Kamanda kova |
Vijana zaidi ya mia tano wanashikiliwa na Jeshi la Polisi nchini Tanzania
kwa tuhuma za kujihusisha na Vitendo vya uhalifu vilivyozua taharuki na
hofu kubwa mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.
Vijana hao wanatuhumiwa kusababisha hofu kubwa jijini Dar es Salaam
kwa kile kilichoelezwa kitendo cha kulipiza kisasi kufuatia kifo cha
mwenzao aliyefariki kwa kupigwa mawe na wananchi waliojichukulia sheria
mkononi.Kamanda wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salam Suleiman Kova amethibitisha kukamatwa kwa Vijana hao kwa tuhuma za uhalifu jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita
Vijana hao zaidi ya mia tano wakiwa washiriki wakuu katika Kundi la vijana waporaji lijulikanalo kama Panya Road wanashikiliwa na Jeshi la polisi kufuatia msako mkali unaoendelea jijini kote Dar es Salaam baada ya tukio la mwishoni mwa wiki ambapo jiji la Dar es Salaam lilikumbwa na taharuki kubwa baada ya vijana hao kuanza kufanya vitendo vya uporaji mitaani.
Kova amesema katika msako huo unaoendelea mbali na kuwakamata vijana hao katika msako huo pia wamekamatwa wakiwa na Puli,kete na misokoto ya Bangi pamoja na Mirungi na Lita 150 za pombe haramu ya Gongo.
Watuhumiwa hao wamekamatwa katika maeneo mbali mbali jijini Dar Es Salaam katika sehemu mbali mbali kama kwenye vituo vya mabasi ,kwenye majumba mabovu na pia kwenye makazi yao kutokana na msako huo kufanyika nyumba kwa nyumba.
Hii ni mara ya kwanza kwa kundi kubwa la watuhumiwa kukamatwa kwa wakati mmoja na kushikiliwa huku wakisubiri kufikishwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment