Friday 30 January 2015

Awatisha watangazaji kwa bunduki bandia studioni

Mwanamume aliyekuwa ameshika bunduki bandia amekamatwa ndani ya studio ya matangazo ya televisheni nchini Uholanzi na kusababisha matangazo kusitishwa kwa muda.
Wafanyakazi waliamrishwa kutoka nje ye jengo lenye studio hizo katika eneo la Media Park mjini Hilversum.
Mtu huyo aliyekuwa amevalia suti akiwa amebeba kilichofanana na bunduki, aliingia katika studio hizo na kutaka apewe muda wa kuongea hewani.
Baadaye polisi walifanikiwa kumkamata baada ya kumshinda nguvu.
Maafisa wa polisi walisema mwanamue huyo anazuiliwa kwa kosa la kushukiwa kutoa vitisho , kumiliki silaha na kumteka mtu.
Polisi walifanya msako katika jengo hilo na kuhakikisha hali kuwa shwari.
Waziri wa usalama Ivo Opstelten alisema mshukiwa alikuwa pekee yake katika njama yake.
Nia na lengo la kitendo cha mwanamume huyo hata hivyo haikubainika. Vyombo vya habari nchini Uholanzi, viliripoti kwamba mshukiwa aliaminika kuwa mwanafunzi wa chuo cha mafunzo ya anuai na kwamba aliwapoteza wazazi wake hivi karibuni.
Mshukiwa alinaswa akisema :''vitu ambavyo nitavisema , ni mambo makubwa ya kidunia.Tulikodiwa na shirika la ujasusi.''
Barua yenye vitisho ambayo mwanamume huyo aliikabidhi kwa wafanyakazi wa kituo hicho ilionya dhidi ya mashambulizi ya bomu na uvamizi wa mitandao ikiwa angezuiwa kwenda hewani.Barua hio ilichapishwa kwenye mtandao wa kituo hicho.
Mwandishi mmoja wa habari aliyezungumza na mshukiwa huyo, alisema alidai kutoka kwa kundi la wavamizi wa mitandao, "hackers' collective"
Mwanamume huyo alikuwa amevalia shati leusi na tai huku akiwa amebeba kilichoonekana kama bunduki nyeusi na alionekana kwenye video akiwa anatembea tembea kwenye studio.
Polisi walipoingia katika kituo hicho, waliamwamrisha kuiangusha bunduki yake kitendo alichokifanya huku polisi wakimfunga pingu mikononi.

No comments: