Tuesday, 29 March 2016

Tanzania yasikitika kunyimwa pesa za MCC

Tanzania imehuzunishwa na hatua ya bodi ya shirika la changamoto za milenia (MCC) kusitisha msaada
wake wa awamu ya pili wa dola milioni 472.8 ambazo ni sawa na shilingi trilioni moja pesa za Tanzania.
Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Bw Augustine Mahiga ameelezea kushtushwa kwake na hatua hiyo ya bodi ya MCC akisema "imepuuza hatua kubwa tu zilizopigwa kidemokrasia" nchini humo.
''Inasikitisha kuwa demokrasia yetu inatathminiwa tu na matokeo ya uchaguzi wa visiwani Zanzibar,''
Waziri wa mambo ya nje bwana Augustine Mahiga
Kuhusiana na uchaguzi wa Zanzibar Bw Mahiga anasema kuwa Tanzania, ilifanya kila kitu kuambatana na sheria na katiba ya nchi wala hakuna tatizo ama ukiukwaji wa sheria.
Mahiga anasema kuwa huo ni uamuzi wao na kwa sababu hela hizo ni zao wanauhuru wa kuzitumia watakavyo ila anahoji kwanini uamuzi huo uliafikia bila ya majadiliano na serikali ya muungano ya Tanzania.

Bw Mahiga amesisitiza kuwa Tanzania ilifwata katiba yake kuhusiana na uchaguzi wa Zanzibar
Kuhususiana na kupitishwa kwa sheria ya uhalifu wa mitandao bwana Mahiga anasema sheria hiyo ilikuwa inalenga kupambana dhidi ya ugaidi.
Waziri huyo ameonya kuwa watu wanaoishi vijijini ndio watakaoathirika zaidi kwani fedha hizo zilikuwa zimepangiwa kueneza umeme mashinani.
Katika kutoa uamuzi wake, Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) ilisema kuwa Tanzania haijatimiza viwango vinavyohitajika ili kunufaika na ufadhili kutoka kwa shirika hilo, na hivyo basi haitapokea msaada wa awamu ya pili.
Bodi hiyo aidha imesema Tanzania iliendelea na uchaguzi wa marudio Zanzibar ambao "haukushirikisha wote na wala haukuakisi maoni ya wote
Kupitia taarifa, bodi hiyo ilisema kuwa: "Serikali ya Tanzania haijachukua hatua za kuhakikisha kuheshimiwa kwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa kujumuika katika utekelezwaji wa sheria ya Uhalifu wa Mtandao.”
Bodi hiyo aidha imesema Tanzania iliendelea na uchaguzi wa marudio Zanzibar ambao "haukushirikisha wote na wala haukuakisi maoni ya wote, licha ya malalamiko kutoka kwa serikali ya Marekani na jamii ya kimataifa.”

No comments: