Kaya 5,000 za wakulima na wafugaji katika Kata za Isansa na
Igamba, wilayani Mbozi zitaingia kwenye mfumo maalumu wa uchumi
utakaohusisha ufugaji ng’ombe wa maziwa kwa lengo kupambana na umaskini.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Heifer-Tanzania, Dk
Henry Njakoi alisema hayo juzi wakati wa akizindua wa mradi wa
kuboresha ustawi wa maisha ya wakulima na wafugaji mjini hapa.
Dk Njakoi alisema mradi huo unatekelezwa chini ya
Heifer-Tanzania na kaya 2,000 kati ya 5,000 zitaingizwa moja kwa moja
kwenye mpango wa thamani ya maziwa kupitia mfumo wa kitovu cha biashara
ya maziwa.
“Mradi huu utawapatia wafugaji wapya ng’ombe wa
maziwa 400 na kuwapa mafunzo kwa njia ya shamba darasa wakulima 1,600,”
alisema Dk Njakoi na kuongeza:
“Tunataka wananchi wawe na vyanzo zaidi vya mapato ili kukabiliana na hali ngumu ya maisha.”
Alisema kupitia mradi huo, wananchi wa wilaya hiyo
wataongeza kipato kwa njia ya kushiriki kazi za uzalishaji maziwa,
kupata maji safi na nishati mbadala kwa mahitaji ya nyumbani.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Rosemary Senyamle alisema mpango wa
sasa wa Serikali ni kutaka kuona wananchi wananufaika na ufugaji.
Alisema Serikali ina mpango wa kuhakikisha maziwa yanazalisha faida katika jamii.
“Niseme tu kwamba, mradi huu unaimarisha sawia
juhudi za Serikali kujenga uchumi wa wananchi na kuifanya Tanzania
ijitegemee katika kuzalisha na kusindika bidhaa za maziwa,” alisema
Senyamle.
No comments:
Post a Comment