Monday 10 March 2014



Maafisa wa Vietnam wanaoitafuta ndege ya Malaysia iliyopoteza mawasiliano na waongozaji wa safari za ndege kati ya Malaysia na Vietnam Jumamosi iliyopita wanasema wameona kitu kinachoshukiwa kuwa mlango wa ndege hiyo aina ya Boeing 777 ambayo mpaka sasa haijulikani iliko. Meli mbili za polisi wa baharini ziko katika eneo hilo yapata kilometa 60 kusini mwa kisiwa cha Tho Chu katika Ghuba ya Thailand. Maafisa wa Malaysia leo wameanza kupima sampuli za mafuta yaliyoonekana yakielea siku ya Jumamosi katika eneo hilo. Wakati huo huo maswali yameibuka kuhusu vipi abiria wawili walivyoweza kuingia katika ndege hiyo kutumia pasi za kusafiria zilizokuwa zimeibwa. Polisi ya kimataifa, Interpol, imethibitisha kuhusu pasi hizo, lakini ikasema maafisa hawakuangalia orodha yake ya hati zilizoibwa kabla ndege hiyo kuondoka Kuala Lumpur siku ya Jumamosi kuelekea Beijing ikiwa na watu 239. Wizi wa pasi hizo, moja ikimilikiwa na raia wa Austria, Christian Kozel na nyingine ya Luigi Maraldi wa Italia, uliripotiwa kwa Interpol baada ya kutokea nchini Thailand mwaka 2012.

No comments: