Wednesday 2 March 2016

Tanzania na Kenya kuimarisha ushirikiano

Rais Uhuru na Magufuli katika ikulu ya rais nchini Tanzania
Kenya na Tanzania zimekubaliana kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu na kukuza biashara.
Katika mazungumzo ya viongozi wa nchi hizo mbili, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameeleza kufurahishwa kuona Rais John Magufuli wa Tanzania yupo tayari kuhakikisha nchi hizo zinakuwa karibu na miradi ya maendeleo inaharakishwa.
Mradi mwingine wa maendeleo walio ujadili ni kuzalisha ajira kupitia viwanda.

'' Kwa sababu nia yetu sisi ni kuona maendeleo yatakayogusa wananchi wa kawaida, tumalize umasikini, uchumi ukue, na hivyo hatuwezi kufanya tukiwa tumetengana'' alisema Kenyatta.
Kwa upande wake Rais Magufuli amesema Tanzania na Kenya zina kila sababu za kuimarisha mahusiano ya kibiashara hasa katika ujenzi wa viwanda, utakaozalisha ajira kwa kuwa watu wake ni wamoja.
''Wazee wetu mzee Kenyatta na mzee Nyerere walijenga mazingira mazuri ya kuwa na nchi hizi mbili, wakati wakipigania uhuru, sasa sisi vijana wetu ni wakati wetu kwenda mbele kwa ajili ya maendeleo'' alisema Rais Magufuli.
Rais Magifuli ameutaja mradi moja wapo kuwa ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Tanzania kwenda Kenya kupitia Namanga.

No comments: