Monday 12 January 2015

CCM wamshambulia mdhamini CHADEMA

Muslim HassanaliMJUMBE wa Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Muslim Hassanali, amedai kushambuliwa na Katibu Kata wa Kisutu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Sauda Addey, baada ya mjumbe huyo kukataa kubandikwa kipeperushi cha wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa serikali za mitaa kupitia CCM mbele ya eneo lake la biashara.
Hassanal, anadai tukio hilo lilitokea Jumamosi saa tano asubuhi, baada ya wafuasi wa CCM kubandika kipeperushi chao katika eneo lake la biashara lililopo mtaa wa Mali Kisutu jijini Dar es Salaam.
Kushambuliwa kwa Hassanal, kumekuja ikiwa ni siku chache zimepita huku baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa katika maeneo mbalimbali nchini wakiwa wameshashambuliana na wengine kupoteza maisha.
Akizungumzia namna alivyoshambuliwa, Hassanal alisema baada ya kufika ofisini kwake, alikuta kipeperushi hicho na alipouliza watu aliowakuta wakamuambia kuwa makarataisi hayo yamewekwa usiku na kwamba hawamjui aliyeweka.
“Kisheria lile ni eneo langu ninalolimiliki kibiashara, hivyo yeyote anayetaka kulitumia ni lazima aonane na mimi nimpe ruhusa ama la, sasa hawa CCM wamekuja kuweka pasipo ridhaa yangu na mimi siipendi CCM, nikiona hata rangi zao nasikia kichefu chefu nikaona ngoja niziondoe,” alisema Hassanal na kuongeza;
Unajua ile ni sehemu ya biashara wanafika watu wa kila itikadi, sasa kubandika picha kama zile zinaweza kuvuruga biashara zangu, isitoshe kwa kulitambua hilo ndio maana nimeshindwa hata kubandika picha za wagombea wa CHADEMA ambacho ni chama changu.
Alidai kuwa, baada ya kuyaondoa matangazo hayo viongozi wa Kata hiyo wa CCM wakiambatana na wafuasi wao, walimvamia na kumfanyia vurugu zilizosababisha uharibifu wa miwani yake ya macho, vifaa, nyaraka na upotevu wa baadhi ya vitu.
Alisema kutokana na fujo hizo, alifika kituo cha Polisi Kisutu, ambako wakamueleza hawana mamlaka ya kushughulikia kesi za kisiasa, hivyo alifikishe suala hilo kituo kikuu cha kati.
Hassanali, alisema baada ya kushauriwa hivyo, aliamua kwenda kituo hicho lakini cha kusikitisha hakuweza kupata ushirikiano wa kutosha na alitakiwa kurudi kituoni hapo Jumatatu, ambako alifanya hivyo.
“Leo kama mnavyoniona hapa bado nasumbuliwa, nataka kufungua jalada lakini bado wahusika wanazunguka tu kwa kunieleza kuwa msimamizi wa shauri langu hajafika, hata hivyo niliweza kuhojiwa na kuandika maelezo yangu,” alisema.
Wakili wa Hasanali, Fredrick Kihwelo, alikiri mteja wake kufanyiwa vurugu na kwamba baada ya kufika polisi, waliandika maelezo na kuambiwa uchunguzi unaendelea.
“Pamoja na kukwama siku ya Jumamosi, leo tumekuja tena, tangu asubuhi tuko hapa na hatimaye tumefungua kesi ya jinai, kimsingi suala hili litakuwa kwenye uchunguzi baada ya hapo litapelekwa kwa DPP ambaye ndio ataamua kama litapelekwa mahakamani,” alisema wakili huyo.
Kwa upande wake, Sauda alisema zoezi la kubandika picha za wagombea limefanyika Jiji zima kisheria tangu miaka ya nyuma na hakutegemea katika eneo hilo kama angekuwepo mtanzania mwenye asili ya Asia asiwe mfuasi wa CCM.
“Sisi hatukujua kama pale kuna mtu wa CHADEMA tena Muhindi, kama tungejua tusingebandika, kwani kwa zaidi ya miaka 25 tumekuwa tukibandika,” alisema Sauda.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Mary Nzuki, alisema suala hilo bado liko kwa mkuu wa kituo kwa ajili ya uchunguzi na mara litakapokamilika litafikishwa kwake kwa hatua zaidi.

No comments: