Monday, 5 January 2015

Zaidi ya wafuasi 500 wa kikundi cha Panya Road wakamatwa

Kamanda kova
Vijana zaidi ya mia tano wanashikiliwa na Jeshi la Polisi nchini Tanzania kwa tuhuma za kujihusisha na Vitendo vya uhalifu vilivyozua taharuki na hofu kubwa mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.
Vijana hao wanatuhumiwa kusababisha hofu kubwa jijini Dar es Salaam kwa kile kilichoelezwa kitendo cha kulipiza kisasi kufuatia kifo cha mwenzao aliyefariki kwa kupigwa mawe na wananchi waliojichukulia sheria mkononi.
Kamanda wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salam Suleiman Kova amethibitisha kukamatwa kwa Vijana hao kwa tuhuma za uhalifu jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita
Polisi wakiwa katika doria
Vijana hao zaidi ya mia tano wakiwa washiriki wakuu katika Kundi la vijana waporaji lijulikanalo kama Panya Road wanashikiliwa na Jeshi la polisi kufuatia msako mkali unaoendelea jijini kote Dar es Salaam baada ya tukio la mwishoni mwa wiki ambapo jiji la Dar es Salaam lilikumbwa na taharuki kubwa baada ya vijana hao kuanza kufanya vitendo vya uporaji mitaani.
Kova amesema katika msako huo unaoendelea mbali na kuwakamata vijana hao katika msako huo pia wamekamatwa wakiwa na Puli,kete na misokoto ya Bangi pamoja na Mirungi na Lita 150 za pombe haramu ya Gongo.
Watuhumiwa hao wamekamatwa katika maeneo mbali mbali jijini Dar Es Salaam katika sehemu mbali mbali kama kwenye vituo vya mabasi ,kwenye majumba mabovu na pia kwenye makazi yao kutokana na msako huo kufanyika nyumba kwa nyumba.
Hii ni mara ya kwanza kwa kundi kubwa la watuhumiwa kukamatwa kwa wakati mmoja na kushikiliwa huku wakisubiri kufikishwa mahakamani.

Boko haramu yavamia kambi ya Jeshi


Boko Haram yaendelea kutekeleza mashambulizi yake nchini Nigeria
Kundi la Boko Haram lililoteka nyara vijana 40 kutoka mkoa wa Borno siku ya Jumamosi, sasa limevamia kambi ya jeshi la kimataifa iliyoko katika mji wa Baga.

Maafisa wakuu nchini Nigeria waliarifu kwamba kundi hilo lilibeba kila kitu kutoka kwenye kambi hiyo na kutoroka baada ya uvamizi.

Ndani ya kambi hiyo ya jeshi la kimataifa, mlikuwa na vikosi vya kijeshi kutoka Chad, Cameroon na Nigeria.

Baga ulikuwa ni mojawapo ya miji kadhaa ya mwisho iliyokuwa chini ya udhibti wa serikali. Jeshi la Nigeria limekuwa likiendelea kupambana na Boko Haram kwa miaka mitano katika mikoa mitatu ya kaskazini mwa nchi iliyokabiliwa na kundi hilo.

David Moyes aifundisha soka Barcelona huku Madrid ikilalia Kichapo

Wachezaji nyota wa ligi kuu ya Hispania, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wa Real Madrid
Ligi Kuu ya Hispania, La Liga imezidi kuleta ushindani mkubwa baada ya vinara wa ligi hiyo, Real Madrid na Barcelona kupoteza katika mechi zao za mwishoni mwa wiki.
Kikosi cha aliyekuwa kocha wa timu ya Manchester United David Moyes ambaye kwa sasa anainoa timu ya Real Sociedad ya ligi kuu ya Hispania, La Liga, imeiadhibu Barcelona kwa goli 1-0 alilojifunga mwenyewe mchezaji wa Barcelona Jordi Alba, mapema katika dakika ya pili ya mchezo.

David Moyes kocha wa Real Sociedad ya Hispania
Kipigo Real Madrid cha 2-1 kutoka kwa Valencia mapema Jumapili kingewawezesha Barcelona kuelekea mbele katika kinyang'anyiro cha ubingwa wa ligi hiyo endapo timu hiyo ingeshinda.
Lakini kocha Luis Enrique alianza mchezo huo kwa kutowaanzisha wachezaji wake mashuhuri akiwemo Lionel Messi, Neymar na Dani Alves.
Barcelona ilishindwa kusawazisha goli walilojifunga wakati Moyes akipata ushindi wa pili akiwa meneja wa timu ya Sociedad.
Messi, Neymar na Alves walirejea katika mazoezi Ijumaa wiki iliyopita baada ya mapumziko marefu ya Krismasi Amerika Kusini ambako ligi ilisitishwa ili kusherehekea siku kuu hiyo.
Enrique alifanya mchezo wa kubahatisha kwa kutowapanga wachezaji hao katika mchezo wake na Real Sociedad ambayo imekuwa kikwazo kwa Barcelona katika michezo ya nyuma.

Wachezaji wa Real Sociedad wakishangilia goli katika moja ya michezo yao ya ligi kuu ya Hispania
Na kwa hiyo imethibitika kwa mara nyingine kwamba Barcelona hawana chao katika uwanja wa Anoeta sasa ikiwa ni michezo sita, Barcelona ikipoteza kwa Real Sociedad.
Kwa upande wake Real Madrid ilijikuta ikipoteza mchezo wake dhidi ya Valencia baada ya kucharazwa mabao 2-1 licha ya Real Madrid kuongoza kipindi cha kwanza kwa bao la penalti lililofungwa na Cristian Ronaldo dakika ya 14.
Valencia ilijipatia magoli yake yote mawili kipindi cha pili yakifungwa na Barragán dakika ya 52′ na Otamendi dakika ya 65.
Real Madrid inaongoza msimamo wa ligi ya Hispania ikiwa na pointi 39 katika michezo 16 ikifuatiwa kwa karibu na Barcelona yenye pointi 38 baada ya kucheza mechi 17.

Mapya yaibuka vurugu za kikundi cha uhalifu cha Panya Road

Ayubu Mohamed maarufu Diamond enzi za uhai wake.
Baada ya saa 24 kupita tangu kundi maarufu la waporaji la Panya Road, kuvamia na kusababisha shughuli mbalimbali kusimama kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, chanzo cha uhalifu huo kimebainika.
Hali hiyo iliwafanya wakazi wa jiji hilo kusitisha shughuli mbalimbali kutokana na kuhofia usalama wao, huku usafiri ukiadimika.
Tukio hilo linaelezwa lilitokea ikiwa ni ishara ya kundi hilo kumuenzi mwenzao aliyefikwa na mauti akidaiwa kutaka kuiba pikipiki.
Mkazi wa Magomeni Kagera, Mohamed Chalamira alisema, “Wakati wakitoka kuzika walikuwa wakiambiana kuwa mwanajeshi hawezi kuuawa na kuzikwa bila kupigwa mizinga hivyo tutakwenda kulianzisha ili polisi wapige mabomu na ndicho kilichotokea.”
Aliongeza: “Ni tukio lililotuacha tukishangaa, kwani polisi mmoja aliyekuwa na silaha alitaka kumkamata mwenzao, lakini alipotoa panga tu yule polisi alikimbia, hii haiwezekani yaani polisi anakimbia mhalifu? Ilikuwa saa 9 vijana waligeuza eneo hilo (Magomeni Kagera) kama eneo lao.”
Kuhusu vijana waliokamatwa Chalamira alisema: “Hao vijana wawili waliokamatwa mmoja kweli anahusika, lakini mwingine ni hahusiki kwani dereva, huyo mshikaji atasota huko wakati hahusiki, polisi wafanye uchunguzi wao kwani haiwezekani kundi hili likasababisha mtafaruku...Mimi mwenyewe juzi nimepoteza simu na nimeumia hapa katika goti.”
Familia yazungumza
Kaka mkubwa wa marehemu, Mohamed Ayubu maarufu ‘Diamond’, Moshi Hamadi alisema mdogo wake huyo alizaliwa mwaka 1995 Magomeni Kagera na kukulia  kwenye familia hiyo, lakini aliondoka kutokana na tabia zake kuanzia kubadilika.
Alisema Ayubu hakubahatika kumaliza elimu ya msingi kutokana na kujiingiza katika makundi ya wavuta bangi akiwa darasa la nne na alipoonywa hakukubali na alichukia na kuamua kuondoka nyumbani kwao.

Alisema baada ya mazishi kumalizika aliwataka vijana wasifanyie fujo za aina yoyote katika eneo hilo kwa sababu lawama itakua kwao.
“Walikubali, lakini nilikuwa nasema kujifurahisha, kwani sura zao zilivyokuwa nilifahamu lazima watafanya fujo na kweli walifanya hivyo,” alisema.
Aliongeza: “Tulipokuwa tunatoka makaburini saa 11.45 jioni tuliwakuta polisi wametanda maeneo haya na walipoona kundi la watu waliwatawanya vijana hao kwa kufyatua risasi.”
Mashuhuda wazungumzia
Vijana waliokuwa kwenye kijiwe cha Magomeni Kagera ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao waliliambia gazeti hili kuwa hali ilikuwa mbaya kwani kila mtu alikuwa anakimbia kunusuru roho yake.
Walisema Polisi wakiwa ndani ya gari waliloegesha eneo hilo kuna dada aliibiwa simu na hao Panya Road, lakini vijana wa eneo hilo wakawakimbiza na kuwanyang’anya simu na kumrudishia mwenyewe huku, Polisi wakitizama tukio hilo.
Vijana waliokuwa kijiwe eneo la Tandale kwa Mtogole walisema walikuwa wanamfahamu Ayubu wakati wa uhai wake, lakini hawakuwa wakijua kijiwe chake maalumu ni wapi kwa sababu alikuwa anafahamika kila kona.
Kaniki
Katika hatua nyingine makamanda wa polisi mkoa wa Dar es Salaam, akiwemo Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, wametakiwa kutodharau taarifa za uhalifu zinazotolewa na wananchi kwa kisingizio cha madai ya uvumi.
Taarifa toka ndani ya Jeshi la zilizolifikia gazeti hili jana zilisema kuwa hayo yalielezwa na  Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Abdulrahman Kaniki alipokutana na makamanda hao katika kikao cha dharura kilichofanyika Makao Makuu ya jeshi hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Naibu IGP, alisisitiza kwa makamanda hao umuhimu wa kuthamini na kuzifanyia uchunguzi wa haraka taarifa za uhalifu zinazotolewa na wananchi.
Panya road 36 mbaroni
“Huyu alikuwa ni mtoto wa pekee kwa mama yake, hakuwahi kupata mtoto mwingine, ndiyo maana hawezi kuzungumza presha imempanda,” alisema Hamad baada ya mwandishi kuomba kuzungumza na mama yake mzazi na alijibiwa hivyo.
Kauli ya Hamadi iliungwa mkono na mama mkubwa wa marehemu Ndam Moshi ambaye alisema Ayubu hakutaka vitendo vyake vijulikane na alipokuwa akienda kuwasalimia walipomgusia kwamba siku hizi anajihusisha na masuala ya wizi alikuwa anakataa na kulia kutwa nzima.
Kuhusu taarifa za kifo chake, Hamadi alisema walipigiwa simu na vijana wasiowafahamu kuwataarifu kuwa Diamond amefariki dunia kwa kukatwa mapanga eneo la Tandale kwa Mtogole ambako kulikuwa na mkesha wa Mwaka Mpya.

Mkazi wa Tandale karibu na eneo walipouona mwili wa Ayubu ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema: “Tuliamka asubuhi juzi (Januari Mosi) na kuambiwa kuna mwili umetupwa pale darajani (Daraja la Kwa Sindano linalotenganisha Tandale na Sinza-Yemen).”
Aliongeza: “Hapo ilikuwa kama saa tatu asubuhi, tuliukuta mwili wa kijana huyo ukiwa uchi wa mnyama huku tofali kubwa likiwa limewekwa kichwani kwake...Polisi walikuja na kuondoka nao mwili wa marehemu hatukujua walipokwenda kuuhifadhi.”
Hamadi  alisema mwili wa marehemu waliukuta katika Hospitali ya Taifa Muhimbili  ukiwa  umekatwa kwa mapanga maeneo ya kichwa na kuufanya kuharibika na miguu ikiwa kama imechomwa moto na ukiwa hauna nguo.
Mama mkubwa wa marehemu Ndam alisema kuwa hajawahi kukaa msibani kwa wasiwasi kama msiba huo, alisema kilichokuwa kinatokea nje katika msiba huo kilitaka kusababisha mauti ya mama yake Ayubu kutokana na presha, kwani kulikuwa na idadi kubwa ya vijana ambao hakuwafahamu.
Kwa nini msiba huo umehusishwa na Panya Road?
Hamadi alisema walipokuwa wanarudi na mwili wa marehemu kutoka Muhimbili walikuta kundi kubwa la wahuni limetanda maeneo ya jirani na nyumbani kwao na kadiri walivyokuwa wakisogea ndiyo walizidi kukuta umati wa wahuni.
Alifafanua hakuwa akimfahamu hata kijana mmoja kati yao wala ndugu zake hakuna aliyekuwa akiwafahamu kila mtu kwenye familia hiyo alikuwa anashangaa.
“Baada ya kufika waliupeleka mwili wa marehemu moja kwa moja Msikiti wa Magomeni Kagera uitwao Masjid Rahman kwa ajili ya kuswalia, kwani kila kitu kuosha na kuuandaa mwili wa marehemu kwa ajili ya mazishi ilifanyika Muhimbili,” alisema Hamadi.
Hali ilikuwaje msikitini hadi makaburini
Tofauti na kauli zilizokuwa zikitolewa na wengi kuwa maziko ya kijana huyo yalitawaliwa na vitendo vya kihuni, Shekhe Hassan Khamisi Majaliwa ambaye ni babu wa marehemu na ndiye aliyeongoza mazishi ya kijana Ayubu alisema hakukuwa na vurugu hadi walipomaliza kuzika.
“Baada ya kupokea mwili uliswaliwa kabla ya swala ya saa kumi na baada ya kuuswalia na kutoka nje ndipo vijana  hao ambao kwa miaka 40 niliyoishi hapa sikuwahi kuona umati wa vijana kama hao...Vijana hao waliupokea mwili na kuubeba wenyewe kistaarabu na kumkataza mtu yeyote kushika jeneza kwa madai kuwa hawamfahamu kama wanavyomfahamu wao.”
“Walipofika katika makaburi ya Kihata (nyuma ya msikiti huo)  aliwataka watulie na wao kwa wao wakawa wanatulizana isipokuwa mmoja wao alikuwa kalewa na alishika betri ya simu alikuwa akifanya kama vile anachukua picha, baada ya kisomo wakati mwili unafukiwa akalirusha hilo betri likafukiwa na udongo hicho ndiyo kitu pekee kilichowekwa ndani ya kaburi hilo,” alisema Sheikh Majaliwa.

Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Sala Seleima Kova alisema tangu tukio hilo lilipotokea wameendelea na msako mkali na kufanikiwa kuwatia nguvuni vijana 36.
“Tunawashikilia vijana 36 na msako huu unaendelea, tunawakamata wale wote wenye rekodi ya kufanya uhalifu...tunawaomba wananchi wanaotumia mitandao ya kijamii kuepuka kutuma taarifa ambazo hawana uhakika nazo ambazo kwa namna moja au nyingine zinahatarisha usalama,” alisema Kova
Baadaye, Taarifa kwa umma iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Bulimba alisema, “Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa vijana hao wanaojihusisha na vikundi hivyo kuacha tabia hiyo mara moja. Tumejipanga vizuri katika mikoa yote kuhakikisha kwamba nchi inaongozwa kwa kufuata utawala wa sheria, hatutamwonea mtu yeyote ama kikundi cha watu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi na kutia hofu wananchi.”
Kamanda wa Polisi wa Ilala, Mary Nzuki alisema kijana mmoja ameuwawa eneo la Kipunguni-Mombasa jijini Dar es Salaam saa 10 alfajiri ya kuamkia jana.

SOURCE; MWANANCHI

Jeshi la Polisi wakamata magaidi Dar es Salaam

Jeshi la polisi nchini Tanzania linawashikilia baadhi ya vijana wanaotuhumiwa kufanya vurugu kwa kuwapora watu mali.
Kundi la kihuni la vijana linalojulikana kama ''Panya Road'' lilifanya vurugu kwa kuwapora watu mali zao na kwenye maduka ya mitaa mbalimbali jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita.
Msemaji wa jeshi la Polisi nchini humo Advera Bulimba amesema vijana 36 walikamatwa na wanahojiwa.
Amefahamisha kuwa vijana hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani uchunguzi ukikamilika.
Aidha Msemaji wa jeshi la Polisi amefafanua kuwa ''Panya Road'' ni vikundi vidogo vidogo vya watoto wahuni wanaojiingiza katika vitendo vya uhalifu.

Sunday, 4 January 2015

Mtoto wa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga afariki

Fidel Castro
Fidel Odinga mwana wa aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga amepatikana akiwa ame
Fidel Castro
fariki nyumbani kwake huko Karen.
Maafisa wa polisi tayari wameanzisha uchunguzi kuhusiana na kifo cha mfanyibiashara huyo ambaye pia amekuwa akionekana katika ulingo wa kisiasa.
Maafisa wa Polisi wanasema kuwa uchunguzi wa mapema umeonyesha kuwa Fidel alikuwa nje usiku wa jumamosi na alirudi mapema jumapili.
Aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga.

Haijulikani ni nini kilichosababisha kifo chake.
Kundi la wabunge pamoja na maseneta liliwasili katika nyumba ya Raila baada ya kupata habari hizo.
Maafisa wanaosimamia kesi hiyo wanasema kuwa wanataka kujua ni wapi Fidel alikuwa usiku wa jumamosi na alikuwa na nani

Mwili wa shahid wa ICC wapatikana

Mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita ICC

Maafisa wa polisi nchini Kenya wameupata mwili wa shahidi muhimu wa mahakama ya ICC siku chache tu kabla ya kutoa ushahidi wake katika kesi ya naibu wa rais katika mahakama hiyo.
Ripoti za vyombo vya habari nchini Kenya zinasema kuwa mwili wa Meshash Yebei ulipatikana karibu na mto zaidi ya wiki moja baada ya kuonekana akibebwa na kuingizwa katika gari moja lisilo na nambari za usajili katika mji wa Eldoret,umbali wa kilomita 200.
Bwana Yebei alitarajiwa kusafiri kuelekea mjini Hague kwa kesi dhidi ya bwana Ruto-makamu wa rais ambaye anakabiliwa na mashtaka yanayohusiana na mashambulizi dhidi ya watu wa jamii ya kikuyu katika makaazi ya wakalenjin huko Rift valley wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi miaka saba iliopita.