Saturday 16 April 2016

Yanga kuipiga mtibwa na kurejea kilelen ?


Yanga vs Mtibwa -znz 1

MECHI Tatu za ligi kuu Tanzania bara zinataraji kuchezwa Jumamosi na siku ya Jumapili. Mabingwa watetezi Yanga SC walio nafasi ya pili ya msimamo wakiwa na alama 56 watawakaribia Mtibwa Sugar ya Turiani, Morogoro iliyo nafasi ya nne na pointi 43.
Mchezo huu utapigwa katika uwanja wa taifa siku ya leo Jumamosi. Mchezo mwingine siku ya leo utawakutanisha Coastal Union ya Tanga iliyo mkiani mwa msimamo na alama 19 baada ya kucheza michezo 26.
Coastal watakuwa nyumbani ( Mkwakwani) kuwakaribisha JKT Ruvu ya Pwani katika pambano kali kuepuka vita ya kuteremka daraja. Kikosi cha JKT Ruvu chini ya kocha mzoefu, Abdallah ‘King’ Kibadeni kipo nafasi ya 13 kikiwa na alama 24 katika michezo 24 waliyo kwishacheza.
Siku ya Jumapili, viongozi wa ligi hiyo, timu ya Simba SC watawakaribisha Toto Africans ya Mwanza katika pambano lingine linalokutanisha timu zenye malengo tofauti. Simba ina pointi 57 baada ya kucheza michezo 24, wakati Toto iliyo nafasi ya 11 ina pointi 27.
YANGA V MTIBWA
Haitakuwa rahisi kwa Mtibwa kupata walau pointi moja mbele ya Yanga katika mchezo huu. Yanga itakuwa na nafasi ya kuishinda Mtibwa Sugar katika game zote mbili za msimu kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2008/09.
Mtibwa ilijijengea tabia ya kutopoteza mchezo katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro tangu mwaka 2009. Lakini msimu huu walipoteza kwa kuchapwa 2-0 (Magoli ya Donald Ngoma na Malimi Busungu,) na wata cheza uwanja wa Taifa wakiwa na rekodi ya kupoteza michezo minne iliyopita ya VPL.
Yanga wanashindania taji na ushindi dhidi ya Mtibwa yenye uhakika wa kubaki top 5 na nafasi finyu ya kumaliza top3 utawafanya vijana wa Mkufunzi, Hans Van der Pluijm kurejea kileleni mwa msimamo baada ya kuenguliwa takribani mwezi mmoja uliopita na mahasimu wao Simba.
Yanga wamecheza michezo 23, baada ya mchezo wa Jumamosi hii watabakiwa na michezo minne tu kabla ya kumalizika kwa msimu. Baada ya timu yake kuishinda Mwadui FC wiki mbili zilizopita kocha wa Mtibwa, Mecky Mexime alisema kwamba ‘wanacheza ligi ili kupata kipato tu cha kuendeshea maisha yao kwa kuwa ligi inachezeshwa katika utaratibu mbaya kwa baadhi ya timu.
Mtibwa haitakuja kushindana na Yanga bali itakuja kukamilisha ratiba na kucheza mchezo wao. Mecky tayari alishasema hilo wiki kadhaa zilizopita na mtazamo wake huo ndiyo unanifanya niamini Yanga watashinda na kurejea kileleni kwa kuwa wao wanashindania ubingwa na itawabidi wapambane hadi siku ya mwisho ya msimu kutimiza malengo yao.  Yanga kuifunga Mtibwa mara mbili mfululizo itakuwa ni rekodi mpya na ngazi yao nzuri kuelekea juu ya msimamo.
COASTAL V JKT RUVU
Kikosi cha King kinakwenda Tanga kikiwa na rekodi ya kutoshuka daraja tangu walipopanda mwaka 2002. Ushindi utawafanya JKT Ruvu kupanda hadi nafasi ya 11 na kuwapeleka Toto Africans nafasi ya 12 (timu zote zitakuwa na alama sawa 27 ikiwa JKT Ruvu itashinda dhidi ya Coastal.)
Kupoteza mchezo huu kwa Coastal itakuwa ni sawa na kuanza safari yao katika ligi daraja la kwanza msimu ujao. Pointi 19 walizonazo na 12 wanazoposwa kuzikusanya katika game zao nne za mwisho itawafanya vijana wa kocha Ally Jangalu kufikisha alama 31-pointi ambazo hata kihesabu zinawanyima nafasi ya kucheza VPL msimu ujao.
Stand Unite tayari wana alama 34, Majimaji FC wana pointi 33, wakati timu za Ndanda SC na Mbeya City FC zenyewe tayari zimekusanya pointi 30 kila timu. Toto, Kagera Sugar, JKT Ruvu, JKT Mgambo, na African Sports ndiyo timu pekee zisizofikisha alama 30 hadi sasa.
Coastal tayari wamechelewa lakini wanaweza kujaribu kushinda game zao zote nne zilizobaki ili kusubiri atma yao mwisho wa msimu. Sare au matokeo ya kupoteza mchezo dhidi ya JKT Ruvu yatawashusha daraja japo haitakuwa rasmi.
SIMBA V TOTO
Mechi ya kwanza baina ya timu hizi ilimalizika kwa matokeo ya sare ya kufungana goli 1-1 katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. Simba wanafahamu jinsi timu hiyo ya Mwanza inavyowasumbua kila wanapokutana, na ili kuendelea kugombea ubingwa kikosi cha Jackson Mayanja kinapaswa kushinda game hii siku ya Jumapili katika uwanja wa Taifa.
Toto inayoundwa na wachezaji wengi vijana waliopata kufanya vizuri katika timu ya Simba B itakuwa ikicheza mchezo wake wa 27 wa ligi, pia itacheza na Yanga wiki chache zijazo.
Kushindwa kupata walau alama moja dhidi ya Simba watakuwa wamejipeleka katika ‘shimo’ hivyo watalazimika kupambana kwa kuamini pointi moja katika kila mchezo ulio mbele yao ina faida kubwa kama hawatapata ushindi. Hii itakuwa mechi nyingine kali wikendi hii.

No comments: