Friday, 21 March 2014

Mtikila asema wajumbe wanatishwa

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Mchungaji Christopher Mtikila amedai kwamba kuna vitisho vinavyotolewa vya kuwashughulikia wajumbe wanaopinga Muungano.

Amedai kwamba kumekuwa na uvunjaji wa kanuni na Katiba ya nchi waziwazi unaofanywa na kikundi kidogo cha watu ambao wanatishia wasiowaunga mkono.

Alitoa kauli hiyo jana mchana alipokuwa akiuliza swali katika semina ya Bunge hilo iliyokuwa ikiendeshwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba Kenya, Amos Wako.

Wako ambaye ni Seneta wa Busia Mashariki na aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya, alialikwa katika Bunge la Katiba kutoa uzoefu wa namna nchi hiyo ilivyopita katika mchakato huo.

“Mimi nililonalo halihusu mazungumzo tuliyopata kutoka kwa wenzetu wa Kenya, ni kuhusu Kanuni ya 4, uhuru wa maoni na kujieleza. Waheshimiwa wabunge, ndani ya Bunge hili ni juzi kulikuwa na watoa mada na wachangiaji wazuri. Nimetafakari kwa uzalendo wangu na ukomavu wangu wa kisiasa nikaona tusipojadiliana, tutaharibu matarajio ya wananchi na sitaogopa suala la kuwa tutashughulikiwa kama wenzetu.”

Mchungaji Mtikila alisema kumekuwa na vitisho kwa baadhi ya wajumbe ambavyo vinalenga kuwafunga midomo wajumbe ambao wanawakilisha kundi la Watanzania milioni 45.

Mtikila alisema kumekuwa na vitisho kwa baadhi ya wajumbe wanaopinga Muungano akisema msimamo huo unatoka katika kikundi alichokiita ni cha CCM.

Akifafanua, alisema hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Profesa Mark Mwandosya aliyoitoa juzi ilikuwa nzuri, pia ilijaa vitisho.

Katika mchango wake, Profesa Mwandosya aliwataka wajumbe wa Bunge hilo kuwa makini na watulivu wakati wa kusikiliza hotuba ya Rais leo na kuacha zomeazomea.

Mtikila alidai kwamba Profesa Mwandosya alisema Rais wa nchi ni Amiri Jeshi Mkuu ambaye ana uwezo wa kuamuru chochote kauli ambayo hata hivyo, ilitolewa na mjumbe mwingine, Dk. Zainab Gama ambaye alimtaka Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta kutumia kanuni kuwadhibiti wajumbe wanaokwenda kinyume na kanuni walizojiwekea.

Mtikila alidai kuwa misimamo imewahi kuwadhuru waliosimamia ukweli ambao walishughulikiwa akiwataja Dk. Stephen Ulimboka, Horace Kolimba na Dk. Sengondo Mvungi.

“Hata mimi nilishangilia kwa baadhi ya maeneo kuhusu suala la ujio wa Rais, lakini Mwandosya alitoa mifano ya nchi kadhaa huku akisahau kuwa tumeona kina Tony Blair (aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza), wakipigwa mayai viza, akataka tukumbuke kuwa anayekuja ni amiri jeshi mkuu... hii ni kujenga hofu kwa wabunge,” alisema Mtikila.
Mjumbe huyo alisema aliyeajiriwa na akafanya vizuri anapaswa kushangiliwa lakini aliyekosea ni vyema akakosolewa kwa kuzingatia uhuru wa mtu kwa mujibu wa Kanuni 4 ya Bunge hilo na Ibara ya 100 ya Katiba Kifungu cha 27 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Alijipambanua kuwa amekwenda Dodoma akiwa na msimamo mmoja ambao kila mtu anaufahamu kuwa anapinga Muungano kwa sababu anaitaka Tanganyika.

Akijibu hoja hizo, Sitta alisema katika nchi ya kidemokrasia kama Tanzania ambayo inaongozwa kwa sheria, watu wanashughulikiwa kwa sheria.

Alisema ndani ya Bunge kinachowashughulikia watu ni kanuni, akasema hatarajii kuona watu wakiingia na mayai viza ndani ya Bunge kwa ajili ya kumpiga mtu yeyote.

Alisema kilichoelezwa na Profesa Mwandosya kilikuwa ni umuhimu wa kuwapo staha bungeni na siyo vitisho kwa wajumbe na kwamba kama kuna watu ambao wanaweza kuwa na hasira, kuna njia nyingi za kuzionyesha lakini siyo ndani ya Bunge. Alimtaka Mchungaji Mtikila asiogope na awe na amani.

No comments: