CHELSEA ndiyo timu pekee ya Uingereza iliyojihakikishia nafasi ya kushiriki mechi za robo fainali za Ligi ya Mabingwa barani Ulaya baada ya kuinyamazisha Galatarasay ya Uturuki kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.
Kwa mujibu wa BBC, matokeo hayo yanaipa Chelsea ushindi wa jumla ya mabao 3-1.
Hatua ya kocha Jose Mourinho kumpumzisha mshambulizi wake, Fernando Torres, na badala yake kumchezesha nyota wa Cameroon, Samuel Eto'o, ilizaa matunda punde baada ya kipenga cha kwanza.
Etoo ambaye majuzi alikejeliwa kutokana na umri wake mkubwa alimnyamazisha Mourinho kwa kufunga bao la kwanza kunako dakika ya nne na kufufua matumaini ya mashabiki wa Chelsea na hasa Uingereza.
Wawakilishi wengine wa Uingereza Manchester city na Arsenal tayari wameondolewa kwenye mashindano hayo, hivyo matumaini ya Waingereza yamebaki kwa Chelsea.
Vijana wa Stanford Bridge hawakuzembea, kwani waliendeleza gongagonga hadi dakika tatu kabla ya kipenga cha mwisho kipindi cha kwanza wakati mkwaju wa John Terry ulipotemwa na kipa wa Galatasaray, Fernando Musiera na kisha Garry Cahili akacheka na wavu na Kuihakikishia Chelsea fursa ya kusonga mbele.
Katika mechi ya awali iliyochezwa nchini Uturuki, timu hizo zilimaliza mchezo kwa matokea 1-1.
Mshambulizi wa Galatasaray, Didier Drogba, alishindwa kung'ara Stamford Bridge na badala yake kushuhudia timu yake ya zamani ikifuzu robo fainali Ligi ya Mabingwa.
Chelsea wanaungana na vinara wa ligi kuu Hispania, Real Madrid, ambao wamefuzu robo fainali baada ya jana kuichapa Shalke 04 ya Ujerumani kwa mabao 3-1.
Real wamepata ushindi wa jumla ya mabao 9-2 baada ya mchezo huo wa marudiano uliochezwa Uwanja wa Bernabeu.
No comments:
Post a Comment