uwanja wa Mwalimu Nyerere |
Kamanda wa Polisi wa JNIA, Khamis Suleiman
alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Hussain Ahmed Ally Mansour(34), raia wa
Kuwait ambaye alikamatwa uwanjani hapo jana majira ya saa 5 usiku
wakati akijiandaa na safari ya kuelekea nchini Kuwait kupitia Dubai
na Shirika la Ndege la Emirates .
Kamanda Selemani alisema Mansour alikamatwa na
wanyama hao ambao aliwahifadhi kwenye mifuko midogo midogo ilivyowekwa
katika begi kubwa lenye rangi nyeusi.
“Kenge waliwekwa kwenye mifuko midogo midogo 15 na
kila mmoja kuna kenge 15 na mifuko mingine walikaa wawili,”alisema
kamanda Selemani.
Alisema kati ya Kenge hao, 15 walikufa na walio hai walikuwa 134 ambao walikuwa wamefichwa kwenye mifuko hiyo.
Seleman alisema wakati wanafanyiwa upekuzi ndipo
walipogundua kuna vitu ambavyo vinafanana na nyoka na kuamua
kuwashirikisha wataalamu wa maliasili ambao walibaini kuwa begi hilo
lilikuwa na Kenge.
“Huyu mtuhumiwa alikuja nchini Januari 6,alitiliwa
mashaka na polisi wa JNIA na tulimuamuru akae pembeni kwa upekuzi
zaidi na kugundua anasafirisha kenge bila Kibali,”alisema Selemani.
Selemani alisema walipoendelea kumuhoji mtuhumiwa
huyo alidai kuwa alikuja nchini kwa ajili ya kuchukua viumbe aina ya
ndege lakini baada ya kuwakosa aliamua kubeba Kenge hao.
Kamanda Selemani aliwaomba wananchi kuwa na
uzalendo wa nchi yao wanapoona mtu anasafirisha rasilimali za nchi watoe
taarifa katika jeshi la polisi.
Alisema polisi wataendelea kuimarisha ulinzi
katika maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege ili kudhibiti aina hiyo
ya utoroshaji wa nyara.
Julai 31, mwaka jana raia wa Vietnam, Dong Van
(47) naye alikamatwa uwanjani hapo akiwa na meno 65 na kucha 447 za
simba zenye thamani ya Sh189.4 milioni.
No comments:
Post a Comment