Panga pangua ya saba ya Baraza la Mawaziri
iliyofanyika juzi imefikisha mawaziri 61 waliotemwa, kujiuzulu au
kufariki dunia tangu Rais Jakaya Kikwete aingie madarakani mwaka 2005,
huku mawaziri 16 wakihimili mawimbi hayo hadi sasa.
Katika mabadiliko hayo saba yaliyofanywa katika
kipindi cha miaka tisa, wako waliobadilishwa wizara, kupandishwa kutoka
naibu waziri kuwa waziri kamili, huku sura mpya zikiingizwa.
Mabadiliko hayo yalitokana na mawaziri kutakiwa
kuwajibika kutokana na kashfa mbalimbali, huku mengine yakitokana
mawaziri kufariki na moja likitokana na Waziri Asha-Rose Migiro
kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Katika panga pangua hiyo, mawaziri 16 wamefanikiwa
kudumu katika baraza hilo tangu Rais Kikwete aingie madarakani ambao ni
Sofia Simba, Profesa Mark Mwandosya, Stephen Wasira, Dk Hussein Mwinyi
na Dk John Magufuli.
Wengine ni Profesa Jumanne Maghembe, Dk Shukuru
Kawambwa, Hawa Ghasia, Dk Mary Nagu na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye
kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo, alikuwa naibu waziri na baadaye
waziri wa Tamisemi.
Mawaziri wengine waliopo sasa ambao mwaka 2005
walikuwa manaibu mawaziri ni Gaudencia Kabaka, Bernard Membe, Celina
Kombani, Christopher Chiza na Mathias Chikawe.
Naibu waziri pekee ambaye alikuwamo katika baraza
la mawaziri la kwanza la Rais Kikwete akiwa na wadhifa huohuo ni Dk
Makongoro Mahanga ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira.
Waliotemwa
Mawaziri waliotemwa au kujiuzulu tangu Rais
Kikwete aingie madarakani, wakiwamo wale walioshindwa katika
kinyang’anyiro cha ubunge ni Edward Lowassa, ambaye alijiuzulu, Antony
Diallo, Dk Ibrahim Msabaha, Basil Mramba, John Chiligati, Andrew Chenge,
Joseph Mungai, Dk Emmanuel Nchimbi, Lawrence Masha, Mustafa Mkulo,
William Ngeleja, Dk Cyril Chami, Omary Nundu, Bakari Mwapachu na
Kingunge Ngoimbale-Mwiru.
Wengine ni Ezekiel Maige, Dk Hadji Mponda, Teresa
Huvisa, Shamsi Vuai Nahodha, Nazir Karamagi, Dk Mathayo David, Khamis
Kagasheki, Profesa Anna Tibaijuka, Profesa Sospeter Muhongo, Dk Batilda
Buriani, Joseph Mungai, Diodorus Kamala, Mohamed Seif Khatib, Mwantumu
Mahiza, Profesa Peter Msola na Profesa David Mwakyusa, Philip Marmo na
Juma Ngasongwa.
Naibu mawaziri ni Dk Luca Siyame, Balozi Seif Ally
Idd, Hezekiah Chibulunje, Shamsa Mwangunga, Daniel Nsanzugwanko,
Hezekiah Chibulunje, Rita Mlaki, Dk Charles Mlingwa, Zabein Mhita,
Athuman Mfutakamba, Dk Lucy Nkya, Goodluck Ole Medeye, Benedict Ole
Nangoro, Gregory Teu, Philipo Mulugo, Mohamed Abood, Dk Aisha Kigoda,
Omari Yusuf Mzee, Jeremiah Sumari, Dk Maua Daftari, Zakia Meghji, Joel
Bendera, Abdisalaam Issa Khatib na James Wanyancha.
Pia, wapo ambao walifariki dunia ambao ni Salome Mbatia, Juma Akukweti, Jeremiah Sumari na William Mgimwa.
Badiliko la Kwanza
Katika baraza lake la kwanza Rais Kikwete aliteua
mawaziri na naibu mawaziri 60 Januari 2006 na ilipofika Oktoba 2006,
Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya kwanza makubwa ya baraza lake la
mawaziri kwa kuwahamisha vituo vya kazi mawaziri 10 na naibu mawaziri
wanane.
Mawaziri waliohusika na mabadiliko hayo ni Diallo
(Maliasili na Utalii) ambaye alihamishiwa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo
na Profesa Maghembe (Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana) kupelekwa
Wizara ya Maliasili na Utalii.
Dk Msabaha (Nishati na Madini) alihamishiwa Wizara
ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Karamagi (Viwanda na Biashara)
alihamishiwa Wizara ya Nishati na Madini, Mramba (Miundombinu)
alihamishiwa Viwanda na Biashara na Chiligati (Mambo ya Ndani)
alihamishiwa Wizara Kazi, Ajira na Vijana.
Mawaziri wengine ni Chenge (Ushirikiano Afrika
Mashariki) alihamishiwa Wizara ya Miundombinu, Dk Kawambwa (Maendeleo ya
Mifugo) alihamishiwa Wizara ya Maji, Wasira (Maji) alihamishiwa Wizara
ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Mungai (Kilimo, Chakula na Ushirika)
alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani.
Naibu Mawaziri waliohamishwa wizara zao na
kupelekwa wizara nyingine ni Dk Nchimbi (Habari, Vijana, Michezo na
Utamaduni) kwenda Wizara ya Kazi, Nsanzugwanko (Kazi na Ajira) kwenda
Wizara ya Habari, Michezo na Utamaduni, Dk Mathayo (Biashara na Viwanda)
kwenda Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Chibulunje (Kilimo,
Chakula na Ushirika) kwenda Wizara ya Viwanda na Biashara.
Wengine ni Dk Buriani (Wizara ya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto) kuhamishiwa Wizara ya Mipango, Uchumi na
Uwezeshaji, Mbatia (Mipango, Uchumi na Uwezeshaji) kwenda Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Masha (Nishati na Madini) kwenda
Mambo ya Ndani na Membe (Mambo ya Ndani) kuwa Naibu Waziri wa Nishati na
Madini.
Badiliko la Pili
Februari 2007, Rais Kikwete alifanya uteuzi wa
mawaziri wawili na naibu waziri wawili baada ya aliyekuwa Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk Asha-Rose Migiro kuteuliwa
kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Nafasi ya Migiro
ilichukuliwa na Membe.
Dk Buriani aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Bunge na Uratibu) kujaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya kifo cha
Akukweti. Kabla ya uteuzi huo Buriani alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya
Mipango, Uchumi na Uwekezaji.
William Ngeleja aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa
Nishati na Madini na Gaudence Kayombo aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa
Mipango, Uchumi na Uwekezaji.
Badiliko la tatu
Februari 12, 2008 baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu,
Edward Lowassa kujiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond, Kikwete
alivunja Baraza la Mawaziri na kuliunda upya.
Lowassa alijiuzulu sambamba na waliokuwa mawaziri
wawili Dk Msabaha na Karamagi ambao wote walikuwa wameiongoza Wizara ya
Nishati na Madini kwa nyakati tofauti. Nafasi zao zilizibwa na William
Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Kamala (Afrika Mashariki), huku Pinda
akiteuliwa kuchukua nafasi ya Lowassa.
Badiliko la nne
Rais Kikwete alifanya mabadiliko mara ya nne
katika baraza lake Mei, 2008 baada ya Chenge, ambaye ni mbunge wa
Bariadi, kujiuzulu kutokana na kashfa ya ununuzi wa rada na nafasi yake
kujazwa na mbunge wa Bagamoyo, Dk Kawambwa huku Rais Kikwete pia
akibadilisha mawaziri kadhaa.
Badiliko la tano
Mei 2012, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya tano
katika baraza lake baada ya kuwaondoa mawaziri sita baada ya ripoti ya
Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kubaini kuwa walikiuka
maadili ya utumishi wa umma na kushindwa kuwajibika kisiasa kusimamia
mali za umma.
Katika mabadiliko hayo waliondolewa walikuwa ni Mkulo (Fedha),
Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Maige
(Maliasili na Utalii), Nundu (Uchukuzi) na Dk Chami (Viwanda na
Biashara). Wengine waliotemwa ni Mfutakamba (Naibu, Uchukuzi) na Naibu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Nkya.
Mawaziri walioziba nafasi hizo ni William Mgimwa
(Fedha), Kagasheki (Utalii), Dk Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), Dk
Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara), Dk Mwinyi (Afya), Profesa Muhongo
(Nishati na Madini), Dk Seif Rashid (Naibu, Afya) na George
Simbachawene (Naibu, Nishati na Madini).
Manaibu wapya walioingia ni January Makamba
(Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Dk Charles Tizeba (Uchukuzi) na
Amos Makala (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo). Wengine ni Dk
Binilith Mahenge (Maji), Stephen Masele (Nishati na Madini), Angela
Kairuki (Katiba na Sheria), Janet Mbene na Saada Mkuya Salum (Fedha).
Badiliko la sita
Januari 19, 2014, Rais Kikwete alifanya mabadiliko
katika Baraza la Mawaziri kwa kuteua mawaziri wapya wawili na manaibu
mawaziri wapya wanane, huku akiwapandisha vyeo manaibu mawaziri wanne
kuwa mawaziri kamili.
Katika mabadiliko hayo, Rais Kikwete aliwapumzisha
Dk Terezya Huvisa, ambaye alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Mazingira), Gregory Teu, aliyekuwa Naibu Waziri wa Viwanda na
Biashara na Philipo Mulugo aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi.
Wengine waliopumzishwa ni Benedict Ole-Nangoro
aliyekuwa naibu waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Goodluck
Ole-Medeye aliyekuwa naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi.
Mabadiliko hayo yalikuwa yanalenga kujaza nafasi
zilizoachwa na Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii, Dk Nchimbi
(Mambo ya Ndani ya Nchi), Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na
Dk Mathayo (Maendeleo ya Mifugo) waliotemwa Desemba 2013 kutokana na
kashfa ya Operesheni Tokomeza na nafasi ya Dk Mgimwa, aliyefariki dunia
kutokana na maradhi.
Mawaziri wapya walioteuliwa wakati huo ni Dk
Asha-Rose Migiro (Katiba na Sheria), Dk Titus Kamani kuwa Waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Wengine aliowateua kuwa naibu mawaziri ni Mwigulu
Nchemba, Naibu Waziri wa Fedha, Dk Kebwe Stephen, Naibu Waziri, Afya na
Ustawi wa Jamii na Jenista Mhagama, naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi.
Pia, Dk Pindi Chana aliteuliwa kuwa Naibu Waziri
wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na Kaika Telele, Naibu Waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi. Wengine ni Godfrey Zambi, naibu Waziri
Kilimo, Chakula na Ushirika, Juma Nkamia, Naibu Waziri Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo na Mahmoud Mgimwa, Naibu Waziri, Maliasili na
Utalii.
Naibu mawaziri waliopandishwa kuwa mawaziri ni Saada Mkuya
(Waziri wa Fedha), Lazaro Nyalandu (Maliasili na Utalii) na Dk Seif
Seleman Rashidi ( Afya na Ustawi wa Jamii), Dk Binilith Mahenge
alipandishwa kutoka Naibu Waziri wa Maji na kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais (Mazingira).
Dk Hussein Ali Mwinyi alihamishwa kutoka Afya na
Ustawi wa Jamii kwenda Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na wengine
kadhaa walihamishwa.
Badiliko la saba
Juzi, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya saba
ambayo yanawezekana kuwa yatakuwa ya mwisho kutokana na kusalia miezi
sita kabla ya kuvunjwa kwa Bunge kupisha Uchaguzi Mkuu utakaofanyika
Oktoba.
Mabadiliko hayo baada ya mawaziri wawili, Profesa
Tibaijuka (kufutwa kazi) na Profesa Sospeter kujiuzulu kutokana na
kuhusishwa na kashfa ya Tegeta Escrow.
Walioingia ni manaibu waziri wawili, Charles
Mwijage (Nishati na Madini) na Anna Malecela (Elimu na Ufundi). Wengine
walihamishwa ambao ni Wasira kutoka Ofisi ya Rais kwenye Kilimo na
Ushirika, Lukuvi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi.
Wengine ni Dk Nagu kwenda Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu) na Jenister Mhagama (Waziri Mkuu, Uhusiano, Uratibu na Bunge).
Dk Harrison Mwakyembe anahamia Afrika Mashariki
(kutoka Uchukuzi) na nafasi yake inachukuliwa na Sitta akitokea Wizara
ya Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment