MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amevunja ukimya baada ya
kuzungumzia tuhuma mbalimbali ambazo zimekuwa zikielezwa juu yake,
ikiwamo usaliti ndani ya chama chake na hatima yake ya siasa baada ya
kutimuliwa.
Katika mahojiano haya, zitto anatoa maelezo yote juu ya tuhuma dhidi yake.
Swali: Mwaka 2009, ulitaka kugombea uenyekiti wa Chadema, uamuzi huo
ulikuwa ni wako mwenyewe ama kuna watu nyuma yako walikushawishi kufanya
hivyo?
Jibu: Chadema nilivyoingia kwenye uongozi Makao Makuu, kulikuwa na
wabunge watano, wanne wa kuchaguliwa na mmoja wa viti maalumu.
Nilivyoingia pale nilipewa nafasi ya kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi na wa
Mambo ya Nje kwa ajili ya kujenga mahusiano ya chama chetu na vyama
vingine vya kimataifa, hiyo kazi niliifanya kwa ubora na mpaka sasa
uhusiano wote ya Chadema na vyama vya nje, niliyajenga mimi.
Mwaka 2005 niliandika mkakati wa uchaguzi tukapata majimbo mengi zaidi,
tulipata asilimia nane ya kura hivyo tukapata wabunge sita wa viti
maalumu.
Kabla ya hapo Chadema ilikuwa ikizidiwa hata ya UDP, pamoja na kwamba kilikuwa na wabunge tangu 1995.
Wabunge wake hawakujitanabaisha kama wapambanaji wa misingi ya kitaifa,
tulivyoingia (Bungeni) sisi na kina Ndesamburo (Mbunge wa Moshi mjini,
Philemon Ndesamburo), DK Slaa (Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Willibrod
Slaa), tukaanza kubadilisha hali hiyo.
Tukaanza kupambana na ufisadi, kabla ya hapo Dk. Slaa alikuwa bungeni
kwa miaka 10 lakini hakuwa machachari kama ilivyokuwa kuanzia 2005.
Alivyoingia mwaka 2005 ndipo tukaanza na hoja kama zile za EPA na Buzwagi.
Baada ya hapo mimi na kina Profesa Kitila Mkumbo tukaona kuna haja ya
kubadilisha chama, mwaka 2009 nilivyotaka kugombea uenyekiti nilikuwa na
nia ya dhati kabisa.
Ndani ya Chadema kuna watu wanaamini katika uliberari, kama biashara na taji, hawa ni watu kama kina Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe), sisi tunaamini katika demokrasia ya jamii. Hapa kwenye kundi
hili unatukuta mimi kina Profesa Mkumbo, Profesa Mwesiga Baregu, na
wenginr, tulitaka kukitoa chama kwenyel mrego wa kihafidhina kwenda
kwenye ujamaa.
Hata hivyo wazee walinitaka niache kugombea nikaacha, ni kweli
ukiangalia chanzo cha ugonzi ni mwaka 2009, ila mimi sikudahani kama
kitu kile kingeleta chuki, nilidhani mambo yangeishia pale.
Swali: Nini kilifanya iwe vigumu kumaliza tofauti zako na Chadema?
Jibu: Mara zote nimekuwa nikiwaambia Chadema kwanza waniambie kosa langu
ni nini, Ndesamburo aliwahi kunifuata ili tuyamalize, Wenje naye
alinifuata na siku kutaka tuyamalize, lakini upande mwingine viongozi
nao wanasema yao kwa hiyo ni undumilakuwili tu kila mahali.
Swali: Kuna baadhi ya watu wanaamini kuwa wewe na Mbowe mna ugomvi
binafsi, tofauti na vile ambavyo watu wanadhani kuwa mnagombea uongozi.
Wengine wanasema uliwahi kutoa siri zake, juu ya kuwa na nyumba Dubai,
madai haya yana ukweli?
Jibu: Kama Mbowe ana mali nje mimi kwa kweli sijui, mimi nilitoa hoja
ikaundwa kamati ya uchunguzi, kama ilimkuta ana mali nje sijui.
Hata hivyo kama ana nyumba, ama mali nyingine ni kwa nini auogope?
Kama una nyumba Marekani, Afrika Kusini, Dubai ama wapi hiyo siyo tabu,
ilimradi kwenye tamko la maadili (Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma)
uwe umesema kuwa unazo na TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) wajue
umepata wapi hizo fedha.
Swali: Lakini inadaiwa kuwa ulikaa na Mbowe wewe akakueleza kama mtu
wake wa karibu kuwa ana nyumba Dubai na wewe ukatoa hizo habari kwa umma
na ndicho kilichomuudhi.
Jibu: Mimi sijawahi kukaa na Mbowe kuzungumza hayo mambo. Sina ugomvi
binafsi Mwenyekiti wa Chadema, siku zote nimekuwa nikimchukulia kama
kaka, ndiyo maana hata akinishambulia nimekuwa nikijitahidi kukaa kimya.
Mwanzoni kabisa yeye alikuja chuo kikuu kunifuata, mwanzoni mwa mwaka
2001, nikiwa mwanachama wa Chadema lakini siyo kiongozi, yeye akiwa
Mbunge wa Hai, alikuja akaniambia naomba tuzungumze utusaidie kwenye
chama.
Alikuwa anataka kufanya mabadiliko ya katiba ya chama, nikatumia nafasi
yangu ya uanaharakati wa wanafunzi na uwezo wangu wa uchambuzi tukafanya
hivyo tulivyofanya.
Tukabadilisha chama mimi na yeye, mabadiliko makubwa ambayo yanaonekana
hivi sasa Chadema ni kazi ambayo tulifanya mimi na yeye, hata gumboe
mwaka 2009 niliona ni jambo la kawaida. Kilichopo ni mitizamo tofauti ya
namna ya kuendesha siasa, na tofauti hizo zimesababisha yatokee
yaliyotokea.
Wakati mwingine nikikaa peke yangu huwa yangu na kujiuliza, huwa sioni
msingi wa ugomvi wangu na chadeama, naona ni ugomvi tu wa madaraka na
juhudi za watu kutaka kuondoa wengine katika ulingo.
Katika mazingira kama hayo ni rahisi kutoa tafsiri kwamba kuna ugomvi binafsi.
Yeye (Mbowe) alikuja hapa Kigoma akafanya mkutano wa hadhara
akanitukana, akasema alinisaidia sijui gari, sijui nini, yaani alikuja
nyumbani kwetu kunisimanga.
Nikasema huyu mtu ananisimanga, kwanza ni mambo ya kishamba, kwamba
unamsaidia mtu halafu unakuja kumsema, kwanza kuna vitu ambavyo mimi
mwenyewe nimemsaidia labda kifedha ama siyo fedha, na tunajua kati ya
mimi na yeye.
Siyo vitu naweza kuibuka nikasema nilimdharau sana kwa kweli, na juzi
nimemsikia huko Shinyanga akisema kuwa hawezi kukaa na kuongea na mimi
kwamba ni msaliti na mambo kama hayo. Huu ni undumilakuwili kwa kweli
kwa sababu huku anatuma watu kwamba kina Ndesamburo (Philemon
Ndesamburo), kwamba tuongee tuone namna ya kuyamaliza haya mambo alafu
yeye huku nyuma akikaa anaongea yake.
Kwa hiyo binafsi naamini sina ugomvi naye sanasana ni tofauti za
kiitikadi. Mimi na yeye tumekaa Bungeni miaka 10, naomba tu watu
watupime.
Katika miaka yangu 10 ni hoja gani nimezisimamia na yeye ni zipi amezisimamia.
Mimi siku zote siasa zangu ni hoja na issue za kusaidia wananchi na nafurahi ninavyosimamia vitu na kuona vikienda.
Swali: Mara kadhaa viongozi wa chama chako wamekuwa wakikutuhumu kwa
kusaliti chama, na kwamba kwa upande mmoja unatumiwa na CCM na upande
mwingime usalama wa taifa, ni kwa nini ushutumiwe kwa tuhuma kama hizo?
Jibu: Kwenye siasa ukitaka mwanasiasa amalizike ni kumpa hizo tuhuma.
Lakini waulize (Chadema), ni taarifa zipi zinapelekwa kwenye usalama wa
taifa, watu haohao walisema siendi kwenye vikao vya chama, wala ofisini,
sasa hizo taarifa ninazozipeleka ni zipi wakati kwenye vikao wala
ofisini siendi? Mtu anayepeleka taarifa ni yule asiyekosa kwenye vikao.
Anahudhuria kila kikao ili apate taarifa za kupeleka.
Lakini pia angalia, mwaka 2010 nilitoa taarifa ya kumuomboa Waziri
Mkuu, hoja ile ikaungwa mkono kwa kusainiwa na wabunge wa pande zote,
hivyo ikasaidia kuondoa baadhi ya mawaziri waliokuwa na shutuma.
Mwaka 2013 kulikuwa na Operesheni Tokomeza. Ripoti ya Kamati ya Bunge
iliyokuwa imewasilishwa ilikuwa inamtaja waziri mmoja tu, lakini
nilisimama na kujenga hoja mawaziri wengi tu wakaondolewa.
Mwaka 2014 nimepeleka hoja ya Escrow na nikaisimamia, mawaziri
wameondoka, serikali imetikisika, sasa mtu anayetumika na Chama Cha
Mapinduzi kwa nini aiangushe serikali ya chama hicho mara tatu ndani
miaka mitano? Mtu ambaye anatumika inawezekanaje alete mjadala
utakaoingusha serikali?
Ndiyo maana sipotezi muda kujibizana na propaganda za aina hiyo, watuambie ni taarifa gani zilipelekwa huko zikawaathiri?
Swali: Baada ya Mahakama kutoa uamuzi wake na Mwansheria Mkuu wa
Chadema, Tundu Lisu kutangaza kuwa umefukuzwa uanachama kwa kuwa
kukishitaki chama ni kujifukuza katika chama moja kwa moja, tangu ukiwa
kiongozi wa chama uliwahi kukitilia shaka kifungu hicho kwa kuwa hivi
sasa umeonekana kukilalamikia.
Jibu: Hiki kifungu kipo kwenye kanuni na wala siyo Katiba, kilitungwa
mwaka 2013. Mwaka huo kuna mabadiliko fulani fulani yalifanywa.
Mabadiliko yale yalikuwa na malengo fulanifulani ikiwamo kulenga watu
fulanifulani.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri, mamlaka ya kutoa haki iko kwenye chombo
kimoja tu nacho ni Mahakama, kila raia ana haki ya kwenda mahakamani
kudai haki, unaposema mwananchama wa Chadema akienda mahakamni amejivua
uanachama ina maana wewe huitambui Katiba ya Jamuhuri.
Hii ina maana kama mwanachama amekipangisha chama, na chama kikashindwa
kulipa kodi, yule mwanachama akienda mahakamani amejivua mwenyewe
uanachama kwa kuwa haruhusiwi kwenda mahakamani.
Hicho ni kipengele ambacho hakikupaswa kuwap, Wanachama wa Chadema
waende mahakamani kushtaki kipengele hicho ili kitangazwe kuwa siyo
halali.
Chama kinachopambana kushika dola hakipaswi kuwa na vipengele kama hivi.
Ila yote kwa yote hiki kipengele kimewekwa mwaka 2013 na mwaka 2015
kikatumika kwangu, ni wazi kilitungwa kwa ajili yangu.
Swali: Baada ya kufukuzwa Chadema, ni nini hatma yako kisiasa?
Jibu: Nina ziara ya kuzunguka na wananchi wa jimbo langu kuangalia jinsi
ya kuwatumikia, leo (jana) nawaaga rasmi kwamba sintakuwa nao baada ya
uchaguzi mkuu wa mwaka huu, lakini ni nini kinachokuja baadaye ya hapo
tutakijua vizuri wiki ijayo (wiki hii).
Hatujajua kama Chadema wameandika barua kwa Spika ili kunitangaza kuwa
jimbo liko wazi, kama ndivyo tutakaa kujua ni nini cha kufanya.
Ilipaswa baada ya kesi kwisha taratibu zifuatwe, mpaka sasa sijapata
taarifa zozote za kufukuzwa ndiyo maana nasema mpaka wiki kesho iishe
tutajua, nitakuwa na nia ya kuendelea kutumikia kwenye jimbo lolote
Oktoba.
Swali: Una mpango wa kujiunga na ACT?
Jibu: Tusijaribu kuvuka mto kabla hatujafika pa kuvukia.
Swali: Vipi hukumu ya Mahakama Kuu juu ya kesi yako na Chadema?
Jibu: Kwenye kazi yangu kuna miguu ya watu wengi naikanyaga, taarifa
yangu ya Escrow nimewakanyaga mpaka mahakama. Kwa hiyo yawezekana kabisa
mahakama iliona hapa ndipo kwa kunikanyaga, ama yawezekana kabisa ni
taratibu.
Inaonekana kuna uhusiano wa karibu wa mahakama na wanasheria wa Chadema,
sisi tulisikia kwenye vyombo vya habari kwamba hukumu ya kesi yetu
imetolewa.
Hata baada ya hukumu hiyo, tulijaribu kufuatilia ili kupata hukumu,
kwa siku mbili tulizungushwa, siku ya tatu tukaambiwa kuwa jalada lipo
kwa jaji kiongozi.
Lakini mimi bado nina imani kwamba wakuu wa mahakama watachunguza jambo hili na kuona kama kuna cha kufanya.
Sisi tulipaswa kuitwa mahakamani, lakini hatukuitwa, kuna taratibu za
mahakama hazikufuatwa, tuna imani kuwa viongozi wa mahakama watachunguza
kama kuna suala la rushwa katikati hapa ama kuna nini.
Lakini pia hali hii imenifanya niwe na kiu zaidi ya kuhakikisha nikipata
tena nafasi nitafanya operesheni kwenye mfumo wa mahakama kwa kuwa
umekuwa na malalamiko sana ya kuwaumiza wananchi.