Monday, 5 January 2015

David Moyes aifundisha soka Barcelona huku Madrid ikilalia Kichapo

Wachezaji nyota wa ligi kuu ya Hispania, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wa Real Madrid
Ligi Kuu ya Hispania, La Liga imezidi kuleta ushindani mkubwa baada ya vinara wa ligi hiyo, Real Madrid na Barcelona kupoteza katika mechi zao za mwishoni mwa wiki.
Kikosi cha aliyekuwa kocha wa timu ya Manchester United David Moyes ambaye kwa sasa anainoa timu ya Real Sociedad ya ligi kuu ya Hispania, La Liga, imeiadhibu Barcelona kwa goli 1-0 alilojifunga mwenyewe mchezaji wa Barcelona Jordi Alba, mapema katika dakika ya pili ya mchezo.

David Moyes kocha wa Real Sociedad ya Hispania
Kipigo Real Madrid cha 2-1 kutoka kwa Valencia mapema Jumapili kingewawezesha Barcelona kuelekea mbele katika kinyang'anyiro cha ubingwa wa ligi hiyo endapo timu hiyo ingeshinda.
Lakini kocha Luis Enrique alianza mchezo huo kwa kutowaanzisha wachezaji wake mashuhuri akiwemo Lionel Messi, Neymar na Dani Alves.
Barcelona ilishindwa kusawazisha goli walilojifunga wakati Moyes akipata ushindi wa pili akiwa meneja wa timu ya Sociedad.
Messi, Neymar na Alves walirejea katika mazoezi Ijumaa wiki iliyopita baada ya mapumziko marefu ya Krismasi Amerika Kusini ambako ligi ilisitishwa ili kusherehekea siku kuu hiyo.
Enrique alifanya mchezo wa kubahatisha kwa kutowapanga wachezaji hao katika mchezo wake na Real Sociedad ambayo imekuwa kikwazo kwa Barcelona katika michezo ya nyuma.

Wachezaji wa Real Sociedad wakishangilia goli katika moja ya michezo yao ya ligi kuu ya Hispania
Na kwa hiyo imethibitika kwa mara nyingine kwamba Barcelona hawana chao katika uwanja wa Anoeta sasa ikiwa ni michezo sita, Barcelona ikipoteza kwa Real Sociedad.
Kwa upande wake Real Madrid ilijikuta ikipoteza mchezo wake dhidi ya Valencia baada ya kucharazwa mabao 2-1 licha ya Real Madrid kuongoza kipindi cha kwanza kwa bao la penalti lililofungwa na Cristian Ronaldo dakika ya 14.
Valencia ilijipatia magoli yake yote mawili kipindi cha pili yakifungwa na Barragรกn dakika ya 52′ na Otamendi dakika ya 65.
Real Madrid inaongoza msimamo wa ligi ya Hispania ikiwa na pointi 39 katika michezo 16 ikifuatiwa kwa karibu na Barcelona yenye pointi 38 baada ya kucheza mechi 17.

No comments: