Friday 21 March 2014

UCB yatoa mkopo wa bilion 9.2

BENKI ya Uchumi (UCB) inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, imefanikiwa kutoa mikopo ya zaidi ya shilingi bilioni 9.2 kwa kipindi cha miaka nane, lengo likiwa ni kuwawezesha wateja wake kuendesha miradi mbalimbali ya maendeleo na kujikwamua kiuchumi.
Hayo yalibainishwa jana na Meneja mkuu wa Benki hiyo Bi. Angela Moshi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mafanikio mbalimbali waliyoyapata toka kuanzishwa kwa benki hiyo mwaka 2005.
Bi.Moshi alisema benki hiyo imeendelea kukua kwa kasi na hadi kufikia Desemba 31 mwaka jana, rasilimali zake zilifikia bilioni 17, Amana sh. bilioni 13, Hisa sh. bilioni 2.5 na mikopo iliyotolewa ikifikia sh.bilioni 9.2.
"Benki yetu ya uchumi imeendelea kukua kwa kasi na tangu kuanzishwa kwake mwaka 2005 hadi Desemba 2013 tumeshafanikiwa kutoa mikopo ya sh.bilioni 9.2 na katika kipindi cha mwaka jana 2013, benki hii ilipata faida ya sh. milioni 603 baada ya kulipa kodi ya serikali ya sh.milioni 150," alisema Bi.Moshi.
Meneja huyo akizungumzia huduma zinazotolewa na benki hiyo alisema kwa sasa zimefikia huduma 13, na moja ya huduma hizo ni utoaji huduma kupitia simu ya mkononi (UCB Mobile).
Alisema UCB Mobile inaenda sambamba na nia na shabaha ya kuanzishwa kwa benki hiyo ambayo ni kuwafikia wananchi wengi hususan wale wa kipato cha chini na waishio maeneo ya vijijini ikiwa ni pamoja na kuwapatia huduma za kifedha kwa gharama nafuu.
Alisema huduma ya UCB Mobile inafaida nyingi kwa wateja ikiwa ni pamoja na kupunguza msongamano ndani ya benki,kuwezesha wateja kuweka, kurejesha mikopo na kutoa fedha kwa haraka zaidi bila usumbufu.
"Huduma hii ya UCB Mobile ni ya uhakika na inafaida nyingi, kwani mteja wetu anaweza kupata huduma za kibenki akiwa mahali popote, anaweza kulipia huduma mbalimbali ikiwemo ada za shule, ada ya mtihani na huduma nyingine nyingi," alisema.
Meneja huyo alitumia nafasi hiyo kuwataka wateja wa benki hiyo kujiunga na UCB Mobile na kwa wananchi ambao hawana akaunti kujitokeza kufungua akaunti katika benki hiyo, ili kuweza kunufaika na huduma mbalimbali zitolewazo na benki hiyo.
Akizungumza mwenyekiti wa Bodi ya UCB Wilson Ndesanjo, alisema tangu kuanzishwa kwa benki hiyo imeweza kuwapa wanahisa wake gawio lililotokana na faida mara nne, hivyo kutoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro na mikoa mingine,kununua hisa za benki hiyo kama njia ya uwekezaji wa uhakika

No comments: