Wakazi wawili wa Dar es Salaam wamekamatwa eneo la Kilambo
mkoani Mtwara lililopo mpakani na nchi ya Msumbiji wakiwa na pakiti zenye uzito
wa kilo 64 za dawa za kulevya aina ya heroin.
Akizungumza na Mwananchi jana, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya
Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Rogers Sianga alisema watuhumiwa
walikamatwa Desemba 7 wakiwa na dawa hizo zikitokea mkoani Pemba nchini
Msumbiji kuingizwa Tanzania.
Sianga alisema pakiti hizo zilifichwa kwenye gari na kila
moja ilifungwa kwa ujazo wa kilo moja.
Alisema watuhumiwa walipokamatwa walipelekwa kwa Mamlaka ya
Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa ajili ya ukaguzi wa kina.
Sianga alisema utaratibu wa kisheria unafanyika ili
kuwafikisha mahakamani.
Kwa mujibu wa marekebisho ya sheria ya kudhibiti na
kupambana na dawa za kulevya, mtu akikamatwa anasafirisha dawa hizo zaidi ya
gramu 20 hapewi dhamana na adhabu yake ni kifungo cha maisha iwapo atatiwa
hatiani.
Sianga alisema DCEA imewadhibiti wafanyabiashara wa dawa za
kulevya ambao sasa wanaitumia Msumbiji kupitishia mizigo na baadaye kuiingiza
nchini.
Alisema wana taarifa kuwa wafanyabiashara haramu wa dawa za
kulevya wamekimbilia nchi za jirani na wataendelea kuwafuatilia kuhakikisha
haziingii nchini.
Kamishna huyo alisema juzi waliteketeza ekari nne za bangi
eneo la Arumeru Magharibi mkoani Arusha.
Alisema mamlaka inaendelea kuwatafuta watuhumiwa wanaohusika
na mashamba hayo.
Kamishna wa Sheria wa DCEA, Edwin Kakolaki alisema kwa
mujibu wa kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za
Kulevya namba 5 ya mwaka 2015 kama ilivyofanyiwa marekebisho watuhumiwa
hawatapata dhamana.
Alisema iwapo watatiwa hatiani na Mahakama, adhabu ni
kifungo cha maisha na mali zao ikiwemo gari waliokuwa wakilitumia kusafirishia
dawa za kulevya zitataifishwa.
Kakolaki alisema washtakiwa wa bangi na mirungi kwa mujibu
wa kifungu cha 11(1) (b) cha sheria hiyo wakipatikana na hatia adhabu ni
kifungo cha miaka 30 jela na huwa hakuna faini au dhamana.
Februari 10, Rais John Magufuli alianza kuisuka Mamlaka ya
Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kumteua Sianga.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment