MFUNGAJI Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, straika Amissi
Tambwe, amesema haelewi tatizo ni nini, lakini yaliyomtokea kwenye mechi
mbili za mwisho za Yanga kwenye Kombe la Mapinduzi ni maajabu kwake.
Tambwe amemaliza michuano hiyo bila kuwa na bao, lakini akasema hatasahau mechi hizo.
Akizungumza na mwandishi wetu, Mrundi huyo ambaye
aliifungia Simba mabao 19 katika msimu uliopita wa ligi, alisema siyo
jambo geni kwake kupoteza nafasi za kufunga, lakini nafasi ambazo
amezipoteza katika mechi dhidi ya Shaba na JKU hatazisahau.
Tambwe alisema hajui nini kilitokea wakati
akimalizia nafasi ambazo alikuwa akizipata uwanjani kwani hali hiyo
haijawahi kumtokea tangu atue nchini.
“Sijui nini kimenitokea, sijawahi kukosa mabao ya
namna hii, nafasi kama hizi ndiyo siku zote nimekuwa nafunga
nimejishangaa sana kwa kweli,” alisema Tambwe.
“Siku zote nimekuwa sitaki kujiamini kupita kiasi
ili niweze kufunga, lakini nilivyofanya hadi nikakosa sijui nini
kimetokea, acha tu ndio mpira.”
Tambwe alikosa kufunga akiwa katika nafasi nzuri
katika mechi ya makundi dhidi ya Shaba ambayo Yanga ilishinda bao 1-0,
pia alishindwa kufunga dhidi ya JKU katika robo fainali juzi Alhamisi
walipofungwa bao 1-0.
No comments:
Post a Comment