Mchungaji Ambilikile Mwasapile maarufu Babu wa Loliondo akitoa huduma ya kikombe kwa wagonjwa |
NGORONGORO . Mchungaji Ambilikile Mwasapile maarufu Babu wa
Loliondo aliyehudumia maelfu ya watu ndani na nje ya nchi kwa dawa aliyoitoa
kwa kipimo cha kikombe amedai ameoteshwa kuwa umati utarudi kijijini Samunge
kupata dawa.
Amesema ana uhakika wa jambo hilo kwa kuwa hata mwaka 2011
kabla ya maelfu ya watu kufika nyumbani kwake alioteshwa, hivyo amejiandaa
kuweka miundombinu bora zaidi na hasa ujenzi wa vibanda atakavyovitumia kutoa
huduma.
Mchungaji Mwasapile alisema hayo jana Jumapili Desemba
10,2017 mbele ya ujumbe wa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Joseph Kakunda
aliyekuwa mkoani Arusha kukagua miradi ya maendeleo, ikiwemo ya kuwawezesha
wananchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Miongoni mwa waliofika kupata ‘kikombe’ kwa gharama ya Sh500
mwaka 2011 walikuwemo wafanyabiashara maarufu, wanasiasa na viongozi waandamizi
serikalini.
Akizungumzia dawa yake anayodai inatibu maradhi mengi
amesema kwa sasa anaitoa kwa watu wachache wanaofika kijijini hapo.
Miongoni mwao amesema ni watalii wanaofika kutembelea
vivutio vya kitalii vilivyopo katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
"Huwa nawauliza watalii namna walivyoifahamu dawa yangu
wanasema habari za ‘kikombe cha Babu’ imeenea katika nchi zao za Ulaya na
Amerika," amesema Mwasapile.
Naibu Waziri wa Tamisemi, Kakunda akiwa na ujumbe wake baada
ya kupata kikombe alimshukuru Mchungaji Mwasapile kwa alivyolifanya Taifa
kujulikana na kusababisha maendeleo ya kijamii katika Kijiji cha Samunge.
Ametoa mfano wa barabara ya kutoka wilayani Longido na
Kigongoni wilayani Monduli ambazo zimeboreshwa kutokana na idadi kubwa ya watu
waliokuwa wakifika kupata huduma ya dawa.
Amesema hata huduma ya mitandao ya mawasiliano ya simu
ilifika eneo hilo kwa haraka kutoka na watu wengi waliohitaji kuwasiliana na
ndugu zao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro,
Raphael Siumbu amesema Mwasapile amechangia shughuli za maendeleo kutokana na
idadi kubwa ya waliokwenda kijijini hapo na kusababisha mzunguko wa fedha kuwa
mkubwa.
Amesema watu wengi kijijini Samunge wamepanda miti inayotumika kutengenezea dawa
hivyo kuchangia utunzaji wa mazingira na huduma za kijamii kuongezeka.
No comments:
Post a Comment