Thursday 3 March 2016

Magufuli na Kenyatta wazindua barabara Arusha

EACRais Kenyatta aliwasili Tanzania jana kwa mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Rais wa Tanzania John Magufuli na mwenzake wa Kenya Uhuru Kenyatta wanaweka jiwe la msingi katika barabara itakayounganisha mji wa Arusha nchini Tanzania na mji wa Voi nchini Kenya.
Barabara hiyo kutoka Arusha hadi Taveta inatarajiwa kurahisisha uchukuzi na kuimarisha biashara kati ya mataifa hayo mawili.
Ina umbali wa kilomita 234 na ni sehemu ya mradi mkubwa wa barabara inayotoka Arusha na kupitia Holili na Taveta hadi Mwatate. Jiwe la msingi limewekwa na marais hao wawili eneo la Tengeru, Arusha.
Mwaka uliopita Rais Kenyatta na Rais wa Tanzania wakati huo Jakaya Kikwete walizindua mradi wa ujenzi wa barabara hiyo ya Taveta-Mwatate/Voi iliyo upande wa Kenya.

Mradi wa ujenzi wa barabara hizo mbili umefadhiliwa kwa pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika na serikali za Kenya na Tanzania.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa kanda hii wa AfDB Gabriel Negatu benki hiyo imetoa $218 milioni za kutumiwa kwenye mradi huo, Kenya ikipokea $116 milioni na Tanzania $102 milioni.
Huo ndio mradi wa pili wa barabara wa kuunganisha Kenya na Tanzania uliofadhiliwa na benki hiyo, wa kwanza ukiwa barabara za Arusha-Namanga/Namanga-Athi River.

No comments: