Friday 14 March 2014

Roboti kuongoza magari Dar

Magari yakipita pembeni mwa roboti anayeyaongoza katika moja ya barabara za jiji la Kinshasa, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Tanzania inatarajia kuweka roboti hao ili kupunguza mzigo wa kuongoza kwa askari wa usalama barabarani ambao mmoja huudumia magari yapatayo 1,400 kwa siku

Matumizi ya roboti katika kuongoza magari imeelezwa kwamba inaweza kusaidia kukabiliana na tatizo la foleni za magari Jijini Dar es Salaam.

Mkakati huo umeelezwa kwamba utakuwa mbadala bora zaidi wa taa au askari wa usalama barabarani ambao wamekuwa wakiongoza magari kwenye makutano ya barabara.

Katika maeneo mengi, taa za kuongoza magari zimeshindwa kusaidia kupunguza msongamano huku askari hao wakitupiwa lawama na baadhi ya watumiaji wa barabara kwamba wamekuwa wakipendelea upande mmoja.

Roboti zimeonekana kuwa na sifa ya kipekee kwa uwezo wake wa kuongoza magari bila upendeleo hasa kwa kuhakikisha hakuna upande unaoelemewa na msongamano.

Kwa mujibu wa Mtandao wa Televisheni ya CCN ya Marekani, Jiji la Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) limefanikiwa kutumia roboti kuongoza magari na kupunguza foleni kwa kiwango kikubwa.

Roboti mbili zimefungwa katika jiji hilo na zinafanya kazi hiyo kwa saa 24, huku zikitumia kamera maalumu kurekodi kila tukio na kurahisisha kuwabaini wanaokiuka sheria za usalama barabarani.

Roboti hizo ambazo zimetengenezwa na Wakongo wenyewe, zina urefu wa futi nane na zinafanya kazi kwa saa 24 zikitumia nguvu za jua.

Zina uwezo wa kuinua na kushusha mikono wakati wa kuzuia au kuruhusu magari. Pia zina uwezo wa kuwaeleza waenda kwa miguu wakati mwafaka wa kuvuka barabara.

Mapema mwaka huu, Kenya ilifunga kamera maalumu (CCTV) kwa ajili ya kuongoza magari na kuratibu makosa ya barabarani katika jiji la Nairobi.

Hivi karibuni, Kamanda wa Usalama Barabarani Tanzania, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Mohammed Mpinga alikaririwa akielezea umuhimu wa kufunga kamera hizo kwa lengo la kuimarisha usalama.

Mataifa yenye magari mengi kama China ambayo ina magari milioni 120 yaliyosajiliwa imechukua hatua madhubuti kukabiliana na foleni katika miji yake.

Moja ya mikakati hiyo ni kuimarisha usafiri wa umma na kuweka tozo maalumu kwa wanaoingia na magari binafsi mijini.
Kwa Dar es Salaam, mikakati iliyopo sasa ni ujenzi wa barabara kwa ajili ya mabasi yaendayo kasi ambao umeshaanza kuanzia Kivukoni hadi Kimara, usafiri wa treni kuanzia Ubungo hadi Stesheni na Pugu Mwakanga mpaka Kurasini na ujenzi wa barabara za juu, Ubungo na Tazara ambao hata hivyo, haujaanza.

Wakati huohuo, Manispaa ya Temeke imeeleza mkakati wa kupunguza foleni.

Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Temeke, Joyce Msumba alisema jana kwamba katika mkakati huo, itapanua Barabara za Temeke Sokota-Mtoni kwa Aziz Ali; Kizuiani-Kibada na Mbagala Kilungule-Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Alisema upanuzi wa barabara hizo utakaoanza mwakani, uko katika Mradi wa Maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam unaofadhiliwa na Benki ya Dunia. “Barabara hizo zitakuwa za njia nne ambazo zitakuwa na vituo vikubwa vya daladala na zikikamilika, zitapunguza msongamano wa magari kwa kiasi kikubwa,” alisema.

Msumba alisema baadhi ya nyumba zitabomolewa kupisha ujenzi huo na wakazi wake watalipwa fidia.

Alisema wakati wa upanuzi wa Barabara ya Temeke Sokota- Mtoni kwa Aziz Ali, Kituo cha daladala cha Temeke Mwisho kitavunjwa.

Kituo hicho kilijengwa na manispaa hiyo kwa gharama ya Sh126 milioni na tangu kilipokamilika mwaka 2012, hakijawahi kutumika. Daladala zilizotakiwa kukitumia zinaishia Tandika ambako hakuna kituo maalumu.

DRC

Roboti mbili zimefungwa katika jiji la Kinshasa, DRC na zinafanya kazi hiyo kwa saa 24, huku zikitumia kamera maalumu kurekodi kila tukio na kurahisisha kuwabaini wanaokiuka sheria za usalama barabarani

No comments: