Monday 12 January 2015

Simba mwendo mdundo yaikebehi Yanga

SIMBA ni kama wanawakebehi watani wao Yanga ambao juzi Alhamisi waliondoshwa kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi na JKU ya Zanzibar.
Unajua Msimbazi wamesemaje? Wamesema wao hawana lelemama na watakomaa na kuhakikisha wanatinga fainali na kutwaa taji.
Simba ilifanikiwa kutinga nusu fainali ya mashindano hayo mapema Jumatano baada ya kuifunga Taifa Jang’ombe mabao 4-0 na leo Jumamosi inacheza na Polisi Zanzibar kusaka tiketi ya fainali.
Polisi wao walitinga hatua hiyo baada ya kuwavua ubingwa KCCA ya Uganda kwa penalti 5-4 baada ya matokeo ya suluhu ndani ya dakika 90.
Nusu fainali nyingine itakuwa kati ya Mtibwa Sugar na wababe wa Yanga ambao ni JKU, utakuwa kama marudio ya ule wa hatua ya makundi uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Mtibwa imetinga hatua hiyo baada ya kuifunga Azam kwa penalti 7-6 baada ya sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90 wakati JKU wao waliifunga Yangao bao 1-0. Mechi zote zitachezwa Uwanja wa Amaan.
Kocha wa Simba, Goran Kopunovic alisema ameshtushwa na kitendo cha Azam na Yanga kuondoshwa katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo lakini amewaambia wachezaji wake kuwa wakomae na kuupa uzito mchezo huo ili waweze kutinga fainali na kutwaa taji hilo.
“Tunaingia kwa akili moja ya kutengeneza nafasi na kuzitumia, tunaingia kwa umakini mkubwa, tumedhamiria kutinga fainali na kutwaa taji hili,” alisema kocha huyo.
Naye kocha wa Mtibwa, Mecky Maxime, amesema hatma ya mchezo wao wa leo na JKU iko mikoni mwa wachezaji wake kwani wanafahamu ni kitu gani wanatakiwa kukifanya uwanjani ndani ya dakika 90 za mchezo huo.
“Tulimaliza maandalizi ya mechi hizi tangu tuko kwetu Morogoro, tumekuja huku kucheza na wachezaji wangu wanafahamu kuwa tunahitaji nini, tunawafahamu JKU na tulicheza nao kwenye mchezo wa makundi, ni timu nzuri na upinzani utakuwa mkubwa,” alisema Maxime.
Ligi Kuu Bara
Kwenye mechi za Ligi Kuu Bara leo Jumamosi Ndanda FC ya Mtwara itaikaribisha Polisi Morogoro kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
Ndanda ina pointi tisa baada ya kushinda mechi tatu na kupoteza sita nyingine za msimu huu na inashika nafasi ya 12.
Polisi wao wapo kwenye nafasi ya tano na pointi zao 13 baada ya kushinda michezo mitatu, sare nne na kupoteza miwili huku wakiwa wamefunga mabao manane na kufungwa saba katika mechi tisa zilizopita.
Kwenye Uwanja wa Azam Complex, leo Jumamosi JKT Ruvu itakuwa wenyeji wa Stand United ya Shinyanga. Ruvu inashika nafasi ya sita na pointi zake 13 baada ya kushinda michezo minne, sare moja na kupoteza mingine minne huku pia ikiwa na mabao nane ya kufunga na nane ya kufungwa.
Stand wao wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa wanashika nafasi ya tisa na pointi zao 11 baada ya kushinda mechi mbili, sare tano na kupoteza michezo mingine miwili. Hata hivyo timu hiyo haijawahi kupoteza mechi yoyote ugenini.
Kesho Jumapili, Mgambo JKT itacheza na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga. Mgambo inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi tisa baada ya kushinda mechi tatu pekee na kufungwa nyingine tano. Imefunga mabao manne na kufungwa tisa katika mechi hizo.
Ruvu Shooting inaingia kwenye mchezo huo ikiwa inashika nafasi ya nane na pointi zake 11 baada ya kushinda mechi tatu, sare mbili na kupoteza mechi nyingine nne. Imefunga mabao matano na kufungwa saba katika mechi hizo tisa za awali.
Kocha wa Mgambo, Bakari Shime alisema: “Nawafahamu Ruvu Shooting ni timu nzuri na hilo linaufanya mchezo kuwa mgumu zaidi, lakini tutacheza kwa kushambulia kwa dakika zote 90 ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri.”
Kocha wa Ruvu Shooting, Tom Olaba alisema: “Sijabahatika kuwaona Mgambo siku za karibuni lakini nitatumia dakika 45 za kwanza kuwasoma, baada ya hapo ni vita kali.”

No comments: