Tuesday, 27 January 2015

Ufisadi Mpya watarajiwa Kuibuliwa tena Bungeni

Zitto kabwe
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kesho itawasha moto upya bungeni wakati itakaposoma ripoti maalumu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikitarajiwa kuibua kashfa tatu nzito ikiwamo ya misamaha ya kodi.
Kashfa nyingine zinazotarajiwa kuibuliwa kesho ni, ufisadi katika gharama za ujenzi wa jengo la watu mashuhuri (VIP) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na uuzaji wa nyumba ya Bodi ya Korosho.
Habari zilizolifikia  jana na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe zilisema kuwa, tayari kamati hiyo imepokea ripoti ya ukaguzi huo ambayo inaonyesha ufisadi wa kutisha katika maeneo hayo matatu na mengineyo.
Masuala hayo matatu pia yaliibuka wakati wa vikao vya kamati za Bunge vilivyomalizika Dar es Salaam wiki iliyopita, huku bodi ya korosho ikibanwa kuhusu nyumba yake aliyouziwa Mbunge wa Kibaha Mjini (CCM), Silvestry Koka.
Kwa mujibu wa habari hizo, ripoti hiyo inayoonyesha jinsi ufisadi wa kutisha ulivyofanywa katika ujenzi wa jengo la (VIP Lounge) na Serikali inadai ilitumia Sh12 bilioni kulijenga, lakini mthamini wa majengo ya Serikali ameeleza kuwa jengo hilo lina thamani ya Sh3 bilioni.
Katika suala la misamaha ya kodi, PAC imepokea taarifa kutoka kwa CAG ikionyesha kuwa misamaha hiyo iliyokuwa imefikia Sh1.5 trilioni mpaka Juni 2013, lakini baada ya mwaka moja misamaha hiyo imeongezeka hadi Sh1.8 trilioni mpaka Juni 2014.
“Kwa mwaka moja tu, misamaha ya kodi imeongezeka kwa zaidi ya Sh300 bilioni. Kiasi hiki ni kama escrow fulani (Fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, Sh306 bilioni),” chanzo cha habari kilidokeza.
Katika vikao vya kamati hiyo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilieleza kuwa misamaha ya kodi imepanda kutoka Sh1.4 trilioni mwaka 2012/13 hadi Sh1.8 trilioni mwaka 2013/14, chanzo kikiwa ni misamaha ya kodi katika miradi mikubwa. Ilisema kati ya misamaha hiyo, Sh676 bilioni zinatokana na misamaha ya kodi inayotokana na Ongezeko la Thamani (VAT) na kuwa hali hiyo itapungua iwapo nchi itaanza kutumia Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Pia, TRA ilifafanua kuwa mpaka sasa wafanyabiashara na kampuni kubwa zimefungua kesi katika mahakama ya rufaa wakipinga kulipa kodi ambayo inafikia Sh1.7 trilioni.
Mvutano mwingine unaotarajiwa kuibuliwa katika ripoti hiyo ni uwasilishwaji wa utata wa uuzwaji wa nyumba  ya Bodi ya Korosho.
Awali, hati ya nyumba hiyo ilikuwa ya Taasisi ya Kilimo Tanzania ambayo ilifutwa mwaka 1963, kabla ya mtu mwingine kuibadilisha hati na kuiuza kwa Koka mwaka 2011.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mudhihir Mudhihir alisema Koka aliuziwa nyumba na taasisi hiyo ambayo haikuwa mmiliki halali.
Alisema nyumba hiyo iliuzwa kwa Sh300 milioni na katika juhudi za bodi kufuatilia taratibu za kuirudisha, ikagundulika kuwa hati imeshabadilishwa, kusisitiza kuwa uuzwaji wa nyumba hiyo ulifanyika kimakosa bila kufuata sheria na taratibu.
Juzi Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alikaririwa akiwataka wananchi kutoa taarifa kuhusu makusudio ya kuuza nyumba za Serikali na mashirika ya umma, kutokana na madeni mbalimbali ili ziweze kukombolewa kabla ya kuuzwa.

No comments: