Sunday 13 March 2016

Wafanyakazi Waliofukuzwa NIDA Wagoma Kupokea Barua Za Kuachishwa Kazi


Baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) waliofutiwa mikataba ya kazi, wamegoma kupokea barua za kuachishwa kazi wakidai kwamba hawajui kilichoandikwa kuhusu hatima ya madai yao Wafanyakazi hao walikutana jana Dar es Salaam na kiongozi wao, Seif Kibangu alisema wamekubaliana kutochukua barua hizo hadi pale watakapopata ushauri kutoka kwa wanasheria.

“Licha ya mishahara ya miezi mitatu tuna madai yetu mengine ikiwamo makato ya mafao yetu yaliyotakiwa kupelekwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, pia tumekuwa tukikatwa bima ya afya asilimia tatu ya mishahara yetu hatujui hatma yake.

"Sasa leo wanataka tuchukue barua hizo tena kwa kusaini kabla ya kujua kilichoandikwa hapana tuendelee kuvumilia haki yetu tutaipata,” alisema Kibangu.
Aliwakosoa waliochukua barua hizo akisema waliajiriwa kwa makundi, ingawa pia wapo waliopewa kazi hiyo kwa vimemo.

“Hili ni jasho letu, hatuibi cha mtu kwa hiyo tunastahili kupata haki zetu zote, mishahara tunayodai kwa miezi mitatu, acha hayo madai mengine... Tunadaiwa huko tunapoishi kwa kweli tunaomba wahusika waingilie kati jambo hili linatuumiza na kuyumbisha maisha yetu,” alisema.

 Akizungumza kwa niaba ya madereva wenzake, George Mmari alidai kuna gharama nyingi walizoingia ambazo Nida inapaswa kuzilipa ikiwamo malipo ya kuegesha na kuosha magari waliyokuwa wakiendesha.

Akizungumzia madai hayo, Ofisa Habari Mwandamizi wa Nida, Rose Mdami alieleza kushangazwa na hatua ya wafanyakazi hao kugoma kuchukua barua zao badala ya kuzipokea ili wajue kilichoandikwa ili kama wana madai waandike barua na kuyaorodhesha.

No comments: