Sunday 30 March 2014

SNURA napunguza mauno

MWANADADA anayetamba katika tasnia ya muziki wa mduara pia katika uigizaji wa filamu, Snura Mushi ‘Snura’ amesema ameamua kupunguza kukatika viuno katika video za nyimbo zake kutokana na kukosolewa na hata kutolewa kwenye baadhi ya vipengele vya tuzo za Kilimanjaro Music Awards (KTMA).

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Snura alisema hata kabla Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) hawajapiga stop ushiriki wa nyimbo zake kwenye kinyang’anyiro hicho, alikuwa ameshabadilika kwa kuwa tayari video yake ya ‘Nimevurugwa’ ilikuwa imefungiwa.

Alisema yeye ameshabadilika kabla hata hatujafika huko kwenye Kili kwa sababu ‘Nimevurugwa’ ilifungiwa muda kidogo kabla ya Kili kuikosoa na kwamba wimbo wake wa ‘Ushaharibu’ alikuwa ameshafanya video ikitoka watu watajua ni jinsi gani ameweza kubadilika.

Ameeleza kuwa si kwamba kwenye ‘Ushaharibu’ hakutakuwa tena na uchezaji ule wa kukata viuno bali atapunguza kidogo, akitofautisha na video nyingine zilizotangulia.

“Kweli kwenye video si kwamba hakuna kabisa kiuno ila nimepunguza, nimeacha viuno ambavyo nina uhakika kwamba siwezi kufungiwa jamani, sijakatika kama kwenye ‘Nimevurugwa’, wakati nafanya wimbo wa ‘Nimevurugwa’ sikuhisi kama ninaweza nikafungiwa kiukweli, laiti kama ningejua nisingeweza kufanya vile, mimi nilichukulia kama ni ubunifu na utundu wangu ndiyo maana nikafanya vile,” alisema Snura.

Hata hivyo, amedai kuwa kuna mashabiki wake ambao wangependa kuona anacheza kama alivyokuwa akicheza zamani, hivyo ataendeleza mchezo huo kwenye shoo zake atazofanya kwenye kumbi mbalimbali.

No comments: