WAKATI mwingine maisha sio popote. Hali imeanza kuonekana kuwa
ngumu kwa mshambuliaji wa Barcelona, Luis Suarez, katika maisha yake ya
Catalunya kutokana na kufukuzwa kwa watu wawili muhimu kwake
waliompeleka klabuni hapo.
Barcelona imewafukuza Mkurugenzi wa Ufundi, Andoni
Zubizarreta pamoja na msaidizi wake, Carles Puyol na hatua hiyo
imemweka Suarez katika presha kubwa.
Nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay ameanza
kutazamwa kwa jicho baya tangu alipohamishwa kwa dau la Pauni 75 milioni
kutoka Liverpool Julai mwaka jana na bado hajakirejea kiwango chake cha
upachikaji mabao.
Suarez ameifungia Barcelona mabao matatu tu katika
mechi 12 na hatima yake imeanza kuangaliwa kwa karibu na klabu kubwa za
Ligi Kuu England.
Mara kadhaa Barcelona imekuwa ikichukua maamuzi
magumu ya kuwauza mastaa wake katika muda mfupi kama wakishindwa
kuonyesha makali.
Barcelona haina mpango wa kumuuza Suarez, lakini
anaweza kujikuta katika wakati mgumu katika kipindi cha majira ya joto
pindi Barcelona itakapofanya uchaguzi wa kupata viongozi wapya.
Rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu, juzi
Jumatano wakati timu yake ikijiandaa na pambano la jana Alhamisi la
Kombe la Mfalme, alitoboa kuwa ataitisha uchaguzi mkuu wa timu hiyo
mapema kuliko ilivyo kawaida.
Hata hivyo, hata kama utawala mpya wa Barcelona
hautaafiki uwezo wa Suarez, bado haionekani kama Barcelona itakubali
kumpoteza Suarez kutokana na timu hiyo kufungiwa kusajili wachezaji,
hatua iliyochukuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Soka (Fifa)
baada ya kuchemsha katika uhamisho Neymar.
Mpaka sasa Suarez amefunga bao moja tu la Ligi Kuu
Hispania katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Cordoba kwenye mechi ya Desemba
20 mwaka jana, kabla ya kufunga mabao mawili katika mechi mbili za Ligi
ya Mabingwa Ulaya dhidi ya timu za Apoel Nicosia na PSG.
No comments:
Post a Comment