimwi wataitumia, lakini kwa sasa haiwezi kuzungumzia tafiti za ugonjwa huo ambazo zipo nyingi.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Michael John, amesema kwa sasa zipo tafiti nyingi, lakini wao kama wizara wanasubiri mwongozo kutoka WHO ambao ndiyo unathibitisha ubora wa dawa na matumizi yake.
“Zipo tafiti nyingi tunazisikia zinafanyika, lakini hili la Ukimwi ni mapema mno kulizungumzia ila kinachohitajika ni kusubiri mwongozo wa WHO ambao ndio wanatuongoza kwenye orodha ya dawa na matumizi yake katika magonjwa mbalimbali,” alisema John.

Juzi mashirika mbalimbali ya habari yalitoa taarifa juu ya utafiti mpya wa dawa ya mseto ya kimiminika ijulikanayo kama PrEP ambayo inatarajiwa kuleta faraja kwa wenza ambao mmoja anaishi na virusi vya Ukimwi huku mwingine akiwa hana.
Dawa hiyo inadaiwa tayari imeanza kutumika kwa baadhi ya mashoga nchini Uingereza na Marekani ambapo huweza kuondoa hatari ya kuambukizwa hadi asilimia sifuri.
Pia itaondoa changamoto iliyokuwapo katika njia namba moja ikiwa pamoja na kujikinga na virusi vya Ukimwi, yaani kutumia kondomu wakati wa kufanya tendo la ndoa.
Kutokana na matumizi ya kondomu wenzi hao walikuwa hawawezi kupata watoto bila uwezekano wa kuhatarisha afya ya mwenzi ambaye hana VVU.

No comments: