Ayubu Mohamed maarufu Diamond enzi za uhai wake. |
Hali hiyo iliwafanya wakazi wa jiji hilo kusitisha shughuli mbalimbali kutokana na kuhofia usalama wao, huku usafiri ukiadimika.
Tukio hilo linaelezwa lilitokea ikiwa ni ishara ya
kundi hilo kumuenzi mwenzao aliyefikwa na mauti akidaiwa kutaka kuiba
pikipiki.
Mkazi wa Magomeni Kagera, Mohamed Chalamira
alisema, “Wakati wakitoka kuzika walikuwa wakiambiana kuwa mwanajeshi
hawezi kuuawa na kuzikwa bila kupigwa mizinga hivyo tutakwenda
kulianzisha ili polisi wapige mabomu na ndicho kilichotokea.”
Aliongeza: “Ni tukio lililotuacha tukishangaa,
kwani polisi mmoja aliyekuwa na silaha alitaka kumkamata mwenzao, lakini
alipotoa panga tu yule polisi alikimbia, hii haiwezekani yaani polisi
anakimbia mhalifu? Ilikuwa saa 9 vijana waligeuza eneo hilo (Magomeni
Kagera) kama eneo lao.”
Kuhusu vijana waliokamatwa Chalamira alisema: “Hao
vijana wawili waliokamatwa mmoja kweli anahusika, lakini mwingine ni
hahusiki kwani dereva, huyo mshikaji atasota huko wakati hahusiki,
polisi wafanye uchunguzi wao kwani haiwezekani kundi hili likasababisha
mtafaruku...Mimi mwenyewe juzi nimepoteza simu na nimeumia hapa katika
goti.”
Familia yazungumza
Kaka mkubwa wa marehemu, Mohamed Ayubu maarufu
‘Diamond’, Moshi Hamadi alisema mdogo wake huyo alizaliwa mwaka 1995
Magomeni Kagera na kukulia kwenye familia hiyo, lakini aliondoka
kutokana na tabia zake kuanzia kubadilika.
Alisema Ayubu hakubahatika kumaliza elimu ya
msingi kutokana na kujiingiza katika makundi ya wavuta bangi akiwa
darasa la nne na alipoonywa hakukubali na alichukia na kuamua kuondoka
nyumbani kwao.
Alisema baada ya mazishi kumalizika aliwataka vijana wasifanyie
fujo za aina yoyote katika eneo hilo kwa sababu lawama itakua kwao.
“Walikubali, lakini nilikuwa nasema kujifurahisha,
kwani sura zao zilivyokuwa nilifahamu lazima watafanya fujo na kweli
walifanya hivyo,” alisema.
Aliongeza: “Tulipokuwa tunatoka makaburini saa
11.45 jioni tuliwakuta polisi wametanda maeneo haya na walipoona kundi
la watu waliwatawanya vijana hao kwa kufyatua risasi.”
Mashuhuda wazungumzia
Vijana waliokuwa kwenye kijiwe cha Magomeni Kagera
ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao waliliambia gazeti hili kuwa
hali ilikuwa mbaya kwani kila mtu alikuwa anakimbia kunusuru roho yake.
Walisema Polisi wakiwa ndani ya gari waliloegesha
eneo hilo kuna dada aliibiwa simu na hao Panya Road, lakini vijana wa
eneo hilo wakawakimbiza na kuwanyang’anya simu na kumrudishia mwenyewe
huku, Polisi wakitizama tukio hilo.
Vijana waliokuwa kijiwe eneo la Tandale kwa
Mtogole walisema walikuwa wanamfahamu Ayubu wakati wa uhai wake, lakini
hawakuwa wakijua kijiwe chake maalumu ni wapi kwa sababu alikuwa
anafahamika kila kona.
Kaniki
Katika hatua nyingine makamanda wa polisi mkoa wa
Dar es Salaam, akiwemo Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova, wametakiwa kutodharau taarifa za uhalifu zinazotolewa na
wananchi kwa kisingizio cha madai ya uvumi.
Taarifa toka ndani ya Jeshi la zilizolifikia
gazeti hili jana zilisema kuwa hayo yalielezwa na Naibu Mkuu wa Jeshi
la Polisi nchini, Abdulrahman Kaniki alipokutana na makamanda hao katika
kikao cha dharura kilichofanyika Makao Makuu ya jeshi hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Naibu IGP, alisisitiza
kwa makamanda hao umuhimu wa kuthamini na kuzifanyia uchunguzi wa
haraka taarifa za uhalifu zinazotolewa na wananchi.
Panya road 36 mbaroni
“Huyu alikuwa ni mtoto wa pekee kwa mama yake,
hakuwahi kupata mtoto mwingine, ndiyo maana hawezi kuzungumza presha
imempanda,” alisema Hamad baada ya mwandishi kuomba kuzungumza na mama
yake mzazi na alijibiwa hivyo.
Kauli ya Hamadi iliungwa mkono na mama mkubwa wa
marehemu Ndam Moshi ambaye alisema Ayubu hakutaka vitendo vyake
vijulikane na alipokuwa akienda kuwasalimia walipomgusia kwamba siku
hizi anajihusisha na masuala ya wizi alikuwa anakataa na kulia kutwa
nzima.
Kuhusu taarifa za kifo chake, Hamadi alisema
walipigiwa simu na vijana wasiowafahamu kuwataarifu kuwa Diamond
amefariki dunia kwa kukatwa mapanga eneo la Tandale kwa Mtogole ambako
kulikuwa na mkesha wa Mwaka Mpya.
Mkazi wa Tandale karibu na eneo walipouona mwili wa Ayubu ambaye hakutaka kutajwa jina lake
alisema: “Tuliamka asubuhi juzi (Januari Mosi) na kuambiwa kuna mwili
umetupwa pale darajani (Daraja la Kwa Sindano linalotenganisha Tandale
na Sinza-Yemen).”
Aliongeza: “Hapo ilikuwa kama saa tatu asubuhi,
tuliukuta mwili wa kijana huyo ukiwa uchi wa mnyama huku tofali kubwa
likiwa limewekwa kichwani kwake...Polisi walikuja na kuondoka nao mwili
wa marehemu hatukujua walipokwenda kuuhifadhi.”
Hamadi alisema mwili wa marehemu waliukuta katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili ukiwa umekatwa kwa mapanga maeneo ya
kichwa na kuufanya kuharibika na miguu ikiwa kama imechomwa moto na ukiwa hauna nguo.
Mama
mkubwa wa marehemu Ndam alisema kuwa hajawahi kukaa msibani kwa
wasiwasi kama msiba huo, alisema kilichokuwa kinatokea nje katika msiba
huo kilitaka kusababisha mauti ya mama yake Ayubu kutokana na presha,
kwani kulikuwa na idadi kubwa ya vijana ambao hakuwafahamu.
Kwa nini msiba huo umehusishwa na Panya Road?
Hamadi alisema walipokuwa wanarudi na mwili wa
marehemu kutoka Muhimbili walikuta kundi kubwa la wahuni limetanda
maeneo ya jirani na nyumbani kwao na kadiri walivyokuwa wakisogea ndiyo
walizidi kukuta umati wa wahuni.
Alifafanua hakuwa akimfahamu hata kijana mmoja
kati yao wala ndugu zake hakuna aliyekuwa akiwafahamu kila mtu kwenye
familia hiyo alikuwa anashangaa.
“Baada ya kufika waliupeleka mwili wa marehemu moja kwa moja Msikiti wa Magomeni Kagera uitwao Masjid Rahman
kwa ajili ya kuswalia, kwani kila kitu kuosha na kuuandaa mwili wa
marehemu kwa ajili ya mazishi ilifanyika Muhimbili,” alisema Hamadi.
Hali ilikuwaje msikitini hadi makaburini
Tofauti na kauli zilizokuwa zikitolewa na wengi
kuwa maziko ya kijana huyo yalitawaliwa na vitendo vya kihuni, Shekhe
Hassan Khamisi Majaliwa ambaye ni babu wa marehemu na ndiye aliyeongoza
mazishi ya kijana Ayubu alisema hakukuwa na vurugu hadi walipomaliza
kuzika.
“Baada ya kupokea mwili uliswaliwa kabla ya swala
ya saa kumi na baada ya kuuswalia na kutoka nje ndipo vijana hao ambao
kwa miaka 40 niliyoishi hapa sikuwahi kuona umati wa vijana kama
hao...Vijana hao waliupokea mwili na kuubeba wenyewe kistaarabu na
kumkataza mtu yeyote kushika jeneza kwa madai kuwa hawamfahamu kama
wanavyomfahamu wao.”
“Walipofika katika makaburi ya Kihata (nyuma ya
msikiti huo) aliwataka watulie na wao kwa wao wakawa wanatulizana
isipokuwa mmoja wao alikuwa kalewa na alishika betri ya simu alikuwa
akifanya kama vile anachukua picha,
baada ya kisomo wakati mwili unafukiwa akalirusha hilo betri likafukiwa
na udongo hicho ndiyo kitu pekee kilichowekwa ndani ya kaburi hilo,”
alisema Sheikh Majaliwa.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Sala Seleima Kova alisema
tangu tukio hilo lilipotokea wameendelea na msako mkali na kufanikiwa
kuwatia nguvuni vijana 36.
“Tunawashikilia vijana 36 na msako huu unaendelea,
tunawakamata wale wote wenye rekodi ya kufanya uhalifu...tunawaomba
wananchi wanaotumia mitandao ya kijamii kuepuka kutuma taarifa ambazo
hawana uhakika nazo ambazo kwa namna moja au nyingine zinahatarisha
usalama,” alisema Kova
Baadaye, Taarifa kwa umma iliyotolewa na Msemaji
wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Bulimba alisema, “Jeshi la Polisi
linatoa onyo kwa vijana hao wanaojihusisha na vikundi hivyo kuacha tabia
hiyo mara moja. Tumejipanga vizuri katika mikoa yote kuhakikisha kwamba
nchi inaongozwa kwa kufuata utawala wa sheria, hatutamwonea mtu yeyote
ama kikundi cha watu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi na kutia hofu
wananchi.”
Kamanda wa Polisi wa Ilala, Mary Nzuki alisema
kijana mmoja ameuwawa eneo la Kipunguni-Mombasa jijini Dar es Salaam saa
10 alfajiri ya kuamkia jana.
SOURCE; MWANANCHI
SOURCE; MWANANCHI
No comments:
Post a Comment