Friday, 16 December 2016

Utafiti wa NIMR Wagundua watu 83 waliougua ugonjwa wa zika Nchini



Watu 83 hapa chini wamegundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa zika kati ya watu 533 waliochukuliwa sampuli za damu hapa nchini Tanzania.
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini (NIMR) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Bugando, umeonyesha kuwa watu hao walipata maambukizi hayo kati ya mwaka 2015 na mwaka 2016.
Wakati NIMR ikitoa ripoti yake ya utafiti kuhusu kugundulika watu waliokuwa na virusi vya zika nchini, Januari 31 Serikali ilitoa taarifa kukanusha kuwapo kwa ugonjwa huo nchini.
Taarifa hiyo iliyotolewa kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilitaarifu: “Kumekuwepo na taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari vya kitaifa na kimataifa kuhusu Homa ya Zika ambao ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi kijulikanacho kama “Zika Virus”.
“Ugonjwa wa Homa ya Zika bado haujaingia Tanzania. Wananchi waondoe hofu juu ya uwepo wa ugonjwa huu. Hata hivyo, ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya zika, dengue na malaria ambayo huenezwa kwa namna inayofanana.”

Jana, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk Mwele Malecela alikutana na waandishi wa habari kueleza ripoti ya utafiti wao ikionyesha zika ipo Tanzania na wanaendelea na utafiti kujua ukubwa wa tatizo.

“Utafiti huu ulifanyika kuanzia mwaka 2015 hadi 2016 katika mikoa nane, ambapo jumla ya sampuli 533 za damu zilipimwa na kati yao, watoto wachanga 80 walizaliwa na ulemavu wa viungo mbalimbali ambapo baada ya kufanya utafiti tulibaini asilimia 43.8 ya watoto hao wachanga walikuwa wameambukizwa virusi vya ugonjwa wa zika katika mikoa hiyo,” alisema Dk Malecela.
Aliitaja mikoa iliyofanyiwa utafiti huo kuwa ni Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Geita, Kigoma, Tabora, Singida na Morogoro na kwamba bado taasisi hiyo na Chuo Kikuu cha Bugando wanaendelea na utafiti huo ili kujua ukubwa wa tatizo hilo katika mikoa hiyo.
Dk Malecela alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja ambapo alisema kati ya watu 533 waliopimwa, watu 83 sawa na asilimia 15.6 waligundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa zika na hivyo kupatiwa matibabu ya haraka. “Kwa wale watoto wachanga 80 waliozaliwa na ulemavu, asilimia 43.8 walikuwa wameambukizwa virusi vya zika na mpaka sasa bado tunaendelea na utafiti kubaini ukubwa wa tatizo hili na kuchukua hatua za haraka,” alisema Dk Malecela.
Alisema kwa sasa wanaendelea na utafiti katika mikoa hiyo kwa wanawake waliopata matatizo ya kuharibika kwa mimba ili kujua ukubwa wa tatizo hilo.
Dk Salvatory Florence kutoka Idara ya Magonjwa ya Watoto ya Hospitali ya Hubert Kairuki alisema ugonjwa huo hauna tiba ni kama ugonjwa wa dengue ulivyo ambapo mgonjwa anapaswa kunywa maji mengi.
Dk Florence ambaye pia ni Mhadhiri Chuo cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki, alisema wajawazito wa miezi mitatu wapo katika hatari ya kuzaa watoto wenye matatizo ya mtindio wa ubongo na watoto wenye vichwa vidogo (microcephalus) endapo wataambukizwa virusi hivyo kupitia kwa mama zao.
“Zika ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi kijulikanacho kama “Zika Virus na unaenezwa na mbu aina ya Aedes ambaye huwa ana tabia ya kuuma asubuhi na pia nyakati za mchana na wakati mwingine jioni,” alisema Dk Florence.
Pia, utafiti wa Nimr ulionyesha kuwa waendesha bodaboda katika mkoa wa Dar es Salaam, wapo hatarini kupata virusi vya Ukimwi.
Utafiti huo uliofanyika katika jiji hilo Agosti mwaka huu, umeonyesha kuwa licha ya madereva hao wa pikipiki kuwa na maambukizi madogo ya VVU kwa asilimia 2.5, bado wapo hatarini kutokana na kuwa na wapenzi wengi huku wengi wao wakigoma kutumia kinga.

No comments: