Klabu ya Simba imethibitisha kuachana na kocha msaidizi wa timu
hiyo, Seleman Matola na kueleza kumweka hadharani mrithi wake
atakayesaidiana na kocha mkuu, Goran Kopunovic wakati wowote kuanzia
sasa.
Mapema jana, Rais wa Simba, Evance Aveva alieleza
kupokea barua ya kujiuzulu kwa Matola na kubainisha kuwa katika barua
hiyo, Matola ameeleza kutingwa na majukumu ya kifamilia hivyo hawezi
kuendelea kuinoa Simba kama kocha msaidizi.
Alipotafutwa na gazeti kuzungumzia uamuzi wake
huo, Matola alitaka aulizwe vizuri Aveva ndiye alitolee ufafanuzi suala
hilo na si yeye kwani tayari ameachana na klabu hiyo.
Hata hivyo, kocha huyo alionekana kupoteza mvuto
kwa baadhi ya mashabiki ambao mara kadhaa wamekuwa wakimshinikiza
ang’atuke Simba.
Kwa mujibu wa Aveva, Simba imepokea barua ya
kujiuzulu kwa kocha huyo juzi ikiwa ni siku moja baada ya Simba kuruhusu
kipigo cha magoli 2-1 dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa.
Pia, Aveva amekiri jahazi la timu yao kuendelea
kuzama kutokana na kutoka sare mfululizo na kupoteza mechi mbili kwenye
ligi na kuwa timu ya nne kutoka mwisho na pointi 13 katika mechi 11
ilizocheza.
“Ni kweli timu yetu inakwenda mrama, matokeo
tunayopata hayaridhishi hata kidogo, kama uongozi tulikutana na benchi
la ufundi kuhusu hali ya timu yetu ambao wametuambia ni kutokana na
ratiba ya ligi kuwabana.
“Leo, kocha Goran Kopunovic anatimiza siku 30
tangu alipoanza kuinoa Simba, katika kipindi hicho ameiongoza Simba
kucheza mechi kumi na kwa uwiano katika kila siku tatu wanacheza mechi
moja.
“Kwa hali hii, timu inachoka, wenzetu Yanga na
Azam walitolewa mapema, hivyo kupata muda zaidi wa kujiandaa tofauti na
sisi ambao tumecheza hadi mwisho,” alisema Aveva.
Akizungumzia mpasuko katika klabu yao, Aveva
alisema hawana mpasuko wowote na sasa wanajipanga ili kuhakikisha timu
yao inarejesha makali kwenye ligi kwa kushirikiana pamoja na kuwataka
mashabiki kuwa na subira.
No comments:
Post a Comment