Wakati wananchi wakisubiri vigogo wa serikalini na mawaziri
wanaotuhumiwa kuhusika kwenye kashfa ya uchotaji fedha kwenye Akaunti ya
Tegeta Escrow kufikishwa mbele ya vyombo vya umma, ni watumishi watano
tu wa umma waliofikishwa mahakamani, lakini Mkurugenzi wa Takukuru, Dk
Edward Hoseah ana jibu la suala hilo; kazi yao ni kufikisha mahakamani
‘vidagaa’.
Katika kashfa hiyo ya Sh306 bilioni, mawaziri wa
sasa na zamani pamoja na makatibu wakuu wa wizara, wanatuhumiwa kwa njia
moja au nyingine kuhusika kwenye kufanikisha kwa makusudi au uzembe
uchotwaji wa fedha hizo, kuikosesha mapato Serikali na kupokea mgawo wa
fedha hizo, lakini hadi sasa ni watumishi wa Mamlaka ya Mapato (TRA),
Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi,
Tanesco na Benki Kuu (BoT) pekee waliofikishwa mahakamani.
Wote watano, ambao ni vigogo kwenye taasisi zao,
wameshtakiwa kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ili kufanikisha
mkakati huo ulioibuliwa na gazeti la The Citizen na baadaye Bunge
kulidaka na kufikia maazimio ya kutaka wahusika wote wawajibishwe na
mamlaka zinazowahusu.
Juzi, mkurugenzi huyo wa Takukuru aliliambia
gazeti hili kuwa taasisi yake itaendelea kuchunguza watu wote
waliohusika katika kashfa ya escrow bila ya ubaguzi, lakini akabainisha
kuwa kazi ya kuwapeleka mahakamani mawaziri na vigogo inatakiwa ifanywe
na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Dk Hoseah, ambaye aliwahi kuingia kwenye mzozo wa
DPP wa zamani kutokana na madai yake kuwa mafaili mengi ya kesi za
rushwa hayafanyiwi kazi, alisema sheria haiwaruhusu kuwapeleka
mahakamani mawaziri iwapo watabainika kuhusika kwenye vitendo vya
rushwa.
Kwa mujibu wa kifungu cha 57 cha Sheria Namba 11
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Mwaka 2007, endapo vigogo na
mawaziri watabainika kuhusishwa na vitendo vya rushwa, jalada la
uchunguzi wao litakabidhiwa kwa DPP ili achukue hatua ya kuwapeleka
mahakamani.
Dk Hoseah alisema kwa sasa Takukuru inaendelea na
uchunguzi wake mpaka itakapojihakikishia ushahidi wa kutosha dhidi ya
vigogo hao.
“Bunge lilitoa maazimio yake na likaagiza
kuchukuliwa hatua…Takukuru tulishaanza na tunaendelea na uchunguzi.
Taratibu zote zikishakamilika kisha ushahidi ukapatikana kwa vielelezo
vyote, basi watafikishwa mahakamani wala hakuna tatizo lolote,” alisema.
“Lakini watafikishwa mahakamani baada ya sisi
kuwasilisha jalada letu la uchunguzi kwa DPP ambaye ndiye mamlaka ya
kuwafikisha mahakamani kama sheria inavyotuagiza.”
Udhaifu huo wa sheria pia ulizungumziwa na Bunge
wakati wa kujadili kashfa ya escrow na kuazimia kuwa sheria inayounda
Takukuru ifanyiwe kazi ili iwe na mamlaka hayo ya kufikisha mahakamani
vigogo wa rushwa kubwa.
Waliohusishwa na rushwa
Mawaziri waliotajwa kwenye sakata hilo ni Profesa
Anna Tibaijuka, ambaye alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi na ambaye aliingiziwa Sh1.6 bilioni na mwanahisa wa zamani wa
Kampuni ya IPTL, James Rugemarila. Tibaijuka alivuliwa wadhifa huo
kutokana na sakata hilo.
Wengine ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo, ambaye Rais Jakaya Kikwete alisema amemuweka kiporo baada ya
Bunge kumuona kuwa hakushughulikia vizuri suala hilo na kuisababishia
Serikali kukosa mapato.
Wengine ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti
na ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu, Andrew Chenge, ambaye aliingiziwa
pia Sh1.6 bilioni kwenye akaunti yake na Rugemarila; waziri wa zamani wa
Nishati na Madini, William Ngeleja, aliyeingiziwa Sh40.4 milioni;
aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh40.4
milioni), mbunge wa zamani wa Sumbawanga (CCM), Paul Kimiti (Sh40.4
milioni) na aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk Enos Bukuku (Sh161.7
milioni).
Vigogo waliotajwa kwenye sakata hilo ni Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliackim Maswi, ambaye
amesimamishwa, Fredrick Werema, ambaye alijiuzulu kwa maelezo kuwa
ushauri wake kuhusu suala la kodi kwenye fedha hizo haukueleweka na
ulisababisha tafrani.
Awali, Dk Hoseah aliliambia gazeti dada la The
Citizen kwamba katika uchunguzi wake, hakuna kiongozi wala kigogo yeyote
ambaye atapona.
“Yeyote yule ambaye atabainika katika uchunguzi
wetu, lazima afikishwe mbele ya sheria, hakuna kigogo wala kiongozi
yeyote ataweza kukwepa endapo ushahidi utaonekana wazi,” alisema.
Alipoulizwa kama uchunguzi huo unamjumuisha
Profesa Tibaijuka, mkurugenzi huyo alisema hawezi kutaja jina la mtu kwa
kuwa ni kinyume cha sheria kutaja jina au taarifa ambazo ziko kwenye
uchunguzi.”
Waliofikishwa mahakama ya Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu hadi sasa ni Mhandisi Mkuu wa Mradi wa Umeme Vijijini (Rea),
Theophillo Bwakea na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma, ambao kwa
pamoja wanadaiwa kupokea rushwa ya Sh485.1 milioni.
Wengine ni Meneja Misamaha ya Kodi wa TRA,
Kyabukoba Leonard Mutabingwa, Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco, Steven
Roman Urassa na Mkurugenzi wa Fedha BoT, Julius Rutta Angello
wanaokabiliwa na mashtaka ya kuomba na kupokea rushwa ya jumla ya
Sh1.923 bilioni.
Maoni ya wasomi
Akizungumzia suala hilo, Profesa Gaudence
Mpangalla kutoka Chuo Kikuu cha Ruaha alihoji sababu za Serikali
kushindwa kuchukua hatua za haraka kuijengea uwezo Takukuru ili iweze
kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa aina hiyo.
“Kama tunavyoona hivi sasa inawapandisha kizimbani
watumishi wengine, sasa kuna tofauti gani na waziri atakayebainika
kukutwa na kosa kama hilo? Sioni tofauti yoyote kwa wakosaji hao,”
alisema.
“Udhaifu huo unaweza kujenga imani kwamba Serikali
inawabeba mafisadi kwa mgongo wa ofisi ya DPP kwa sababu mashtaka mengi
hayafanyiwi kazi katika ofisi hiyo.”
Mara kadhaa Dk Hoseah amekuwa akitoa kauli zinazoonyesha kuwa
ameshawasilisha majalada mengi ofisi ya DPP, lakini amekuwa akiyakalia
au kuyarudisha kutaka uchunguzi ukamilike.
Hata hivyo, Profesa Chris Maina wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anaona hilo halitafanyika kwa hivi sasa.
“Kwa jinsi sakata hilo lilivyoibuliwa na ushahidi
kuwekwa wazi na Rais akaonyesha hisia zake, lazima DPP ajaribu kuwa
makini sana na mawaziri au vigogo watakaofikishwa mbele yake,” alisema.
“Inamlazimu achukue hatua za haraka. Hili suala
siyo sawa na mashtaka mengine… lakini tusubiri kwa sababu ni kiongozi
mpya aliyeingia ofisi hiyo hatujui itakuwaje.”
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment