MECHI Tatu za ligi kuu Tanzania bara zinataraji kuchezwa Jumamosi na
siku ya Jumapili. Mabingwa watetezi Yanga SC walio nafasi ya pili ya
msimamo wakiwa na alama 56 watawakaribia Mtibwa Sugar ya Turiani,
Morogoro iliyo nafasi ya nne na pointi 43.
Mchezo huu utapigwa katika uwanja wa taifa siku ya leo Jumamosi.
Mchezo mwingine siku ya leo utawakutanisha Coastal Union ya Tanga iliyo
mkiani mwa msimamo na alama 19 baada ya kucheza michezo 26.
Coastal watakuwa nyumbani ( Mkwakwani) kuwakaribisha JKT Ruvu ya
Pwani katika pambano kali kuepuka vita ya kuteremka daraja. Kikosi cha
JKT Ruvu chini ya kocha mzoefu, Abdallah ‘King’ Kibadeni kipo nafasi ya
13 kikiwa na alama 24 katika michezo 24 waliyo kwishacheza.
Siku ya Jumapili, viongozi wa ligi hiyo, timu ya Simba SC
watawakaribisha Toto Africans ya Mwanza katika pambano lingine
linalokutanisha timu zenye malengo tofauti. Simba ina pointi 57 baada ya
kucheza michezo 24, wakati Toto iliyo nafasi ya 11 ina pointi 27.
YANGA V MTIBWA
Haitakuwa rahisi kwa Mtibwa kupata walau pointi moja mbele ya Yanga
katika mchezo huu. Yanga itakuwa na nafasi ya kuishinda Mtibwa Sugar
katika game zote mbili za msimu kwa mara ya kwanza tangu msimu wa
2008/09.
Mtibwa ilijijengea tabia ya kutopoteza mchezo katika uwanja wa
Jamhuri, Morogoro tangu mwaka 2009. Lakini msimu huu walipoteza kwa
kuchapwa 2-0 (Magoli ya Donald Ngoma na Malimi Busungu,) na wata cheza
uwanja wa Taifa wakiwa na rekodi ya kupoteza michezo minne iliyopita ya
VPL.
Yanga wanashindania taji na ushindi dhidi ya Mtibwa yenye uhakika wa
kubaki top 5 na nafasi finyu ya kumaliza top3 utawafanya vijana wa
Mkufunzi, Hans Van der Pluijm kurejea kileleni mwa msimamo baada ya
kuenguliwa takribani mwezi mmoja uliopita na mahasimu wao Simba.
Yanga wamecheza michezo 23, baada ya mchezo wa Jumamosi hii
watabakiwa na michezo minne tu kabla ya kumalizika kwa msimu. Baada ya
timu yake kuishinda Mwadui FC wiki mbili zilizopita kocha wa Mtibwa,
Mecky Mexime alisema kwamba ‘wanacheza ligi ili kupata kipato tu cha
kuendeshea maisha yao kwa kuwa ligi inachezeshwa katika utaratibu mbaya
kwa baadhi ya timu.
Mtibwa haitakuja kushindana na Yanga bali itakuja kukamilisha ratiba
na kucheza mchezo wao. Mecky tayari alishasema hilo wiki kadhaa
zilizopita na mtazamo wake huo ndiyo unanifanya niamini Yanga watashinda
na kurejea kileleni kwa kuwa wao wanashindania ubingwa na itawabidi
wapambane hadi siku ya mwisho ya msimu kutimiza malengo yao. Yanga
kuifunga Mtibwa mara mbili mfululizo itakuwa ni rekodi mpya na ngazi yao
nzuri kuelekea juu ya msimamo.
COASTAL V JKT RUVU
Kikosi cha King kinakwenda Tanga kikiwa na rekodi ya kutoshuka daraja
tangu walipopanda mwaka 2002. Ushindi utawafanya JKT Ruvu kupanda hadi
nafasi ya 11 na kuwapeleka Toto Africans nafasi ya 12 (timu zote
zitakuwa na alama sawa 27 ikiwa JKT Ruvu itashinda dhidi ya Coastal.)
Kupoteza mchezo huu kwa Coastal itakuwa ni sawa na kuanza safari yao
katika ligi daraja la kwanza msimu ujao. Pointi 19 walizonazo na 12
wanazoposwa kuzikusanya katika game zao nne za mwisho itawafanya vijana
wa kocha Ally Jangalu kufikisha alama 31-pointi ambazo hata kihesabu
zinawanyima nafasi ya kucheza VPL msimu ujao.
Stand Unite tayari wana alama 34, Majimaji FC wana pointi 33, wakati
timu za Ndanda SC na Mbeya City FC zenyewe tayari zimekusanya pointi 30
kila timu. Toto, Kagera Sugar, JKT Ruvu, JKT Mgambo, na African Sports
ndiyo timu pekee zisizofikisha alama 30 hadi sasa.
Coastal tayari wamechelewa lakini wanaweza kujaribu kushinda game zao
zote nne zilizobaki ili kusubiri atma yao mwisho wa msimu. Sare au
matokeo ya kupoteza mchezo dhidi ya JKT Ruvu yatawashusha daraja japo
haitakuwa rasmi.
SIMBA V TOTO
Mechi ya kwanza baina ya timu hizi ilimalizika kwa matokeo ya sare ya
kufungana goli 1-1 katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. Simba
wanafahamu jinsi timu hiyo ya Mwanza inavyowasumbua kila wanapokutana,
na ili kuendelea kugombea ubingwa kikosi cha Jackson Mayanja kinapaswa
kushinda game hii siku ya Jumapili katika uwanja wa Taifa.
Toto inayoundwa na wachezaji wengi vijana waliopata kufanya vizuri
katika timu ya Simba B itakuwa ikicheza mchezo wake wa 27 wa ligi, pia
itacheza na Yanga wiki chache zijazo.
Kushindwa kupata walau alama moja dhidi ya Simba watakuwa
wamejipeleka katika ‘shimo’ hivyo watalazimika kupambana kwa kuamini
pointi moja katika kila mchezo ulio mbele yao ina faida kubwa kama
hawatapata ushindi. Hii itakuwa mechi nyingine kali wikendi hii.