Neno “piga” lina maana ya “fanya kitendo cha kukutanisha vitu
kwa nguvu, fumua, ezeka, zaba, shambulia, chapa na tandika” kwa mujibu
wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Oxford, lakini kwa Waziri Mkuu Mizengo
Pinda neno “wapigeni” lilimaanisha “kuendelea kulinda amani”.
‘‘Baada ya kutoa kauli hiyo kuna watu wakaeleza
kuwa sasa Waziri Mkuu analeta sera za kupiga. Hapana ilikuwa kujaribu
kukemea watu wasileta fujo kama kwamba Serikali iko likizo,’’ alisema
Pinda.
Alisema akiwa bungeni aliwahimiza Watanzania
kuilinda amani na utulivu uliopo nchini kwa gharama yeyote ile na iwapo
atatokea mtu kutaka kuivunja amani hiyo, hatapewa nafasi badala yake
atashughukiwa kwa namna yeyote.
Waziri Pinda alitoa kauli hiyo tata mwaka jana
wakati wa kipindi alichokianzisha bungeni cha mswali ya papo kwa papo
kwa Waziri Mkuu, baada ya kluulizwa kuhusu vitendo vya polisi kupiga
rais badala ya kuwafikisha mahakamani.
Kauli yake ilisababisha wanaharakati kumjia juu na
wengine kutaka kwenda mahakamani kutokana na kwenda kinyume na misingi
ya utawala bora.
Waziri Pinda alitoa tafsiri ya neno hilo
alipoongea na wananchi wa Mkoa wa Katavi wakati akihitimisha ziara yake
kwa kukutana na wananchi wa Tarafa ya Kabungu, Kata ya Mpanda Ndogo
wilayani Mpanda.
Alisema amani iliyopo hapa nchini ni ya miaka mingi iwapo wakitokea watu wanaotaka kuleta chokochoko, watashughulikiwa tu.
Akizungumzia wakimbizi walioko mkoani Katavi ambao
wanatarajiwa kupewa uraia, alisema ni lazima mkoa ujiandae kuwapokea
raia hao wapya na hiyo nayo ni changamoto kubwa kwa mkoa.
‘‘Wakimbizi hao wanaotarajiwa kupewa uraia ni
wengi kwani ni zaidi ya 120 na changamoto kubwa iliyo mbele ya mkoa.
Hivyo ni vyema utaratibu mzuri ukaandaliwa kwa ajili ya kuwapokea raia
hao wapya na mkoa umejiandaa vizuri utalifanyia kazi suala hilo
kuhakikisha amani iliyopo inatunzwa,” alisema.
Alisema mbali ya wakimbizi hao walioko makazi ya
Mishamo wapo wakimbizi wengine walioko kwenye makazi ya Katumba ambao
nao wanakaribia kufikia 80,000 ambao pia watapewa uraia.
No comments:
Post a Comment