KUPIGWA chini kwa Yanga kwenye Kombe la Mapinduzi mjini hapa kumetibua mambo mawili.
Kwanza waandaaji wanalia kwamba mapato
yataporomoka, lakini kocha wa Simba, Goran Kopunovic, amesema atabadili
mbinu zake kuanzia leo Jumamosi.
Amesema watakomaa kwa kutumia nguvu kubwa
kuhakikisha kwa namna yoyote ile wanafanya kilichoishinda Yanga na Azam
ili kulinda heshima ya timu, mashabiki na hata kibarua chake.
Ikohivi; Azam FC iliondoka Zanzibar jana Ijumaa
asubuhi baada ya kutolewa katika Kombe la Mapinduzi wakati Yanga
wakijipanga kuondoka leo Jumamosi, lakini kuondolewa kwa timu hizo
zilizopewa nafasi ya kutwaa ubingwa kumemshtua kocha wa Simba,
Kopunovic, ambaye ametangaza mapambano.
Azam ilitangulia kutupwa nje katika hatua ya robo
fainali kwa kufungwa penalti 7-6 na Mtibwa Sugar mapema juzi Alhamisi
kabla ya Yanga kukumbana na kipigo cha bao 1-0 mbele ya JKU.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kopunovic, alisema
kutolewa kwa Azam na Yanga kumemshtua na sasa amewageukia wachezaji wake
akiwaambia hakuna kudharau chochote. Alisema hakufikiria kama timu hizo
zinaweza zisifike nusu fainali na sasa atauchukulia kwa uzito mkubwa
mchezo wao wa leo usiku dhidi ya Polisi ya Zanzibar.
Alisema wataingia uwanjani katika nusu fainali
hiyo wakiwa na fikra kwamba wanakutana na timu iliyomng’oa bingwa
mtetezi KCCA ya Uganda.
“Mpira ni mchezo wa makosa, Yanga walitengeneza
nafasi nyingi jana (juzi) lakini wakashindwa kuzitumia, ni tatizo
linaloweza kutokea hata kwetu, nimeshawaambia wachezaji wangu tutaingia
kwa akili moja ya kutengeneza nafasi na kuzitumia,”alisema Kopunovic.
“Hakuna aliyetarajia mambo yaliyotokea jana (juzi), hili ni kama somo kwetu kwamba tukifanya makosa nasi tutakwenda na maji.”
Katika nusu fainali nyingine, Mtibwa itacheza na JKU.
Mapato yaporomoka
Kutolewa kwa Yanga kumetibua mipango ya Chama cha
Soka Zanzibar (ZFA) kwani kilitarajia kipate fedha nyingi kwa mapato ya
milangoni.
Mashabiki na wadau wa soka wakiwemo viongozi wa soka visiwani
hapa, wengi wao walitarajia Yanga ingetinga fainali huku wakiipa nafasi
ya kucheza na Simba na kuingiza kiasi kikubwa cha fedha kutokana na
viingilio.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya ZFA, Ally Bakari,
alisema: “Ni kweli kuondolewa kwa Yanga kwenye michuano hii ni hasara
kwetu kwani ndiyo timu pekee iliyokuwa ikiongoza kuingiza mashabiki
wengi uwanjani, inayofuatia ni Simba.
“Kuna hasara kubwa itapatikana baada ya michuano
hii, ukiangalia tangu ianze mechi za Yanga ndiyo zilikuwa zinaongoza
kuwa na mashabiki wengi ikifuatiwa na Simba.
“Hivyo wengi walikuwa na imani kwamba Yanga na Simba zitakutana fainali na mapato yangepatikana mengi, lakini imekuwa kinyume.
“Mashabiki wamekuwa wengi uwanjani kila inapocheza
Yanga kwa kuwa timu hii haijashiriki Kombe la Mapinduzi kwa miaka
miwili, hivyo mashabiki wao wa hapa walikuwa na hamu ya kuiona timu yao
inafika fainali, hii ni hasara kubwa kwa waandaji pamoja na ZFA ambao
ndio wasimamizi wa soka hapa visiwani.”
Leo Jumamosi, Simba itacheza na Polisi wakati
Mtibwa Sugar itacheza na JKU katika nusu fainali ikiwa ni mara yao ya
pili kukutana kwenye mashindano haya, awali walikutana katika hatua ya
makundi na kutoka sare ya bao 1-1.
No comments:
Post a Comment